Malisa: Mgogoro wa machinga unadhoofisha ukuaji Soko la Old airport

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa akizungumza na uongozi wa wafanyabiashara wa soko la Old Airport na Shirikisho la Umoja wa Machinga (Shiuma) ili kubaini chanzo cha mgogoro wao.

Muktasari:

  • Baada ya kuibuka mvutano baina ya uongozi wa machinga katika Soko la Old Airport na Shirikisho la Umoja wa Machinga Jiji la Mbeya (Shiuma), inadaiwa kuwa hali si shwari ya biashara sokoni hapo.

Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amewataka viongozi wa wafanyabishara wadogo (machinga) Jijini hapa kuweka tofauti zao pembezoni na kutumia uwekezaji wa soko la kisasa la Old airport kama tija ya kukuza maendeleo yao kiuchumi.

Hatua hiyo ya Malisa imekuja baada ya kuwepo na mgogoro wa viongozi wa soko hilo na Shirikisho la Umoja wa Machinga (Shiuma), hali aliyotaja kuwa inadhoofisha maendeleo ya soko hilo.

Akizungumza leo Jumatatu Aprili 15, 2024 katika kikao na viongozi hao, Malisa amesema amelazimika kuingilia kati mgogoro huo kwa kuzikutanisha pande zote mbil,i ili kutafuta suluhu ya kudumu.

Malisa amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huo wenye lengo la kuchochea uchumi na inapotokea migogoro, inaathiri ukuaji wa soko kwa wafanyabiashara  kushindwa kufanya kazi iliyotarajiwa na wafanyabiashara wanajikuta wakidhorota kimaendeleo.

“Nimelazimika kuingilia kati mgogoro huo kwa kukaa na pande zote mbili, ili kutengeneza mustakabali mzuri,  lengo ni kuona soko hilo linaleta tija kubwa na kuchochea uchumi wa kipato cha mtu na mapato ya Serikali, nitarejea tena ili kujua mmefikia uamuzi gani,” amesema.

Amesema viongozi wanapaswa  kuwaunganisha machinga  kwa kutumia fursa ya soko hilo lililojengwa na Serikali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wamachinga wa  Soko la Old Airport, Shadrack Mwamwenda amesema mgogoro huo unatokana na viongozi  wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (Shiuma) kuingilia uamuzi wa kufanya maboresho katika soko hilo.

“Changamoto iko kwa viongozi wa Shiuma, tunaomba Serikali kuingilia kati kwani  imewekeza soko la kisasa, lakini wafanyabiashara wengi wako nje, walioingia ndani ni wachache,” amesema.

Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa Shiuma, Jerry Mwatebele amesema kuna kasumba ya viongozi kujimilikisha maeneo  kinyume na utaratibu.

Amesema jambo hilo wao wanapingana nalo na sasa watakaa chini na kukubalina nini kifanyike, ili hali hiyo isiendelee.

Naye mfanyabiashara wa mitumba, Belinda Joel amesema uongozi wa Serikali unapaswa kutumia busara, ili soko hilo liwe kimbilio la machinga.