Prime
Kutoka mipango, mauaji mpaka askari kunyongwa-4

Muktasari:
- Watu saba walishtakiwa kwa kosa moja la kumuua kwa makusudi, mfanyabiashara wa madini, mazao ya biashara na mavazi, Mussa Hamis, Mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
Dar es Salaam. Jana katika mwendelezo wa simulizi ya hukumu ya kunyongwa kwa polisi wawili kati ya saba mkoani Mtwara waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya muuza madini, tuliishia Mahakama ikikamilisha usikilizaji wa ushahidi wa pande zote.
Watu saba walishtakiwa kwa kosa moja la kumuua kwa makusudi, mfanyabiashara wa madini, mazao ya biashara na mavazi, Mussa Hamis, Mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
Tukio hilo lilitokea Januari 5, 2022, katika Kituo cha Polisi Mitengo, ndani ya Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gilbert Sostenes Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Charles Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara), Nicholous Kisinza (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara) na Marco Chigingozi (Mkaguzi Msaidizi).
Wengine ni John Msuya (Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara), Shirazi Mkupa (Mkaguzi Msaidizi) na Salim Mbalu alikuwa Koplo. Sasa endelea.
Baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mtwara kufunga ushahidi wa pande zote, mawakili kesi hiyo waliomba na wakakubaliwa kuwasilisha majumuisho ya hoja za mwisho za kesi hiyo.
Wakati upande wa utetezi ukijikita kuonesha udhaifu wa ushahidi wa upande wa mashtaka kuishawishi Mahakama kuwa Jamhuri imeshindwa kuthibitisha kesi yake na iwaone washtakiwa hawana hatia, Jamhuri ilijenga hoja kuishawishi kuwa imeweza kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa bila kuacha shaka yoyote.
Kila upande ulichambua ushahidi namna ulivyowagusa au ulivyoshindwa kuwagusa washtakiwa, huku ukirejea vifungu mbalimbali vya sheria zinazotumika kwenye kesi za jinai na kesi za rejea zilizowahi kuamuliwa na Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu kuhusu hoja husika katika kesi hiyo.
Mambo yaliyoibuliwa na washtakiwa
Washtakiwa wakati wakitoa utetezi wao, katika majumuisho ya hoja zao za mwisho kupitia kwa mawakili wao, waliibua mambo mbalimbali yakiwamo ya kisheria yaliyogusa msingi wa kesi hiyo.
Kwanza, mshtakiwa wa kwanza, Kalanje ambaye ni shahidi wa kwanza wa utetezi na mshtakiwa wa pili, Onyango, ambaye ni shahidi wa pili wa utetezi, walikana kuwepo eneo la tukio la mauaji Januari 5, 2022.
Kalanje alidai kuwa, mchana wa siku hiyo alikuwa katika Kituo cha Polisi Nanyamba akiwa na polisi wengine wakifundishwa jinsi ya kushughulikia dharura.
Kwa upande wake, Onyango alidai kuwa siku hiyo alikuwa katika Kituo cha Polisi Mtwara akitekeleza majukumu yake.
Pia, Kalanje aliibua hoja ya kasoro ya hati ya mashtaka akidai kuwa, haijabainisha muda wa kutendeka kwa kosa hilo.
Wadai kituo cha polisi ni hewa
Vilevile Kalanje, Onyango, mshtakiwa wa tatu Kisinza aliyekuwa shahidi wa tatu wa utetezi na mshtakiwa wa sita, Mkupa aliyekuwa shahidi wa sita, katika utetezi wao waliibua hoja nyingine ya kisheria.
Walidai kuwa, jina la Kituo cha Polisi Mitengo (mauaji yalikofanyika) halijaoneshwa kwenye kanuni za mwongozo wa utendaji wa Jeshi la Polisi (PGO).
Hoja hiyo ilisisitizwa na mawakili wa Kalanje, Wakili Majura Magafu na wakili wa Onyango, katika majumuisho ya hoja zao za mwisho.
Mawakili hao walidai kuwa, mujibu wa PGO 13, hakuna Kituo cha Polisi Tanzania au Mkoa wa Mtwara, kinachoitwa Kituo cha Polisi cha Mitengo.
Hivyo, walidai kuwa mauaji yalitokea katika kituo kisichokuwepo kisheria, kwa hiyo waliona kuna utofauti kati ya hati ya mashtaka na ushahidi uliotolewa.
Waliongeza kuwa, kwa kuwa upande wa mashtaka haukufanya marekebisho kwenye hati ya mashtaka, hati hiyo ina dosari kubwa na tiba yake ni kufuta mashtaka kwa kuwa kasoro hiyo iliathiri uwezo wa washtakiwa kujitetea ipasavyo kutokana na utata wa eneo husika.
Vilevile mawakili wa washtakiwa wa kwanza na wa pili walidai kuwa, hakuna ushahidi madhubuti unaothibitisha kuwa Mussa amefariki, kwa kuwa chanzo cha kifo hakikubainika.
Msingi wa kesi ya upande wa mashtaka
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwaita mashahidi 28, lakini kati ya mashahidi hao wote, hakuna shahidi aliyetoa ushahidi wa moja kwa moja kwamba alishuhudia tukio la mauaji ya Mussa.
Badala yake kesi ya upande wa mshtaka ilijengwa zaidi katika ushahidi wa mazingira, unaokubalika kisheria.
Hivyo, katika majumuisho ya hoja zake za mwisho, Jamhuri walikuwa na jukumu la kuionesha Mahakama kuwa ni kwa namna gani ushahidi huo wa mazingira umeweza kuwagusa washtakiwa kiasi cha kuwafanya wapatikane na hatia.
Ili kuishawishi Mahakama iwatie hatiani washtakiwa, upande wa mashtaka ulikuwa na wajibu kuonesha kuwa, ushahidi huo umethibitisha viini vikuu vitatu vya hatia ya kosa la mauaji ya kukusudia.
Viini hivyo ni kifo cha kisicho cha kawaida, washtakiwa ndio waliohusika na kifo hicho na tatu walitenda hivyo kwa nia ovu ama kwa kudhamiria.
Hoja za Serikali
Serikali katika majumuisho ya hoja zake hizo, ilianza kusema imethibitisha kwa ushahidi wa kiini cha kwanza cha shtaka, kuwa Mussa alifariki kifo kisicho cha kawaida.
“Mheshimiwa Jaji, kwa mujibu wa sheria ilivyo, kosa la mauaji linaweza kuthibitishwa kwa ushahidi wa mazingira hata bila ripoti ya uchunguzi wa maiti au kuwasilishwa mwili wa marehemu,”ilieleza Serikali.
Huu ni msimamo wa kisheria kupitia uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi baina ya Jamhuri dhidi ya Hamisi Said Luwongo Meshack na Mahakama ya Rufani katika rufaa ya John Dickson Ngongole dhidi ya Jamhuri (rufaa ya jinai namba 477 ya 2021), Mahakama ilisema:-
“…sababu ya kifo inaweza kuthibitishwa kwa mambo mengine mbali na ripoti ya kitabibu, kwani si sharti la kisheria kwamba sababu ya kifo lazima ithibitishwe kwa ripoti ya kitabibu,”mwisho wa kunukuu msimamo huo.
Katika rufaa ya Mathias Bundala dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 62 ya 2004 Mahakama ilibainisha pia kuwa: (wakanukuu uamuzi ulisemaje).
“Sio sharti la sheria kwamba, sababu ya kifo lazima ibainishwe katika kila kesi ya mauaji. Tunatambua utaratibu kwamb, kifo kinaweza kuthibitishwa kwa ushahidi wa mazingira hata bila kuwasilishwa kwa mwili wa mtu anayedaiwa kufa.
“Mheshimiwa Jaji, kumekuwepo ushahidi wa kutosha na unaozidi kiasi, kuthibitisha Mussa Hamis Hamis alifariki na kifo chake hakikuwa cha kawaida,”ilieleza Serikali.
Kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, Hawa Ally, ambaye ni mama mzazi wa marehemu, tangu Januari 5, 2022 Mussa alipopelekwa Mtwara kwa agizo la washtakiwa (polisi), hajamuona tena mwanawe.
Ushahidi sampuli za DNA
Aidha, shahidi wa kwanza alichukuliwa sampuli ya mpanguso wa mate kwa ajili ya uchunguzi wa mpangilio wa vinasaba (DNA).
Hili lilithibitishwa pia na shahidi wa 10, Abdallahi Kimuja, Shahidi wa tatu, Yustino Mgonja (aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara), wakati wa tukio na shahidi wa 17, Inspekta Adelina Adolf Ndyamkana.
Matokeo yaliyotolewa na Mkemia Mwandamizi wa Serikali, Fidelis Bugoye aliyekuwa shahidi wa tisa kwenye ripoti ya uchunguzi wa DNA (kielelezo cha tisa cha upande wa mashtaka) yanaonesha kwamba, vipande vinane vya mifupa vilivyopatikana eneo la tukio vilibeba alama za vinasaba vya mtu wa kiume.
Vinasaba hivyo vililingana kikamilifu na sampuli F ambayo ni mpanguso wa mate ya mama wa marehemu aliyekuwa shahidi wa kwanza ikionesha kwa vipengele 15 vya DNA kuwa ni mama mzazi wa marehemu.
“Mheshimiwa Jaji, hata bila ushahidi wa kisayansi, sababu ya kifo bado imethibitishwa kupitia ushahidi wa mshtakiwa mwenza John Msuya (mshtakiwa wa tano), ambaye chini ya kiapo aliieleza Mahakama hii jinsi marehemu alivyouawa na wenzake watano Januari 5, 2022 katika kituo cha polisi cha Mitengo,” wanaeleza upande wa Jamhuri katika wasilisho lao.
Vile vile ushahidi wa shahidi wa pili wa Jamhuri, Salum Abdallah Ng’ombo na shahidi wa 19, Said Bakari Mnali walisema hawajamuona marehemu tangu Januari 5, 2022 alipokwenda kituo cha polisi.
Kesho usikose uchambuzi zaidi wa ushahidi wa Serikali