Kaya 902 zaachwa bila makazi Moshi

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye akikabidhiwa msaada wa magodoro na wadau mbalimbali kwa ajili ya waathirika wa mafuriko wilayani humo. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Baada ya kufanyika tathmini, imebainika zaidi ya kaya 902 zimeathiriwa na mafuriko ya mvua wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro baada ya mvua kunyesha usiku wa kuamkia Alhamisi Aprili 25, 2024 huku watu saba wakipoteza maisha wakiwamo wanne wa familia moja.

Moshi. Zaidi ya kaya 902 zimebainika kuathiriwa na mafuriko ya mvua wilayani Moshi, Mkoani Kilimanjaro baada ya kufanyika kwa tathmini ya awali.

Mafuriko hayo yalitokea juzi Alhamisi Aprili 25, 2024 baada ya kunyesha kwa mvua kubwa na kusababisha vifo vya watu saba wakiwemo wanne wa familia moja.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Aprili 27, 2024 na Mkuu wa Wilaya hiyo, Zephania Sumaye wakati akikabidhi misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa waathirika wa mafuriko hayo walioweka kambi katika Shule ya Sekondari Lucy Lameck.

Misaada iliyokabidhiwa ni vyakula na magodoro.

Sumaye amesema Serikali ya Wilaya itashiriki katika maziko ya watu hao saba waliopoteza maisha kwa kusombwa na mafuriko na wale walioangukiwa na vifusi vya nyumba Zao.

"Juzi tulipatwa na mafuriko makubwa yaliyoharibu mali na makazi ya watu na baada ya kufanya tathmini ya awali tumebaini jumla ya kaya 902 zimeathirika kwa kuingiliwa na maji yaliyoharibu kila kilichokuwemo ndani zikiwemo samani zote na vyakula," amesema Sumaye.

Amesema baadhi ya waathirika wamepatiwa hifadhi na ndugu, jamaa na marafiki zao na wale waliokosa hifadhi, Serikali imebeba jukumu la kuwaweka kwenye kambi na mojawapo ni hiyo ya Sekondari ya Lucy Lamack.

“Tuna waathirika 55 hapa Lucy Lameck, katika kambi nyingine Moshi vijijini tuna waathirika 102 ambao tumewahifadhi,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Amesema pamoja na Serikali kutoa misaada mbalimbali kwa waathirika hao, amewaomba wadau wengine kujitokeza ili kuwasaidia kwani bado wana uhitaji.

"Nitoe rai kwa wana Moshi waliopo mahali popote, janga hili limetukuta, hawa ni ndugu zetu kama ilivyo desturi yetu sisi Watanzania chochote tulichonacho tutoe, wanahitaji vyakula, mavazi, vifaa mbalimbali, kila anayeguswa na jambo hili afanye  lolote aweze kuchangia kwa namna yoyote inavyowezekana," amesema DC Sumaye

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya ametoa wito kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni wahame haraka ili kuepuka madhara zaidi yanayoweza kutokea .

Joyce Swai, ambaye ni miongoni mwa waathirika waliopo katika kambi hiyo, ameishukuru Serikali pamoja na wadau wengine waliojitokeza kuwapa misaada mbalimbali.

Swahaba Hamad, mmoja wa walioguswa na waathirika hao, amesema wamewiwa kutoa msaada wa magodoro kutokana na majanga yaliyowakuta.

"Tumekuja kuwatembelea wenzetu hawa waliopatwa na majanga ya mafuriko,  tumeona kidogo tulichonacho tuwape ili kiwasaidie, tukio hili lilinigusa na leo nimeleta magodoro 10 angalau yawasaidie," amesema Hamad.