Machumu: Sekta sita bado zina uwakilishi mdogo wa wanawake

Mkurugenzi wa Kampuni ya MwananchI Communications Ltd, Bakari Machumu akizungumza katika Jukwaa la nne la The Citizen Rising Woman lililofanyika Machi 8, 2024 katika ukumbi wa Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam leo.

Muktasari:

  • Wakati hadithi za wanawake 217 zikiandikwa tangu mwaka 2021 lilipoanza jukwaa la The Citizen Rising Woman, Sekta sita ambazo bado zina uwakilishi mdogo zameinishwa.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu amesema sekta sita nchini zinahitaji msukumo zaidi ili ziweze kupata uwakilishi wa wanawake ndani yake.

Ametoa kauli hiyo leo, katika ufunguzi wa jukwaa la nne la The Citizen Rising Woman lililofanyika jijini hapa, lililokwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yenye kaulimbiu isemayo 'Wekeza kwa Wanawake Uongeze Kasi ya Maendeleo'.

Machumu amesema mwaka huu MCL ililenga kuandika makala za kisekta lakini ilipata changamoto ya kupata uwakilishi wa wanawake kwa urahisi katika sekta za madini, nishati, kilimo, elimu, usafirishaji na ujenzi.

Amesema Sekta zote zilizokuwa zimependekezwa ni afya, kilimo, elimu, nishati, madini, utawala, usafirishaji, utawala, sheria, ujenzi, fedha, utalii na fedha lakini waliopatikana kwa urahisi walikuwa katika sekta za utalii, sheria, fedha, utawala na afya.

"Baadhi yao hawakuwa tayari kushiriki kwa kutoa hadithi zao, hii inaashiria kwamba sekta hizi sita za mwisho zinahitaji msukumo mkubwa zaidi," amesema Machumu.

Amesema tangu kuanza kwa jukwaa hilomwaka 2021, habari mbalimbali za wanawake zenye lengo la kuonyesha mchango wao katika uongozi na katika kuleta mabadiliko zimekuwa zikiandikwa.

Hilo lilienda sambamba na kuzitambua taasisi zenye mbinu, mikakati na sera madhubuti za kuwainua wanawake tangu kuanza kuandika habari hizo, michango mingi imepokelewa kutoka kwa wasomaji na wadau mbalimbali.

"Hadi leo hii Machi 8, 2024, tumeweza kuandika makala 217 kuhusu wanawake na jinsi gani taasisi zinawainua katika nafasi za uongozi," amesema Machumu.

Hilo limeenda sambamba na utoaji wa tuzo 35 kwa taasisi zenye mifumo ya kuwezesha wanawake na ambazo zina wanawake wengi kwenye nafasi za uongozi za kufanya maamuzi.

Amesema katika hili, wasomaji wamekuwa na kiu ya kutaka kufahamu kwa undani nini kinawezesha wanawake kufanikiwa katika taaluma zao na namna ambavyo wanaweza kujifunza kutoka kwa mifano hiyo ya kuigwa.

"Hivyo basi, The Citizen Rising Woman imekuwa namna mojawapo ya Kampuni ya Mwananchi kuongeza ubunifu zaidi katika kuwezesha ufikiwaji wa lengo namba 5 (usawa kijinsia) la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, ikitumia maudhui kama daraja linalounganisha wanawake wa Kitanzania na kuhamasisha mafanikio.

Katika hilo, MCL pia inakusudia kutayarisha kitabu cha makala zaidi ya 200 na imemwomba Rais Samia Suluhu Hassan aandike dibaji ya kitabu hicho na ikimpendeza akizindue.

 "Tunaahidi kufuata taratibu zote za kiofisi kuleta ombi hili kwako na tukibahatika na ikikupendeza uje kutuzindulia," amesema Machumu.

Hata hivyo, kutokana na kutambua kuwa ni vigumu kuandika makala kwa wanawake wote waliothubutu ndani ya siku 60, Jukwaa maalumu la wanawake mtandaoni lilianzishwa na Benki ya NMB ili kuhakikisha hata baada ya Machi, basi wanaendelea kujadiliana mtandaoni, kushauriana, kupata fursa za tenda, nafasi za kazi na kujifunza.Na pia makala zote zipo pale.

“Tunawashukuru NMB kwa kuamini wazo hili tangu mwanzo na kuungana nasi kutengeneza jukwaa hilo," amesema Machumu.

Amesema pia kampeni hii ya Rising Woman pia inatarajiwa kuzinduliwa Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) mwezi huu.