Mama asimulia ukuta ulivyodondoka na kuua watoto wake wanne

Silvanus Ndabwe (jirani) akionyesha nyumba upande wa chumba walicholala marehemu hao waliobomokewa na ukuta wa nyumba ya jirani.

Muktasari:

  • Mama atoa simulizi namna ukuta wa nyumba ulivyochukua uhai wa watoto wake wanne waliokuwa wamelala chumba kimoja, huku mtoto mwenye miaka tisa akinusurika

Dar es Salaam. "Sijui nimemkosea nini Mungu, amenipa adhabu kali inayoacha alama isiyofutika katika maisha yangu.”

Haya ni maneno ya Mariamu Julius, aliyoitoa wakati akisimulia jinsi ajali ya ukuta wa nyumba ya jirani ulivyodondokea kwenye nyumba yake na kuchukua uhai wa watoto wake wanne.

Amesema kama Mungu angempa kipawa cha kutabiri ajali hiyo kutokea au kuyafanyia kazi maneno aliyoyasema mwanaye, Stella Rujukundi wakati anakwenda kuwajulia hali basi angewaokoa na wangebaki hai.

“Mtoto wangu Stella aliniambia usiku hawakulala, walikuwa wanaota wanadondokewa na ukuta huo lakini baada ya kunieleza nikawasihi tumuombe Mungu, tumeamka salama ile natoka nilisikia kishindo kikali kugeuka wamefunikwa na ukuta.”

"Sasa Mungu amewachukua, ajali ya ukuta imechukua watoto wangu waliokuwa wananipenda na wakati mwingine kunipa faraja, kweli kifo ni fumbo gumu, watoto wa dada zangu waliokuja kunisalimia sasa kabla ya kurudi Mungu amewachukua sitawaona tena," anasimulia Mariamu huku akitokwa machozi na kushindwa kuendelea kuzungumza.

Tukio hilo linalomfanya mama huyo wa makamu kukumbwa na mazonge kiasi cha kushindwa kujua la kufanya lilitokea asubuhi ya jana Aprili 26, 2024 maeneo ya Tuangoma, Mtaa wa Goroka, Mkoa wa Dar es Salaam.

Amewataja waliofariki dunia ni Lidya Heza (21), Agnes Eliya (20), Stella Rujukundi (20) na Joyce Rujukundi (12) huku wengine saba wakinusurika wakiwa vyumba vingine.

Kudondoka kwa ukuta na kuwaangukia watoto watano ni kutokana na mvua kubwa zilizokuwa zimenyesha maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mkoani humo.

Amesimulia ukuta wa nyumba ya jirani uliangukia kwenye chumba hicho walicholala watoto wake watano kati yao ni hao wanne wamefariki dunia na aliyenusurika ni mtoto Rechael Rujukundi (9) anayesoma darasa la nne Shule ya Msingi Goroka.

Mariamu ambaye ni mama wa familia hiyo amesimulia usiku ya ajali hiyo nyumba nzima ilikuwa na jumla ya watu 11 lakini wengine walionusurika walikuwa wamelala vyumba vya jirani.

"Katika nyumba yangu hii iliyobomoka ilikuwa na vyumba vitatu na siku ya tukio ukuta uliangukia katika chumba walicholala mabinti zangu watano wote wa kike lakini amepona mmoja huyu Rechael wakati watu wanajitahidi kuokoa walimkuta akiwa juu ya chandarua," amesema.

Amesema katika vyumba hivyo chumba kimoja alikuwa amelala yeye na mumewe Sayon Rujukundi ambaye siku hiyo alikuwa amewahi kutoka kwenda kazini.

"Chumba kingine walilala watoto wanne wa kiume, wawili kati yao ni watoto wangu wengine walikuwa ni rafiki zao ambao huwa wanasoma nao," amesema.

Mariamu amesema katika hao, wanne waliofariki dunia wawili ni watoto wake wa kuwazaa ambao ni Stella na Joyce lakini waliobakia ni watoto wa dada zake walikuwa wamekuja kumsalimia kutokea mkoani Kigoma.

Mimi nilikuwa nasoma…

Wiliam Sayon ambaye ni mtoto wake anayesoma kidato cha nne shule ya Sekondari Mikwambe amesimulia siku ya tukio aliamka mapema alikuwa anasoma.

“Ghafla nikasikia ukuta unaanguka katika chumba walichokuwa wamelala dada zangu na walikuwa watano kati yao aliyepona ni mmoja dada yangu mdogo na kilichomsaidia matofali hayakufika sehemu aliyokaa,” amesema.

Wiliam amesema kilichotokea nyumba ya juu ilikuja kudondokea ukuta wa nyumba yao na tope zilianza kuingia na matofali yakafunika kwa juu.

“Hali ilikuwa ngumu kwa sababu matofali yalikuwa mazito kwa kuwa yalikuwa yameshiba maji baada ya kuona mzigo mzito tukaitisha majirani kutusaidia, tulitumia muda mrefu nahisi walizidiwa pumzi,” amesema

Jirani na shuhuda

Silvanus Ndabwe ni jirani na mmoja waliosaidia kuokoa baada ya ukuta kudondokea nyumba hiyo amesema wakati wanajaribu kuokoa waliikuta miili ya watoto hao iko ndani ya chandarua.

“Tulipambana kuwaokoa wadada waliokuwa wamefunikwa na kifuasi na matope yalikuwa yamejaa, vyombo vyote vilivyokuwa karibu vilikuwa vimevunjika,” amesema.

Amesema walianza kutoa udongo na matofali kufikia katikati walisikia sauti ya mtoto mmoja anasema:“Mtuokoe huku akilia (wakati sisi) tukiwa hatumuoni.”

Silvanus ambaye ni shemeji wa Sayona kutokana na kasi ya maporomoko ya udongo huo ilifikia hatua walizidiwa huku akieleza yalikuwa mazito na mvua ilikuwa inanyesha.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda akizungumza na Mwananchi Digital amesema mara baada ya kusikia taarifa za tukio hilo alikwenda kushirikiana na familia kuchukua miili kisha kuipeleka chumba cha hifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Polisi Kilwa Road na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho Jumapili, Aprili 26, 2024.

"Kama Serikali tumetoa majeneza yote manne na tumetoa ubani kidogo wa kusaidia shughuli ya mazishi," amesema Mapunda.

Sixtus aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbinga amesema mazingira ya tukio hilo  yamesababishwa na kudondokewa na ukuta wa nyumba iliyojengwa jirani na nyumba  waliyokuwa wanaoishi watoto hao.

"Kulikuwa na mtu aliyejenga nyumba juu kutokana na jiografia yake kuna kimlima hivi na huyo mtu alikuwa haishi hapo aliondoka muda mrefu sasa kutokana na mvua hizi ikadondokea nyumba waliyokuwa watoto hao na kusababisha madhara hayo," amesema.

Amesema baada ya hapo alipata fursa ya kuzungumza na wananchi wa eneo hilo akiwataka kuwa makini na mvua zinazoendelea kunyesha.

"Nyumba nyingi zinatitia ni muhimu wakaangalia nyumba zao wakiona mambo hayaeleweki wapishe kwa muda kulinda usalama wa maisha na mali zao," amesema.

Amesema mvua zikiendelea wahame maeneo hayo na wanapaswa kuzingatie suala la watoto kwenda shule na wakiona mvua kubwa wasiende au kurudi nyumbani.

"Wakiona mvua kubwa na watoto wako shule basi wasiwaache warudi peke yao wawafuate, wawasaidie katika hizo nyakati," amesema.