Prime
Majaliwa aacha maswali matatu

Muktasari:
- Kassim Majaliwa ameungana na Fredrick Sumaye kuwa miongoni mwa mawaziri wakuu walioongoza kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo, wengine tisa waliongoza chini ya miaka hiyo
Dar/Lindi. Nini kimetokea hadi Kassim Majaliwa kutangaza hagombei tena ubunge wa Ruangwa, je nani atakuwa Waziri Mkuu wa 11 na yeye atafanya nini?
Haya ni baadhi ya maswali ambayo yameibuka saa chache baada ya Waziri Mkuu, Majaliwa kutangaza uamuzi wa kujiweka kando na mbio za ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Saa 10:00 jioni ya leo Jumatano, Julai 2, 2025 ndiyo ilikuwa mwisho wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa wanachama wanaotaka kuwania udiwani na ubunge.
Matarajio ya wengi ni kwamba, Majaliwa angechukua fomu kuwaomba tena ridhaa wana Ruangwa, Mkoa wa Lindi wamchague kwa kipindi cha nne kama alivyolieleza Bunge siku saba zilizopita.
Juni 26, 2025, Majaliwa akilihutubia Bunge la 12 siku moja kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kulihitimisha, aliwashukuru wana Ruangwa kwa kumpa ushirikiano katika kipindi chote akiwa mbunge.
“Naomba Mwenyezi Mungu azidi kuimarisha mshikamano tulionao na naomba kuwajulisha nakuja kuchukua fomu na kuomba tena ridhaa yenu,” alisema Majaliwa huku akishangiliwa na wabunge.
Kauli kama hiyo aliitoa tena Septemba 13, 2024 katika mkutano wa Jimbo la Ruangwa alipoungumzia mafanikio ya utekeleza wa Ilani jimboni humo huku akimpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Watanzania.
“Hatuwezi kukaa kimya, lazima tumshukuru Rais Samia ambaye mimi kwa niaba yenu ninapokwenda kumweleza matatizo yenu hasiti kutupa mabilioni ya fedha…leo tunasisitizwa Samia mitano tena.
Lakini nataka kusema Samia mitano tena na mimi nauhitaji tena ubunge, nataka niendelee kuwatumikia, nataka niendelee kuwahudumia, nataka niendelee kuwawakilisha katika Bunge, nataka niendelee kuwasemea popote mtakapotaka niseme,” alisema Majaliwa huku akisisitiza kwa lugha ya kikwao.
Hakuna sababu iliyowekwa wazi juu ya uamuzi huo wa kuamua kuukacha ubunge kama alivyoutaka na kuthibitisha hadi bungeni. Alianza kuliongoza jimbo hilo tangu mwaka 2010.
Waziri Mkuu mstaafu na mbunge wa zamani wa Hanang mkoani Manyara, Frederick Sumaye amesema kila mtu ana uamuzi wake kwa alichokifanya Majaliwa ni jambo jema uamuzi mzuri.
"Ukiwa Waziri Mkuu unafanya mengi ndani ya Serikali, lakini ukiwa Waziri Mkuu ndiye mtendaji wa Serikali, sasa huwezi tena ukarudia tena ubunge ili kusimimamia Serikali ndio maana mimi niliachia," amesema Sumaye.
"Kwa kawaida ukiwa Waziri Mkuu na muda ukaisha wa miaka 10 jimboni kwako wanatamani uendelee kwa sababu wanajua wananufaika. Hata mimi waliniambia nikawaambia hapana naawaachia vijana," amesema Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu mwaka 1985-1995 katika utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa.
Nguli wa sheria na mwanasiasa, Profesa Abdallah Saffari amesema Majaliwa amekuwa muungwana kwa uamuzi wake huo, akisema:"Mimi ni msema kweli, namsifu Majaliwa maana kuna wengine hadi sasa bado wanagombea ubunge, lakini yeye ametangaza kutogombea tena.”
Hata hivyo, Profesa Saffari amependekeza kuwepo ukomo wa ubunge ili kupunguza wimbi la watu kuutaka kwa sababu wanaamini ndiko kwenye fedha nyingi za haraka kwa kuita 'peponi bungeni.'
"Au kuweka masharti magumu ili kuweka vikwazo kwa wanaotaka kwenda huko.Pia mapato ya bungeni yasitofautiane na maeneo mengine viongozi wengine wa umma," amesema.
Pia, ameshauri kuwa sifa za kuwa ubunge ziwe za juu na zenye tija ili kuondoa kila mtu kwenda bungeni, akisema lazima mhimili huo uheshimike na kuwa na watu wenye akili si kila mtu kwenda.
Juma Ali Khatib, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa amesema:"Nampomgeza Majaliwa kwa kuonesha mfano mzuri wa uongozi…amechukua uamuzi akiwa bado anapendwa na Watanzania kutokana na mfano mwema wa kazi zake katika kipindi chote cha utumishi.”
"Amepumzika ili kutoa nafasi kwa Watanzania wengine, aina viongozi kama Majaliwa wapo wachache duniani, angegombea angekuwa na uwezo wa kushinda tena kuanzia ndani ya chama chake, ila amepumzika," amesema.
Khatib amesema Majaliwa amepumzika akiwa bado ana nguvu ni vema wengine kufuata nyayo zake, akisema anavutiwa na mwanasiasa huyo kutokana na busara na uzalendo.
"Anayeweza kumrithi ni yule kiongozi mwenye kariba kama yake lakini hii itategemea na utashi wa Rais. Si lazima wafanane kwa sura lakini bali wafanane kwa uhodari na uchapa kazi," amesema.
Alichokisema Majaliwa
Hata hivyo, akizungumza na wajumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa na Wilaya ya Ruangwa leo Jumatano, Julai 2, 2025, Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa kumuunga mkono wakati wote ambao amekuwa mbunge wa jimbo hilo.
"Imefika wakati kwa mshikamano tulioujenga sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa wana Ruangwa wengine wapenda maendeleo, waweze kuunganisha nguvu hizi ili kaulimbiu yetu ya Ruangwa kwa maendeleo inawezekana iweze kusonga mbele zaidi."
Aidha, ametoa wito kwa wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya kuwapa ushirikiano wagombea wote wenye nia ya kugombea ubunge wa jimbo hilo.
Pia, amewasihi wana Ruangwa kuendelea kushikamana na itakapofika siku ya uchaguzi wachague wagombea wote watakaowakilisha Chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi huo.
"Viongozi wetu mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza Dk (Emmanuel) Nchimbi watakapokuja tujitokeze kwa wingi kwenye mikutano tusikilize sera, lakini siku ya kupiga kura tuwapigie kura nyingi za kutosha."
Aidha, amemshukuru Rais Samia, viongozi wakuu wa CCM kwa kumuamini na kumpa fursa ya kuwatumikia wana Ruangwa.
Je, Majaliwa atafanya nini?
Kiumri ndiyo kwanza ana miaka 64 akiwa mwenye nguvu. Duru za siasa zinaeleza huenda akapewa jukumu jingine hata la Ukatibu Mkuu wa CCM.
Hii inatokana na kwamba, Katibu Mkuu wa sasa, Dk Emmanuel Nchimbi alikwisha kupitishwa kugombea umakamu wa Rais. Nafasi itakayofanya kiti hicho kuwa wazi au Rais Samia anaweza kumteua kwenye nafasi zingine.
Nani Waziri Mkuu WA 11?
Kujiweka kando kwa Majaliwa na mbio za ubunge, kunatoa fursa kwa Rais Samia endapo ataibuka na ushindi kwenye uchaguzi ujao kuja na jina jipya la Waziri Mkuu wa 11.
Baadhi ya majina yameanza kutajwa tajwa kwamba iwapo wataibuka na ushindi wa ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wanaweza kuukwaa na kuwa wasaidizi wa karibu wa Rais Samia.
Miongoni wa wanaotajwa ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba.
Hawa wanatajwa huenda wakarithi nafasi ya Majaliwa. Dk Biteko ambaye ni Mbunge wa Bukombe, Mkoa wa Geita akitokea kanda ya ziwa, umakini na mienendo yake tangu akiwa Waziri wa Madini hadi sasa, anaweza kuwa chaguo la Rais Samia.
Lukuvi, waziri mwandamizi katika Baraza la sasa, amekuwa Munge wa Ismani Mkoa wa Iringa tangu mwaka 1995.
Ameshika wizara mbalimbali, huyu naye anaweza kuwa mtu sahihi iwapo Rais Samia akimpitisha kwenye chujio lake.
Dk Mwigulu ni miongoni mwa mawaziri ambao wamedumu kipindi chote cha utawala wa Samia.
Amewahi kujitosa katika mbio za urais mwaka 2015 ni mtaalamu wa uchumi na anaweza kuwa Waziri Mkuu wa 11.
Bashungwa, mbunge huyu wa Karagwe ni miongoni mwa mawaziri ambao wamezungushwa katika wizara nyeti. Amewahi kuwa Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Aliwahi pia kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Makamba ni mmoja wa wanasiasa vijana wenye ushawishi. Mwaka 2015 naye alikuwa miongoni mwa wana CCM waliofika tano bora kwenye mbio za urais na amekuwa waziri kwenye ziara mbalimbali.
Kuna kipindi, Makamba alitofautiana na Rais Samia lakini Februari 24, 2025, Rais Samia akiwa ziarani Tanga, alitangaza kumsamehe akisema:"Mwisho kabisa nataka nimwite mwanangu Januari (Makamba) hapa aje huku, arudi kwa mama. Sisi wamama mnatujua ukimkera mama anakupiga kikofi anakufichia chakula si ndio?"
Haikuwekwa wazi hasa Makamba alimkosea nini Rais Samia. Huyu naye anaweza kuwa chaguo sahihi la nafasi ya Uwaziri Mkuu.
Majaliwa ni nani
Kassim Majaliwa alizaliwa Desemba 22, 1960 katika Kijiji cha Mnacho, Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi.
Yeye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto watano. Ameuoa Mary Mbawala na wana watoto wanne, wavulana wawili na wasichana wawili.
Alisoma katika Shule ya Msingi Mnacho, iliyoko Mkoa wa Lindi, kuanzia mwaka 1970 hadi 1976.
Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari Kigonsera kuanzia mwaka 1977 hadi 1980 kwa masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne (O-level).
Mwaka 1981 hadi 1983 alihudhuria mafunzo ya ualimu Daraja ‘A’ katika Chuo cha Ualimu Mtwara.
Kati ya mwaka 1987 hadi 1989, alisoma katika Chuo cha Ualimu Butimba akichukua kozi ya Elimu ya Viungo, Michezo na Utamaduni.
Alihudhuria vyuo mbalimbali vinavyohusiana na michezo, vikiwamo Chuo Kikuu cha Jyvaskyla na Taasisi ya Michezo ya Pajulahti vilivyopo nchini Finland.
Baadaye, alisoma elimu ya sekondari ya juu (kidato cha tano na sita) kati ya mwaka 1991 hadi 1993 katika Chuo cha Ualimu Mtwara.
Kuanzia mwaka 1994 hadi 1998, alisoma Shahada ya Elimu (B.Ed) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 1999, alisoma Stashahada ya Uzamili (Post-Graduate Diploma) katika Taasisi ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Stockholm, nchini Uswidi.
Pia, alihudhuria kozi mbalimbali maalumu za michezo, hasa katika mchezo wa soka. Mwaka 1984, alihudhuria kozi ya awali na ya kati ya ukocha wa soka. Mwaka 1990, alihudhuria kozi ya juu ya ukocha wa soka.
Mwaka 1995, alihudhuria tena kozi ya juu ya ukocha wa soka pamoja na kozi ya Msaidizi wa Mkufunzi wa ukocha wa soka chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Pia, aliwahi kuhudumu kama Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), akihusika na sekta ya Elimu hadi mwaka 2015.
Kabla ya hapo, mwaka 2006 aliteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora, nafasi aliyoitumikia hadi mwaka 2009 alipopelekwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani.
Wasemavyo viongozi wa dini, wanaharakati
Askofu wa Kanisa la Anglikana dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosteness amemtaja Majaliwa kama kiongozi aliyeweza kuonesha uzalendo wa hali ya juu na uchapakazi ulioonekana dhahiri.
Amesema sababu hiyo ilimfanya kupendwa na watu wa hali zote hasa alivyoweza kuweka wazi mapenzi yake kwenye michezo hasa Klabu ya Simba.
“Kuna mengi ya kumzungumzia Majaliwa ama kwa hakika katika utendaji wake ameacha alama, kwanza alikuwa mzalendo, mchapakazi aliyeguswa na watu wa hali ya chini, kila alipokuta changamoto hakusita kuchukua hatua.
“Ni mtu mwenye uthubutu wa aina yake na kupenda kwake michezo kulimfanya ashuke zaidi kwa wananchi wa kawaida,” amesema Askofu Sosteness
Kuhusu aina ya Waziri Mkuu anayetarajiwa, amesema anapaswa kuwa mtu mwenye hekima, busara na atangulize uzalendo kwenye maamuzi yake.
“Tunahitaji kuwa na Waziri Mkuu mwenye kujali masilahi mapana ya Taifa na sio yake binafsi, na hii sio waziri mkuu pekee hata viongozi wengine tunataka wawe na uzalendo na kuangalia utaifa sio ukanda.
“Tunataka pia kuwa na mtu ambaye anaweza kusimamia mipango ya Serikali na utekelezaji wake na awe tayari kuchukua hatua pale ambo yatakavyokwenda ndivyo sivyo. Awe mtu anayesimamia nidhamu,”amesema.
Kwa upande wake, Askofu mstaafu Methodius Kilaini amesema Majaliwa alikuwa kiongozi aliyejiweka karibu zaidi na watu na alikuwa na usikivu wa hali ya juu.
“Nimesikitika sana kusikia anaondoka, alikuwa msikivu licha ya unyeti wake alikuwa anafikika na anakusikiliza unachomwambia. Kwetu viongozi wa dini tumefanya naye kazi na alikuwa tayari kutoa ushirikiano kwa dini zote bila kikwazo chochote.
“Licha ya kuwa sehemu ya awamu mbili tofauti za uongozi alijitahidi kwenda sawa na kila awamu kwa kifupi ni kiongozi wa aina yake nafikiri bado aliendelea kuhitajika,” amesema Askofu Kilaini.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amemtaja Majaliwa kama kiongozi msikivu na mpatanishi aliyetaka kuona wakati wote watu wanakuwa pamoja.
“Uwaziri mkuu wake haukuwa wa makeke bali utendaji. Alikuwa na misimamo hakuwahi kumuonea aibu mtu pale alikuta mambo hovy, alikemea na kuchukua hatua. Uamuzi wake wa kung’atuka kwa hiari ni ustaarabu katika siasa, wanasiasa wanapaswa kujifunza kutoka kwake,” amesema.
Kuhusu Waziri Mkuu ajaye, Sheikh Mataka amesema kwa hali ilivyo sasa anahitajika mtu mwenye uwezo mkubwa katika utendaji kuliko kuzungumza na atakayekuwa tayari kuwa mtumishi wa umma na sio mtawala.
Akitoa maoni yake Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Kaanaeli Kaale amesema Waziri Mkuu huyo alikuwa kiongozi mchapakazi, mvumilivu na mstahimilivu na kuonesha uimara wake hata pale Taifa lilipota msiba mkubwa wa kiongozi mkuu aliyekuwa madarakani.
“Ni kiongozi mstahimilivu ukumbuke kwamba katika awamu ya kwanza aliyoingia madarakani kiongozi wake mkuu alifariki dunia lakini aliendelea kuonesha uimara wake katika kipindi hicho na hata alipoendelea na awamu iliyofuata bado bidii na uchapakazi wake ulionekana dhahiri,” amesema Dk Kanaaeli.
Mawaziri wakuu waliotanguliwa
- Rashidi Kawawa
- Edward Sokoine
- Cleopa Msuya
- Salim Ahmed Salim
- Joseph Warioba
- John Malecela
- Fredrick Sumaye
- Edward Lowassa
- Mizengo Pinga
- Kassim Majaliwa
- ….?