Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanne waliohukumiwa kwa kumuua mwanafunzi, aliyezikwa bila kichwa waachiwa

Muktasari:

  • Mwanafunzi huyo wa sekondari, Hosam Salum (18), alichinjwa na kuzikwa bila kichwa baada ya mwili wake kukutwa kwenye kichaka karibu na barabara ambapo alikuwa akitumia muda wake wa ziada kuendesha bodaboda kwa ajili ya kujipatia kipato

Arusha. Dosari za kisheria zimewaepusha adhabu ya kunyongwa hadi kufa watu wanne, waliokuwa wamehukumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora baada ya kukutwa na hatia ya kumuua aliyekuwa mwanafunzi wa sekondani, Hosam Salum (18).

Mwanafunzi huyo aliyekuwa akitumia muda wake wa ziada kuendesha bodaboda, alikutwa amefariki dunia na mwili wake ukiwa hauna kichwa ambapo alizikwa bila kichwa.

Mauaji hayo ya kutisha yalitokea kati ya Septemba 30, 2015 hadi Oktoba Mosi 2015, katika Kijiji cha Nzega mkoani Tabora, walimuua mwanafunzi huyo aliyekuwa ameazima bodaboda hiyo kwa ajili ya kujipatia kipato.

Walioachiwa huru ni Sanura Maganga, Selemani Said, Paulo Maganga na Juma Benard ambao awali Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Aprili 29,2022 katika kesi ya jinai namba 9/ 2022.

Hukumu iliyowaachia huru imetolewa Juni 30, 2025 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Rehema Mkuye, Dk Paul Kihwelo na Dk Ubena Agatho, katika rufaa ya jinai namba 186/2022 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Katika rufaa hiyo warufani hao walikuwa na sababu tisa ikiwemo Jaji alikosea kuwatia hatiani bila kuzingatia mlolongo wa ulinzi wa kielelezo cha kwanza na pili, Jaji alikosea kisheria kuwatia hatiani kulingana na kukiri kwa washtakiwa wenzake bila uthibitisho na kuwa kesi dhidi yao haikuthibitishwa bila shaka yoyote.

Nyingine ambayo mahakama hiyo ya rufaa iliizingatia ni kuhusu uwakilishi wa warufani wa pili na nne ambao waliwakilishwa na wakili mmoja wakati kulikuwa na mgongano wa kimaslahi baina yao.


Awali

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 10 na vielelezo sita ikiwemo kadi ya usajili ya pikipiki, ripoti ya uchunguzi wa kifo.

Shahidi wa kwanza, Thomas Malugu, ambaye ni dereva bodaboda aina ya SANLG iliyokuwa na namba za usajili  MC217 AFL, alimuazima Hosam (marehemu), lakini baadaye alibaini marehemu hayupo ambapo akishirikiana na wenzake walianza kumtafuta.

Alieleza kuwa Oktoba Mosi, 2015 shahidi wa nne, Hassan Haji ambaye ni mjomba wa marehemu, waliukuta mwili wa marehemu bila kichwa kwenye kichaka karibu na barabara katika kijiji cha Silimuka.

Shahidi huyo alieleza kuutambua mwili huo kwa nguo zake na asili ya kiarabu ya marehemu.

Shahidi wa tatu ambaye aliufanyia mwili huo uchunguzi, Mganga Msaidizi, Amos Richard aliyeufanyia uchunguzi Oktoba 2, 2015, alihitimisha kuwa chanzo cha kifo hicho ni kutokwa na damu nyingi kutokana na kukatwa shingo,ambapo  mwili wa marehemu ulizikwa bila kichwa chake.

Mwezi mmoja na siku kadhaa baadaye, Novemba 12, 2015 mrufani wa kwanza (Sanula), alienda kwa shahidi wa nne akiomba kurekebishiwa pikipiki mpya aliyokuwa nayo.

Shahidi wa nne alitilia shaka ombi hilo ambapo mmoja wa marafiki wa marehemu  aliyejulikana kwa jina la Khamis aliitaja pikipiki hiyo ndiyo marehemu alikuwa akiiendesha mara ya mwisho ambapp waliita polisi.

Shahidi wa 10, Sajenti Deus, alimkamata mrufani huyo wa kwanza kwa kukutwa na pikipiki ya wizi.

Shahidi wa saba, Sajenti George walianza uchunguzi ambapo mrufani wa kwanza alimtaja mrufani wa pili (Selemani) ndiye mmiliki wa pikipiki hiyo,ambaye alikamatwa nyumbani kwake na kofia nyekundu ilichukuliwa kama kielelezo.

Shahidi wa saba alirekodi maelezo ya onyo ya mrufani huyo wa pili, ambapo aliwataja warufani wa tatu na nne jambo lililosababisha kukamatwa kwao.

 Shahidi wa tano, John Kulwa alidai mrufani wa tatu ( Paulo), alimweleza kuhusu biashara ya pikipiki iliyoibiwa na kumuonyesha pikipiki hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na warufani wa kwanza na wa pili.

Shahidi wa sita, Lilian Shirima, aliyerekodi maelezo ya ziada ya mrufani wa pili, Novemba 13, 2015 ambayo yalipokelewa mahakamani kama kielelezo.

Mama mzazi wa marehemu ambaye alikuwa shahidi wa tisa katika kesi hiyo, Mwanne Haji, hakuwa na ushahidi mrefu zaidi ya kueleza mahakama kuwa Hossam(marehemu) alikuwa na umri wa miaka 18 na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari.

Aliieleza kuwa mtoto wake alikuwa akiendesha bodaboda katika muda wa ziada.


Utetezi

Katika utetezi wao warufani wote wanne walikana kumuua Hossam na kukana kufika katika Kijiji cha Silimuka siku ya tukio hilo,licha ya kukiri kufahamiana kupitia kazi zao za kufyatua matofali.

Sanura alikiri kwenda eneo la kazi la shahidi wa nne ambaye ni fundi pikipiki kuomba namba lakini alidai  kuvamiwa na kuteswa na polisi ili akiri makosa yake.

Warufani wa pili na tatu, walidai walikuwa nyumbani siku hiyo ya tukio na kuwa waliteswa na kulazimishwa kukiri.


Uamuzi

Mahakama hiyo baada ya kusikiliza pande zote mbili ilijiridhisha kuwa vipengele vyote vitatu muhimu katika kesi hiyo vilithibitishwa bila kuacha shaka na kuwa kifo kilithibitishwa na ripoti ya uchunguzi wa mwili.

Ilieleza kuwa hali ya kikatili ya mauaji hayo, haswa kukatwa kichwa kwa marehemu, ilionyesha wazi nia ya kusababisha kifo na kukataa utetezi wa warufani na kuwatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.


Rufaa

Katika rufaa hiyo warufani hao walikuwa na sababu saba za rufaa ikiwemo Jaji kukosea kuwatia hatiani bila kuzingatia mlolongo wa ulinzi wa kielelezo cha kwanza na pili, kukosekana kwa ushahidi wa Khamis.

Sababu nyingine ni kwamba maudhui ya kielelezo cha kwanza na sita hayakusomwa kwa lugha inayojulikana kwa warufani hao na kukubaliwa kama kielelezo mahakamani hapo.

Nyingine ni Jaji aliyesikiliza kesi hiyo alikosea kisheria kuwashikilia na kuwatia hatiani warufani kwa kuzingatia maelezo ya onyo ya mrufani wa pili  ambayo yalichukuliwa kinyume na kifungu cha 50(1) (a) na (b), na kifungu cha 57(1) (2) (a) (3) (a) (1) ya Kanuni ya Adhabu.

Nyingine ni Jaji alikosea kisheria kuwatia hatiani warufani hao kwa kuzingatia maelezo ya ziada ya mahakama ya mrufani wa pili, ambayo yalichukuliwa kinyume na Mwongozo wa Jaji Mkuu na kuwa kesi hiyo haikuthibitishwa bila kuacha shaka.

Katika rufaa hiyo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Emanuel Luvinga huku warufani wa kwanza na wa tatu waliwakilishwa na Kanani Chombala huku wa pili na nne wakiwakilishwa na Kelvin Kayaga.

Wakili Kayaga aliieleza mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji kulikuwa na ukiukwaji wa haki wakati wa usikilizwaji hasa uwakilishi kwa mrufani wanne kama inavyooneakana ambapo yeye na mrufani wa pili waliwakilishwa na wakili mmoja.

Alieleza kuwa kutokana na mgongano wa kimaslahi kati ya warufani haikuwa sahihi kuwasilishwa na wakili mmoja na kueleza kuwa kesi hiyo ilikiukwa kuanzia hapo kwenye hukumu na kuomba mahakama kubatilisha hukumu.

Aidha, aliieeleza mahakama kuwa kesi hiyo ikisikilizwa upya hakutakuwa na maslahi ya haki, kwani ukiukwaji wa taratibu za kesi na kutofautiana kwa ushahidi vinapaswa kutafsiriwa ili kuhakikisha inatendeka kwa warufani.

Wakili wa Jamhuri alikubaliana na hoja kuwa haki ya mrufani wa nne ya uwakilishi wa kisheria ilikiukwa.

Kuhusu udhaifu katika ushahidi, alikubali kwamba taarifa ya ziada ya mahakama ilikuwa na udhaifu kama ilivyowasilishwa na wakili wa warufani na kuomba ifutwe ila hakueleza kama inaweza kudumisha hatia ya warufani.

Wakili huyo alihitimisha kwa kuitaka Mahakama kutumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa (AJA) kubatilisha shauri na kuamuru kesi ianze na kila mrufani kuwakilishwa na wakili tofauti.


Uamuzi Majaji

Jaji Agatho amesema kuhusu uwakilishi wa mrufani wa pili na nne waliowakilishwa na wakili mmoja ambapo kupitia maelezo ya onyo na maelezo ya ziada ya mrufani wa pili, yaliwahusisha warufani wengine akiwemo mrufani wa nne.

Amesema hiyo ilisababisha ukiukwaji wa haki ya mrufani wa pili na kuwa mrufani wa nne asingeweza kumhoji mrufani wa pili na kuwa kwa kawaida, tungeweza kutumia kifungu cha 4(2) cha AJA na kubatilisha mwenendo wa mahakama ya mwanzo na kuamuru kusikilizwa tena, kama Wakili wa Serikali msomi alivyowasihi wafanye.

“Hata hivyo, kutokana na mazingira ya kesi na ushahidi uliorekodiwa, tunafikiri haki inahitaji tuzingatie suala la iwapo kusikilizwa upya ndilo chaguo bora zaidi ili kutimiza maslahi ya haki,” amesema.

Jaji Agatho amesema iwapo kesi hiyo itaamriwa kusikilizwa tena itatoa nafasi kwa upande wa mashtaka kuziba mapengo katika kesi yao, jambo ambalo kwa hakika litakuwa na madhara kwa warufani.

Baada ya kupitia mwenendo wa shauri hilo, sababu za rufaa na kusikiliza hoja za pande zote mbili majaji hao walikubaliana na sababu hizo zilizotolewa na warufani na kuwa kutokana na mapungufu hayo hawawezi kuamuru shauri hilo lisikilizwe upya.

Majaji hao waliruhusu rufaa hiyo na kuweka kando iliyotolewa dhidi ya warufani na kuamuru waachiliwe huru na kutoka gerezani.