Mahakama Kuu yatupilia mbali rufaa ya dhidi ya Gekul

Pauline Gekul

Muktasari:

  • Machi 21, 2024 Jaji Kamuzora aliisikiliza rufaa hiyo kwa kuanza kusikiliza hoja tatu za pingamizi la awali lililowasilishwa na mjibu maombi na baadaye akasikiliza hoja sita za rufaa zilizowasilishwa na Wakili Madeleka na kupanga kutoa hukumu leo. 

Babati. Mahakama Kuu Kanda ya Manyara imetupilia mbali rufaa iliyokuwa imefunguliwa dhidi ya Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul baada ya kukubaliana na hoja moja ya pingamizi kati ya tatu zilizowasilishwa na mbunge huyo.

Uamuzi huo umetolewa jioni hii na Jaji Devotha Kamuzora aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo iliyokuwa imefunguliwa na Hashim Ally.

Jaji huyo amesema Mahakama baada ya kupitia hoja za pande zote mbili kuhusiana na pingamizi hilo la awali, amekubaliana na hoja moja ya pingamizi hilo, kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza rufaa hiyo.

Amesema uamuzi wa hoja hiyo moja unatosha kumaliza rufaa hiyo kwa kuitupilia mbali na kwamba, haoni sababu ya kuangalia hoja nyingine mbili za pingamizi hilo la awali lililowasilishwa na mjibu rufaa.

Hata hivyo, Jaji Kamuzora ameeleza kuwa upande ambao haujaridhika na uamuzi huo unaweza kukata rufaa.

Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Peter Madeleka anayemwakilisha Hashim, amesema hawajaridhika nao na wanatarajia kukata rufaa Mahakama ya Rufani kuupinga.

Wakili Madeleka ameongeza kuwa wakikosa haki katika mahakama hiyo, watakata rufaa Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika.

Katika rufaa hiyo mrufani alikuwa na sababu sita za rufaa hiyo akipinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati kuifuta kesi  aliyokuwa amemfungulia mbunge huyo.

Baada ya kuwasilisha sababu hizo za rufaa ndipo mjibu rufaa, Gekul alipoibua pingamizi la awali akiiomba mahakamani hiyo iitupilie mbali rufaa hiyo, huku akibainisha hoja tatu zilizowasilishwa mahakamani hapo Machi 20, mwaka huu, siku moja kabla ya usikilizwaji wa rufaa na pingamizi hilo.

Sababu hizo za rufaa zilisikilizwa pamoja na hoja za pingamizi la Gekul, Machi 21, 2024, kisha Jaji Kamuzora akaahirisha shauri hilo hadi leo Aprili 15, 2024 kwa ajili ya uamuzi.

Machi 21, 2024 Jaji Kamuzora aliisikiliza rufaa hiyo kwa kuanza kusikiliza hoja tatu za pingamizi la awali lililowasilishwa na mjibu maombi na baadaye akasikiliza hoja sita za rufaa zilizowasilishwa na Wakili Madeleka na kupanga kutoa hukumu leo.