Makonda aitwa kamati ya maadili CCM

Paul Makonda

Muktasari:

  • Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemuita Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kwenye Kamati ya Maadili.

Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemuita Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kwenye Kamati ya Maadili.

Makonda anatarajiwa kufika mbele ya Kamati hiyo Jumatatu, Aprili 22, 2024 asubuhi na kukutana na wajumbe wa kamati hiyo.

Hata hivyo, Mwananchi inafahamu kuwa Makonda alitakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Aprili 20, 2024 majira ya asubuhi, lakini haikuelezwa sababu za kusogezwa mbele.

Barua ya wito wa CCM kwa Makonda haikueleza sababu za kumuita huku ikieleza kwamba, kuna masuala mbalimbali kati yake na wajumbe wanakwenda kujadili.

Lakini, wito huo huenda unahusishwa na kauli ya Makonda aliyoitoa wakati wa kumbukumbu ya miaka 40 ya kifo cha Waziri mkuu wa zamani, Edward Sokoine iliyofanyika Monduli, Arusha ambako Makonda alidai kuwa viongozi wakiwemo mawaziri wamekuwa wakilipa watu kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mitandao ya kijamii.

Makonda alitoa onyo kwa viongozi hao akisema kama wakiendelea atawataja hadharani na kwamba, hayuko tayari kuona Rais Samia akitukanwa.

Endelea kufuatilia mitandaoni yetu kwa taarifa zaidi.