Kiwanda cha Sukari Kilombero chakumbuka waathirika wa mafuriko

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya (wa nne kushoto) akipokea mfuko wa mchele kutoka kwa meneja mahusiano wa Kiwanda cha Sukari Kilombero, Victor Byemelwa. Msaada wa chakula chenye thamani ya Sh14 milioni uliotolewa kwa ajili ya waathirika wa mafuriko wilayani humo. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

Siku moja baada ya Waziri, Kassim Majaliwa  kutoa pole na kuzungumza na wananchi, uongozi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero nacho kimetoa pole kwa waathirika

Kilombero. Baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwataka wadau kuwasaidia waathirika wa mafuriko nchini, Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kimeitikia wito huo.

Kiwanda hicho leo Jumatano Aprili 17, 2024, kimetoa msaada wa vyakula tani sita wenye thamani ya Sh14 milioni kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea Mlimba, Ifakara na maeneo mengine ya wilayani humo.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya amesema kwa sasa hali imeanza kutengemaa na tayari waathirika wote wamesharejea kwenye makazi yao ya awali wanaendelea shughuli zao za kila siku.

Hata hivyo, Kyoba amesema msaada uliotoewa ni maharagwe tani mbili, unga tani mbili na mchele tani mbili utawafikia waathirika hao kwa utaratibu uliopangwa tangu awali.

Kyobya amesema tayari wameanza kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu Majaliwa aliyoyatoa jana Jumanne alipokwenda kuwapa pole wananchi wa Mlimba waliokumbwa na mafuriko.

Ametoa maagizo kwa kamati za maafa kuandaa maeneo ya kuwahifadhi waathirika wote wa mafuriko kama yatatokea tena.

Kyobya  amesema katika kutekeleza agizo hilo, yapo maeneo ambayo yameandaliwa kwa ajili ya tahadhari endapo yatatokea mafuriko na watu watapoteza makazi.

Pia, amesema tayari wameshatoa angalizo kwa wananchi wanaoishi kwenye mabonde kuhama katika hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha ili kuepuka madhara yasiwakute.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kwa sasa mvua zinazonyesha wilayani humo ni za wastani na pia maeneo mengi yaliyokuwa na maji yameanza kukauka.

Akizungumzia miundombinu ya barabara, amesema Wakala wa Barabara Tanzanaz (Tanroads) na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) wanaendelea na kazi ya kurekebisha maeneo yote korofi ambayo hayapitiki likiwamo la Mngeta ambalo barabara ilikuwa imekatika.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ameiomba Serikali kupitia mfuko wa maafa, iwapatie Sh1 bilioni Ili kufanya matengenezo ya Reli ya Tazara eneo la Mlimba.

“Uchumi wa wananchi wa Mlimba unategemea sana uwepo wa usafiri wa reli, kwa sasa usafiri huo unaanzia Mlimba hadi Dar es Salaam, tunaamini mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan atatusaidia kiasi hicho cha fedha,” amesema Malima.

Miongoni mwa maagizo aliyoyatoa Waziri Mkuu Majaliwa ni pamoja na kuwataka, Tazara, Tarura na Tanroads kuhakikisha wanafanyakazi usiku na mchana ili kurejesha hali ya usafiri wa treni uweze kuendelea kama awali.

Wakati huo huo, Wilayani Mvomero mvua zimeanza kupungua na waathirika wote wa mafuriko yaliyotokea wiki iliyopita wameanza kurejea kwenye makazi yao.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Linno Mwageni amesema Serikali imeshatoa tani saba za mbegu ya alizeti kwa ajili ya wakulima waliopata hasara baada ya mazao yao kusombwa na maji yaliyotoka Manyara na Wilaya ya Kiteto na kusababisha mafuriko kwenye mashamba yao.