Mafuriko Rufiji hali yazidi kuwa mbaya, tahadhari yatolewa

Wananchi waliokumbwa na mafuriko eeo la Mohoro wakiwa wamejihifadhi shuleni.

Muktasari:

  • Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Pwani lawataka wananchi wanaoishi mabondeni maeneo ya Rufiji na Kibiti kuhama, huku kamati ya maafa ikiwataka wananchi  kuwa makini na wanyama wakali wakiwamo mamba.

Dar es Salaam. Mkuu wa Kitengo cha Maokozi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Naibu Kamishna Mkoa wa Pwani, Bashiri Mahadhi amesema kama mvua zitaendelea kunyesha katika Wilaya ya Rufiji na Kibiti wanategemea hali itakuwa mbaya zaidi.

Jeshi hilo pia limetoa  wito kwa wananchi kuhama kabla ya kukumbwa na maafa zaidi.

Mahadhi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Aprili 11, 2024 akiwa Rufiji ikiwa siku moja imepita tangu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutabiri uwepo wa mvua kubwa katika mikoa 14 ya Tanzania bara na visiwani kuanzia kesho Ijumaa Aprili 12, 2024.

Utabiri huo uliotolewa jana Jumatano Aprili 10, 2024 umebainisha mvua zinategemewa kunyesha kwenye maeneo ya Mkoa wa Dar es salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara, Rukwa, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Ruvuma na visiwa vya Unguja na Pemba.

“Athari zinazotegemewa ni mafuriko na kuathirika kwa shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo,” ulieleza utabiri huo.

Leo Alhamisi asubuhi, televisheni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) imezungumza moja kwa moja na Mahadhi aliyesema  kutokana na hali hiyo wameshawaambia wananchi wahame kwa hiari.

“Tunawaambia wahame kwa hiari hii sehemu ya Rufiji imezidiwa na mvua na kama wanaona wanaishi mabondeni au  eneo lao limezidiwa na maji ni muda muafaka kuhama kwa hiari.”

“Sehemu kubwa ya Mohoro imeathirika na maji ndiyo maana tumewahamisha. Mwanzo kabisa tuliwahamishia Shule ya Mohoro lakini kwa sasa tumewahamisha tena kuwapeleka kambi ya Lundondo tukipisha huduma za elimu kwa watoto wanaosoma ziendelee kutolewa kama kawaida.

“Hali ya shule ni sehemu salama na tuna imani huduma ya elimu itarejea, japokuwa TMA imeshatoa utabiri mvua itaendelea kuanzia Aprili 12 hadi 13 na kinachokuja hatukijui ila kwa sasa hivi hali ni nzuri,” amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Maafa kutoka Mkoa wa Pwani, Roselini Kimaro amesema katika tathmini waliyofanya halmashauri mbili kati ya Kibiti na Rufiji baadhi ya kata zake zimeathirika na mafuriko hayo.

“Rufiji inakata 13 hadi sasa hivi maji yamejaa kata 12 utaona mashamba, makazi na mali mbalimbali za wananchi zimeathirika na haya maji, lakini Kibiti kuna kata tano ambazo zimeathirika na maji zilizoko karibu na bahari kuna vijiji na vitongoji vimefunikwa na maji,” amesema.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Amesema wananchi wengi wa mkoa huo wanajihusisha na kilimo kama mtama, ufuta na mpunga lakini mashamba yote yameshafunikwa na maji na adha kwa wananchi ni kubwa.

“Tunashukuru Serikali kwa kutukimbilia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutuletea chakula pamoja na malazi katika halmashauri zote, pia  huduma nyingine zinatolewa na wadau na tumepewa boti mbili kwa ajili ya uokoaji,” amesema.

Kimaro amesema hadi sasa kiwango cha maji kinazidi kuongezeka na mawasiliano yamekatika baina ya kata na kata kutokana na uharibifu uliotokana na mafuriko hayo.

Tahadhari ya mamba yatolewa

Kimaro pia amesema kutokana na kusambaa kwa maji maeneo mengi kuna wanyama wakali kama mamba wanazagaa sehemu mbalimbali, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari.

“Mathalani Wilaya ya Kibiti kuna wananchi waliojeruhiwa na mamba kwa hiyo watoto wanapokwenda shule au kuvuka wanapaswa kuchukua tahadhari kwa kutoa taarifa mapema kama wameshindwa kutoka sehemu wanayoishi,” amesema.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata Muhoro, Hilda Kuboja amesema asilimia 75 ya eneo hilo limekumbwa na maji, mashamba na makazi ya watu yameathirika kutokana na mvua zinazoendelea.

“Tulianza kutoa tahadhari toka mwanzo na watu wote walioko mabondeni wahame kwa kushirikiana na Kamati za ulinzi na usalama wa kata pamoja na wilaya na mkoa,” amesema.