Maganga wa CWT, wenzake waachiwa kwa dhamana


Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama cha walimu Tanzania (CWT) Japhet Maganga na wenzake tisa walikamatwa Februari 16,2024 wakidaiwa kufanya fujo katika mkutano wa Baraza Kuu la chama chao.

Dodoma. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha walimu Tanzania (CWT), Japhet Maganga na wenzake tisa wameachiwa kwa dhamana baada ya kukaa rumande kwa siku nne.

Maganga na wenzake Kizito Shuli, Alistida Ishengoma, Leonce Mwalatishi, Alphonce Mbasa, Costa Paulo, Hamis Mtundua, Hamisi Chinahova, Daud Mafwili na Kiyola Mahanya walikamatwa Februari 16,2024 wakidaiwa kufanya fujo katika mkutano wa Baraza Kuu la chama chao.

Watuhumiwa hao wameachiwa Leo Jumatatu Februari 18, 2024, saa 12 jioni kwa sharti la kuripoti kesho Jumanne katika kituo Kikuu cha polisi Dodoma saa 3:00 asubuhi ili kujua hatma yao.

Akizungumza nje ya kituo Kikuu cha polisi Dodoma, Wakili wa CWT, Leonard Haule anayewatetea watuhumiwa hao amesema watuhumiwa watajua makosa waliyokamatiwa kesho kwa sababu leo hawajatajiwa mashtaka yoyote yanayowakabili.

"Wameachiwa kwa sharti la kurudi tena kesho saa 3:00 asubuhi, hiyo kesho ndiyo tutajua kama watafikishwa mahakamani au wataachiwa moja kwa moja," amesema Haule.


Amesema mpaka wanaachiwa kosa linalojulikana ni la kufanya fujo kwenye kikao cha chama chao na kitendo cha kukaa mahabusu ya polisi kwa siku nne bila kuwekewa dhamana kinaonyesha kuwa tuhuma hizo ni za kisiasa na si za kisheria.

Watuhumiwa hao ambao hawakutaka kuzungumza baada ya kuhojiwa na mwandishi, wanatetewa na mawakili wanne wa chama cha Walimu Tanzania.


Alivyosimamishwa ukatibu mkuu

Itakumbukwa Februari 17, Rais wa CWT, Leah Ulaya alisema vurugu hizo zilijitokeza baada Maganga kutamka kwenye mkutano huo kuwa hana imani na yeye (Leah) kuongoza kikao kilichokuwa kikijadili sintofahamu ya yeye (Maganga) kunyimwa kibali cha kuendelea kufanya kazi CWT.

Alisema baada ya kutokea kwa tafrani hiyo ilikuwa ngumu kupima kila mtu alikuwa na hisia gani, hivyo vyombo vya usalama viliingilia kati ili kutuliza fujo hiyo na kuwakamata Maganga na wenzake tisa.

Hata hivyo, baada ya Maganga na wenzake kukamatwa na polisi kikao hicho kiliendelea na baraza hilo kutoka na uamuzi kuwa Maganga hawezi kuendelea kutumikia nafasi hiyo ya ukatibu mkuu wa CWT.

 “Imeona hivyo kuwa tayari mamlaka yake ya ajira ilishamtoa kwenye ajira yaani amefukuzwa kazi kwa mujibu wa barua ambayo tumeisoma (katika kikao), iliyotoka katika mamlaka yake ya ajira Temeke (Halmashauri ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam).


Kwa muktadha huo, baraza limeona halikuwa na haja ya kuendelea tena kunyamaza na limefikia uamuzi kuwa hawezi kuwa tena kuwa Katibu Mkuu wa CWT labda kutokee mambo mengine kadri itakavyokuwa mbele,” alisema Leah.


Sakata lilipoanzia

Januari 25 mwaka jana,  Maganga na Makamu wa Rais ,Dinna Mathaman na Rais wa CWT, Leah Ulaya waliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan waliteuliwa kuwa wakuu wa wilaya lakini ni Dinna pekee alikwenda kuapa kushika nafasi ya ukuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Leah aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita wakati Maganga akiteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera hawakwenda kuapa katika nafasi hiyo.


Oktoba mwaka jana uongozi wa Manipsaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ulitoa tangazo katika ukurasa wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kumtaka Maganga arejee katika kituo chake cha kazi.

Katika tangazo hilo, ilionyesha kuwa Maganga aliomba na kibali cha kuazimwa na CWT kwa mara ya Agosti 2017 kilichomalizika Septemba 30, 2020.

Aidha, Maganga aliomba nyongeza ya kibali cha kuanzima Juni Mosi mwaka 2020 na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi alimpa nyongeza Agosti 10 mwaka 2020 kinachoishia Septemba 30 mwaka huu.

Tangazo hilo linasema Maganga ambaye cheo chakle ni mwalimu mwandamizi, aliomba tena kibali cha kuazimwa kwa mara ya tatu lakini Katibu Mkuu Utumishi hajaridhia maombi hayo.



“Hivyo basi Mwalimu Japhet Maganga anapaswa kurejea kwenye kituo chake cha kazi mara moja Oktoba Mosi, 2023,” limesema tangazo hilo ni waajiriwa wa umma.

Hata hivyo, Desemba 5 mwaka jana uongozi wa Manispaa ya Temeke ulitoa barua ukieleza kuwa Maganga amesimamishwa kazi kwa tuhuma za utoro kazini, kukaidi na kukataa maelekezo halali ya viongozi wake.

Akijibu hayo, Desemba 7 mwaka jana Maganga alieleza kushangazwa na barua hiyo kwani yeye ni mwajiriwa wa mkataba wa kudumu wa CWT.

Maganga alisema kinachofanyika ni vita ya madaraja na walioondolewa kwenye uongozi.

Alisema yeye alikoma kupokea mshahara na marupurupu yote kwenye halamashauri ya Manispaa ya Temeke tangu Desemba 2017 baada ya kuajiriwa kwenye nafasi ya uhasibu Makao Makuu ya CWT.

“Unanisimamishaje kwa kazi ambayo sina haja nayo. Kama ni mtoro kazini, sheria inasema mtumishi akikosekana kazini siku tano, amejifukuzisha kazi. Mimi sijaripoti tangu waliposema Oktoba Mosi, wamalize kazi,”alisema.