Tanzania kinara wa amani zaidi Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Tanzania imetajwa kuwa nchi yenye amani zaidi Afrika Mashariki kwa mwaka 2025, kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Global Peace Index (GPI)iliyotolewa na Taasisi ya Uchumi na Amani (Institute for Economics and Peace – IEP).
Katika viwango hivyo vya mwaka huu, Tanzania imeshika nafasi ya 73 kati ya nchi 163 zilizopimwa duniani, na kuongoza ukanda wa Afrika Mashariki mbele ya Rwanda (91), Uganda (113), Kenya (127), Burundi (133), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (160) na Sudan Kusini (161).
Ripoti hiyo, ambayo huchapishwa kila mwaka na IEP yenye makao yake makuu Sydney, Australia, hupima hali ya amani duniani kwa kutumia viashiria 23, ikiwemo usalama wa kijamii, kiwango cha migogoro ya ndani na ya kimataifa na hali ya kijeshi katika nchi husika.
Licha ya kushuka kwa nafasi nane kutoka nafasi ya 65 mwaka 2024, Tanzania inaendelea kushikilia sifa yake kama mojawapo ya mataifa tulivu zaidi barani Afrika huku ikiongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa miongo kadhaa Tanzania imekuwa ikisifika kwa ustahimilivu wa kisiasa, mshikamano wa kijamii na utulivu wa ndani usiotetereka sana hata wakati wa misukosuko ya kisiasa au kiusalama inayolikumba eneo la Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika.
Ripoti hiyo ambayo kwa mwaka huu ilizinduliwa katika Ubalozi wa Australia jijini Nairobi ilieleza kuwa matumizi makubwa ya jeshi yanaendelea kuathiri amani barani Afrika. Mwaka 2025, nchi 23 kati ya 44 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zimeshuhudia kushuka kwa alama zao.
Pia inabainisha kuwa amani duniani imeendelea kudorora, huku ikiwa ni mara ya 13 katika kipindi cha miaka 17 ambapo hali ya amani imekuwa ikishuka kwa kiwango kikubwa. IEP inataja sababu kubwa kuwa ni mivutano ya kijeshi na kisiasa, ongezeko la ghasia za ndani na migogoro ya kikanda.
Iceland, Ireland, New Zealand, Austria na Uswisi ndizo nchi zilizoorodheshwa kuwa na amani zaidi. Nchi zisizo na amani zaidi ni pamoja na Tajikistan, Jamhuri ya Dominika, Tunisia, Guinea ya Ikweta na Urusi.
Kenya yaporomoka, Rwanda yashikilia nafasi ya pili EAC
Kwa upande wa mataifa mengine ya Afrika Mashariki, Kenya imeporomoka kwa nafasi 18 kutoka ya 109 hadi 127, hali inayotajwa kuwa ni matokeo ya migogoro ya kisiasa ya ndani, maandamano ya mara kwa mara na changamoto za kijamii zinazokabili taifa hilo.

Rwanda imeshika nafasi ya pili kikanda baada ya Tanzania, ikiwa ya 91 duniani, huku Uganda ikishika nafasi ya tatu (113), Burundi (133), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (160) na Sudan Kusini (161) ikifunga orodha ya mataifa saba ya Afrika Mashariki yaliyoorodheshwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Kenya, Jenerali mstaafu Robert Kibochi, alisema kwamba ingawa kuna vitisho halisi vya usalama, nchi zinahitaji kufikiria upya namna zinavyokabiliana na migogoro ya baadaye.
“Vita siku zote ni vya kutumia nguvu na kisiasa, lakini tabia yake hubadilika kutokana na teknolojia na jamii. Vita vya sasa vitahusisha silaha zinazoendeshwa na akili bandia, mashambulio ya mitandaoni na makampuni binafsi ya kijeshi, hali inayoyafanya kuwa hatari na yenye vurugu zaidi,” alisema.
Naye mchambuzi wa masuala ya usalama, Dk Hassan Khannenje, alisema kuwa Global Peace Index mara nyingi hufichua mahali ambapo amani inakosekana kwa sababu migogoro inaathiri kila mtu kwa ukaribu zaidi.
Dk Khannenje alionya kuwa bila hatua za pamoja, uongozi wa dunia utaendelea kushindwa, kama inavyoonekana kwenye jitihada zilizokwama za kuleta amani Haiti.
Hali ya Tanzania
Juni 27, 2025 akilihutubia Bunge Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia utendaji wa Jeshi la Polisi, alilipongeza kwa shughuli zake huku akilitaka kuongeza jitihada kukomesha matukio ya watu kupotea, yanayoripotiwa sehemu mbalimbali nchini.
Alisema kasi ya kuwabaini wahalifu na kuwafikisha mahakamani imeongezeka, huku akisema jambo ambalo halijafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani ambalo nalo linaendelea kufanyia kazi.
“Nalielekeza Jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kukomesha matukio ya watu kupotea. Natoa pongezi nyingi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya. Hatuna budi kutambua kwamba, uhalifu unaozuiliwa kwa jitihada za Jeshi la Polisi ni mkubwa kuliko unaofanyika,” alisema.
Kuhusu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alisema uimara na usalama wa mipaka ya Taifa ni matokeo ya jeshi hilo kutimiza jukumu lake la kulinda uhuru na mipaka ya nchi.