Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MJEMA: Sababu 10 za ‘kibongo bongo’ kwanini asilimia 50 ya wabunge hawatarudi 2025

Muktasari:

  • Ukiwasoma wataalamu wa Sayansi ya Siasa duniani wana kama sababu nane hivi za kwanini hili linatokea hata pale ambapo Mbunge amesimamia kikamilifu utekelezaji wa ilani, lakini “kibongo bongo”, kuna sababu kama kumi hivi.

Spika wa Bunge la 12 ambalo limefikia ukingoni, Dk Tulia Ackson anasema tathmini inaonyesha kila Bunge linapovunjwa na kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, asilimia 50 ya wabunge huwa hawarudi bungeni.

Ingawa Spika anasema tathmini inaonyesha ni asilimia 50 hivi, lakini tathmini nyingine huru zinaonyesha ni kati ya asilimia 50 hadi 60 huwa hawarudi na katika uchaguzi mkuu 2015 ni kama asilimia 60 hawakurudi na 2020 ni kama asilimia 50.

Ni jambo la kutafakarisha sana kwamba mbunge anawatumikia wananchi kwa miaka mitano tu, halafu wanamkinai. Kuna sababu.

Ukiwasoma wataalamu wa sayansi ya siasa duniani wana kama sababu nane hivi za kwanini hili linatokea hata pale ambapo mbunge amesimamia kikamilifu utekelezaji wa ilani, lakini “Kibongo Bongo”, kuna sababu kama kumi hivi.

Wanasayansi wa masuala ya siasa wanabainisha sababu kadhaa zinazofanya baadhi ya wabunge wasichaguliwe tena.

Hizi ni pamoja na ukosefu wa uwajibikaji kwa wapiga kura, kushindwa kutekeleza ahadi za chama na mabadiliko ya matarajio kuhusu tabia, mwenendo, kauli na mwonekano wa mbunge na wakati mwingine kuhama chama kilichomdhamini.

Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa, Edward Abbey anasema wanasiasa wetu hawawakilishi watu wanaowapigia kura, bali masilahi ya kibiashara au ya kisiasa ya wanaofadhili kampeni zao za uchaguzi. Hili tuliliona sana 2015 na tutaliona 2025.

Lakini wataalamu wa sayansi ya siasa wanataja sababu kama nane hivi za kwanini wabunge huwa wanahudumu kipindi kimoja au wanakataliwa na wapigakura walewale waliompa kura za kishindo katika uchaguzi uliomwingiza madarakani.

Moja ni kwamba wapiga kura wanaweza kuwa na hisia kuwa mbunge wao hakuwajibika ipasavyo kuwakilisha hoja zao lakini pili ni kwamba hawashirikishi wapiga kura wake, bali anakwenda bungeni na kutoa maoni yake kichwani.

Sababu nyingine ni mbunge anapojiingiza katika kashfa na kuharibu jina lake na nne ni pale wapiga kura wanatofautiana na msimamo wa mbunge katika masuala muhimu yanayogusa maslahi yao, na mbunge anasimama upande wa Serikali.

Hizo ni baadhi ya sababu za wataalamu wa sayansi ya siasa, lakini huku uraiani tuna sababu zetu za kibongo bongo na moja ni kwamba kama uliingia kwa kutumia mgongo wa mtu (God Father) na sasa hayupo, ujue utapigwa chini tu.

Mathalani, katika kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2020, kuna ‘redio mbao’ zinasema Bwana mkubwa ndio aliamua kila kitu na ndiye alikuwa na maamuzi ya mwisho jina gani lirudi hata kama hakuongoza kura.

Kwa waliorudishwa kwa haki kwa sababu walioongoza kuna madudu ya kimaadili waliyafanya, hiyo haina shida, lakini kama jina lako lilirudishwa kwa sababu ya ‘u-God father”, ujue wajumbe wanakusubiri kwa hamu huku ili wapindue meza.

Sababu nyingine ambayo hufanya wananchi wasimrudishe mbunge wao na hii si kwa CCM ni kwa vyama vyote vya siasa, ni pale mbunge anapopoteza mvuto kwa wapigakura wake kutokana na matendo yake ambayo yanamshushia hadhi.

Ukiacha sababu hiyo, kuna wabunge tangu wachaguliwe, kurudi kwao bungeni kumekuwa kwa nadra sana, hafanyi mikutano na wapiga kura wake yaani kwa kifupi huko bungeni anajiwakilisha mwenyewe na hoja ni zake si za wananchi.

Sababu nyingine ambayo inawatia hasira wapiga kura ni pale ambapo mbunge akisaka ubunge namba zake zinapatikana wakati wote, anapokea, kusikiliza na kutoa shauri, lakini akichaguliwa tu hapatikani na mwingine anabadili laini.

Kwa hiyo hapa anakuwa na laini mbili, moja ni ile aliyoitumia wakati wa kuomba kura kwa wananchi, ambayo sasa anaizima au kuiwasha kwa nadra asisumbuliwe na wapiga kura, na laini nyingine ni ya kuwasiliana na “waheshimiwa” wenzake.

Kuna sababu nyingine ambayo inaweza isiwe ya moja kwa moja lakini ni ukweli uliojificha kuwa wagombea ubunge huu wa majimbo na viti maalumu hasa hawa wa CCM hutegemea pia aina ya kiongozi aliyepo madarakani kwa wakati huo.

Mathalan, katika uchaguzi mkuu 2020 tulishuhudia mafuriko ya wasomi, kuanzia maprofesa, wenye shahada ya uzamivu (PhD), wenye shahada za uzamili (masters degree), wahandisi, wataalamu wa uhasibu wenye CPA na shahada ya kwanza.

Hii ni kwa sababu kwa uzoefu wa wateule wa Rais aliowateua kushika nafasi mbalimbali katika serikali kati ya 2015-2020, kwa sehemu kubwa walikuwa ni wasomi, kwa hiyo wahadhiri vyuoni walitoka na kukimbilia ubunge.

Lakini hali kwa sasa ni tofauti, tangu alipoingia Rais Samia Suluhu Hassan hivyo mwelekeo ule wa 2020 hauwezi kuwa sawa na wa 2025 na kuna hisia kuwa safari hii tunaweza kupata sura mpya za wabunge viti maalumu kutoka CCM.

Sababu ya mwisho ambayo kiuhalisia ilipaswa iwe ya kwanza, ni baadhi ya wabunge kushindwa kuitumia vyema ibara ile ya 63 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 katika kuisimamia na kuishauri Serikali katika mambo ya msingi.

Tungekuwa na Katiba ile iliyotokana na rasimu ya Tume ya Jaji Warioba, nina hakika wako baadhi ya wabunge wasingemaliza miaka mitano kwa sababu wangefurushwa na wapiga kura kwa kushindwa kuisimamia Serikali.

Baadhi wapo ambao waliunga mkono sera ambazo zinaenda kinyume na maslahi ya wapiga kura au kinyume na maslahi ya Taifa na wengine kushindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapiga kura wake.

Mathalan, wanaweza kuwaambia wapiga kura wao kwanini bunge halijawahi kutoa msimamo thabiti juu ya wimbi la vitendo vya kutekwa, kupotea na kuuawa kwa watu linaloendelea nchini, ni kwamba hawakuguswa kabisa na matukio haya?

Lakini kuna wabunge ‘wenzangu na mimi’ ambao waligeuka ‘mabubu bungeni’, hawa nao watamlaumu nani wakiwekwa pembeni? Yaani matatizo yote ya msingi waliyonayo watanzania, hawajaona hata moja ama mawili kuyasimamia?

Tunahitaji wabunge makini watakaowawakilisha vyema watanzania bungeni, tunataka wabunge watakaoguswa na matatizo yetu.

Tunahitaji muundo wa Bunge tofauti kabisa na Bunge la 12 ambalo kwangu mimi naliona lilisimama upande wa mhimili wa Serikali badala ya kuushauri na kuusimamia kwa niaba ya Watanzania. Kwa maneno mengine bunge lilipoa.

Ninajuliza sana, mbona wakati wa chama kimoja cha siasa tulikuwa na Bunge lililokuwa na wabunge machachari na walioibua hoja nzito na zenye mashiko? Nini kililipata Bunge hili katikati ya mfumo wa vyama vingi vya siasa lipooze hivi.

Ninatamani sana mhimili huu ufanye utafiti kidogo kwa kuwauliza Watanzania hata kupitia mitandao ya kijamii, waeleze kama walilikubali Bunge hilo kwa asilimia ngapi kuwa liliwasemea watanzania. Majibu yawe wazi kila mtu aone.

Sababu nilizozieleza, zinawasubiri kwenye sanduku la kura kama tutakuwa na uchaguzi wa haki, huru na unaokubalika na dunia itatikisika kwani hata hiyo asilimia 50 aliyoisema Spika Tulia inaweza kufikia hata 80 hawatarudi.

0656600900