Hizi hapa dalili za changamoto ya afya ya akili kwa mjamzito

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kina mama 10 katika 100 walio wajawazito wanapata changamoto ya afya ya akili duniani na 15 kati ya 100 waliojifungua wanapata hali hiyo.

Mwanza. Kukosa usingizi wakati wa ujauzito, kujilaumu, kuwaza sana, kula sana na wakati mwingine kutokula kabisa ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa dalili za changamoto ya afya ya akili kwa mjamzito.

Dalili hizo zimebainishwa leo Ijumaa Aprili 19, 2024 wakati wa kufunga mafunzo kuhusu changamoto ya afya ya akili kwa wajawazito na kina mama waliojifungua yaliyotolewa na Chuo Kikuu cha Aga Khan, Skuli ya Uuguzi na Ukunga jijini Mwanza.

Mratibu wa mafunzo kazini kwa wauguzi na wakunga kutoka chuoni hapo, Aminieli Usiri amesema changamoto hiyo isipowahiwa inaweza kuleta madhara kwa mtoto.

Amesema mjamzito anaweza kupata changamoto ya afya ya akili iwapo kwenye familia yake kuna historia ya watu kuwa na matatizo hayo, mabadiliko ya homoni, changamoto za kiuchumi, kuachwa au kutengwa na jamii.

“Visababishi vya dalili hizi, moja ni changamoto za kiuchumi pale mtu anapokuwa hana kazi, hana fedha, unakuta anapata mawazo ataishije, atamtunzaje mtoto, mwingine pia anaweza akawa amepata mimba bila kutarajia amekataliwa nyumbani au amekataliwa na wazazi wake.

 “Kwa hiyo vitu vikubwa ambavyo kwanza tutawapa ni msaada wa kijamii na matumaini kuwa wanaweza kujifungua vizuri lakini pia tunawasaidia namna gani wanaweza kujihusisha na shughuli za uchumi; wakijihusisha na shughuli hizo basi wanaweza wasipate mawazo ya kutunza watoto wao,” amesema.

Ofisa muuguzi huyo ameongeza kuwa changamoto ya afya ya akili kwa kundi hilo ni tatizo ambalo halijapewa kipaumbele, akidai Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa mapendekezo kuingiza huduma za afya ya akili kwa kina wajawazito na waliojifungua kwa sababu takwimu zinaonyesha kina mama 10 katika 100 walio wajawazito wanapata changamoto hiyo duniani.

“Lakini wawawake 15 katika 100 ambao waliojifungua wanapata pia changamoto hiyo. Nchi zinazoendelea tatizo hilo ni kubwa zaidi kwa kuwa kina mama wajawazito 15 wanapata tatizo la afya ya akili wakati waliojifungua wakiwa 19.8 katika 100,” amesema.

Amesema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo chuo hicho kimeamua kuwanoa wauguzi na wakunga 25 kutoka zahanati na vituo vya afya vya jijini Mwanza ili nao watoe elimu nzuri kwa kina mama hao, itakayowasaidia kuepuka tatizo hilo kabla na baada ya kujifungua.

“Tumewasisitiza wauguzi waelimishe jamii kwa kuhakikisha wote wanaohudhuria kliniki na wanaojifungua wanaelimishwa namna gani wanaweza kujikinga wasipate madhara makubwa ya changamoto ya afya ya akili, pia tumewasisitizia kuwa na lugha nzuri na za upole katika huduma za kliniki ni muhimu,” amesema.

 “Wito wetu tunaiomba jamii itoe dhana potofu kwenye suala zima la tatizo la afya ya akili kwa wajawazito badala yake tuwasaidie kabla na baada ya kujifungua,” amesema.

Ofisa Muuguzi na Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Aga Khan, Kisimbi Mressa amesema wajawazito wanakwenda vituo vya afya wakiwa tayari na changamoto ya afya ya akili, hivyo  wauguzi waache kupuuzia dalili za changamoto hiyo kwa kuwaona wana kiburi au jeuri.

“Mama mjamzito aanze kupewa elimu ya kujikinga na tatizo hilo pindi tu anapoanza kuhudhuria kliniki ili aanze kujichunguza mwenyewe na kupewa msaada,” amesema.

Akifunga mafunzo hayo, Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Diana Okoyi amewataka wauguzi na wakunga hao kutumia mafunzo hayo kwa vitendo kwa kuwasaidia wajawazito wenye changamoto hizo.