Mafuriko yafunga Barabara ya Morogoro-Dodoma

Muktasari:

  • Mvua zinazoendelea kunyesha nchini zimesababisha adha kubwa kwa wasafiri baada ya mafuriko kufunga Barabara ya Dodoma kwenda Morogoro kwa zaidi ya saa tano wilayani Kongwa.

Dodoma. Zaidi ya saa tano Barabara ya kutoka Dodoma kwenda Morogoro imefungwa kusubiri maji yaliyofunga barabara katika eneo la Mtanana wilayani Kongwa mkoani hapa kupungua.

Eneo la Mtanane liko katikati ya Kibaigwa na Mbande njiapanda ya kwenda Kongwa ambapo ni maarufu kwa nyama za mbuzi za kuchoma.

Kufungwa kwa barabara hiyo kunakuja siku ya pili baada ya kufungwa kuanzia saa 11.00 alfajiri hadi saa 7.00 mchana.

Hata hivyo hali hiyo ilirejea tena leo Jumatano, Januari 10, 2024, saa 8.00 mchana ambapo maji yalijaa tena na hivyo kusababisha gari zilizokuwa zikitoka Dodoma kuelekea Morogoro na Morogoro kwenda Dodoma kusubiri.

Hali hiyo iliweka msururu wa foleni ya magari kuanzia Gairo hadi Kibaigwa huku sehemu kubwa ikiwa ni malori ya mizigo na mabasi ya abiria yanayofanya safari zake ndani na nje ya Tanzania.

"Gari zetu zilizoondoka saa moja asubuhi Dar es Salaam zimeshindwa kupita hadi sasa," amesema mmoja wa madereva ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Mmoja wa wakazi wa Kibaigwa, Saida Shomari amesema changamoto hiyo ilianza saa 8.00 mchana baada ya mvua kunyesha kwa saa tatu mfululizo.

"Mimi nimeingia hapa dukani saa 8.00 mchana nasikia kuwa gari zimezuliwa kwa sababu ya maji hapo Mtanane (wilayani Kongwa)," amesema.

Hali hiyo imetoa fursa kwa wafanyabiashara wa chakula hasa wanaochoma mahindi, vitafunwa na vinywaji kuwauzia abiria wa magari yaliyokwama katika maeneo hayo.

Mmoja wa abiria wa basi la BM Coach,  Alfred Mwakatobe ameiomba Serikali kuchukua hatua za kudumu za kutatua changamoto hiyo ili isijirudie tena, kwa sababu wengi wa wasafiri wana shughuli wanazoziwahi wanapokwenda.

"Wengine wana wagonjwa, mikataba ya kibiashara wakienda tofauti na muda wanapoteza fedha nyingi na hata maisha kwa kuchelewa matibabu," amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martine Otieno amesema hatua walizochukua ni kuzuia magari yasipite hadi hapo maji yatakapopungua, ili kuepusha changamoto ya magari kusombwa na maji.

"Tulichofanya ni kuweka ulinzi ili kuhakikisha kuwa hakuna gari litakalopita hadi maji yatakapopungua ili kuepusha kuleta madhara yanayoweza kujitokeza ikiwamo magari kusombwa na maji yanayokatisha barabara," amesema Otieno.