Polisi yawanasa watuhumiwa madai mauaji ya kijana kwa kipigo Geita

Geita. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limewakamata watu wawili akiwemo Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Liyobahika, Ferdinand Antony kwa tuhuma za mauaji ya kijana Enock Mhangwa, huku watuhumiwa wengine watatu wakiwemo mgambo wakiendelea kuwatafuta.
Taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi waliyoitoa leo Julai 4, 2025 ni kutokana na picha mjongeo inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha watuhumiwa hao wakiwa wamemfunga mikono Enock na kumpeleka porini na kuanza kumpifa kwa kutumia fimbo sehemu mbalimbali mwilini.
"Jeshi la Polisi lingependa kutoa ufafanuzi wa picha mjongeo ambayo inaonekana kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha kijana aliyefungwa mikono huku akipigwa kwa fimbo," imeeleza taarifa hiyo.
"Tukio hilo lilitokea Juni 26, 2025 hivyo, kutokana na kushambuliwa kwa kipigo, kijana huyo anayejulikana kwa jina la Enock Mhangwa alifariki dunia," imeeleza taarifa hiyo ya Polisi.
Jeshi la Polisi limesema tayari limewakamata watuhumiwa wawili wanaodaiwa kuhusika katika mauaji hayo, ambao mmoja ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Liyobahika na Hussein Madebe.
"Watuhumiwa wengine tunaendelea kuwatafuta akiwepo Mtendaji wa Kijiji cha Uyovu na mgambo wawili ambao wamekimbia.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa watu wenye tabia za kujichukulia sheria mkononi, waache kwani halitasita kuwakamata ili hatua za kisheria ziweze kuchukuwa mkondo wake kama itakavyo fanyika kwa hawa wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji hayo,"imeeleza taarifa hiyo ya Polisi.
Tukio kupitia video
Katika video fupi ya kwanza aliyoipakia kwenye mtandao wake wa Instagram, Mwanaharakati Godlistern Malisa imewaonyesha watuhumiwa hao wakiwa wamemfunga mikono marehemu Enock huku wakikimbia nao eneo linalodaiwa ni porini.
Video ya pili ilimuonyesha Enock akipigwa na watuhumiwa hao maeneo mbalimbali ya mwili wake huku mikono yake imefungwa akiomba msaada.
"Mzee nielewe mzee nielewe unaniua mzee, mzee nielewe," hayo ni maneno ya Enock akiwa chini amefungwa mikono huku akipigwa na fimbo maeneo mbalimbali mwilini.
Ameongeza "Mtaniua bure naombeni niwalipe jamani," ni kauli ya Enock inayosikika kwenye picha mjongeo iliyopo mtandaoni.