Mbunge atoa mbinu kwa wabunge kushughulika na wateule wa Rais

Mbunge wa Bunda Vijijini (CCM), Mwita Getere akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na taasisi zake kwa mwaka 2024/25 jana Jumatano, Aprili 24, 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Mbunge wa Bunda Vijijini, Mwita Getere ametoa ushauri kwa wabunge kuhusu kushughulikia viongozi wa uteuzi wa Rais, kama vile mawaziri, wanapohisi mambo hayakwendi vizuri.

Dodoma. Mbunge wa Bunda Vijijini (CCM), Mwita Getere amewashauri wabunge kuhangaika na wateule wa Rais wakiwemo mawaziri wanapoona mambo hayaendi sawa.

Getere ameyasema hayo jana jioni Jumatano Aprili 24, 2024, wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Waziri wa Nishati kwa mwaka 2024/25, yaliyowasilishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

Amesema anashindwa kufahamu watu aliowateua Rais Samia Suluhu Hassan na kuwaweka katika vitengo mbalimbali kama ni watu thabiti.

“Kama leo tunahangaika na matatizo ya umeme nchini tuhangaike na Doto, Rais amemteua Doto afanye hiyo kazi tuhangaike naye humu ndani.

Kama ni kilimo tuhangaike na Bashe (Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe) na kama Madini ametuteulia Mavunde (Anthony) kwa hiyo nachosema kama hawafanyi kazi, tuhangaike nao,” amesema.

Amesema kumekuwepo na lugha ambazo hazifanani kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).

Akitoa mfano, amesema kuna kipindi walikuwa wanasema mvua inanyesha lakini maji hayajai na hivyo kusababisha umeme kutozalishwa.

Lakini walipiga kelele na baadaye mvua ilianza kunyesha na baada ya muda mfupi maji yalijaa katika bwawa hilo.

Hata hivyo, amesema baada ya siku mbili walisema Bwawa la Mtera maji yamejaa yanaharibu mifumo ya umeme.

“Sasa maneno gani hayo, maji hayapo umeme hamna, maji yamejaa mifumo imeharibika kwa hiyo tuwe makini sana kwenye hili jambo la umeme.

Niombe Waziri wa Nishati na bahati nzuri Rais amekuteua na kukupa madaraka makubwa kwa hiyo huogopi mtu yoyote, wala hakuna anayekusogelea, angalieni watu wanaokaa kwenye vyanzo vikubwa vya umeme kwa mfano Bwawa la Mtera, la Mwalimu Nyerere kama wana muda mrefu katika maeneo hayo,” amesema.

Amemtaka kuangalia kama wanatenda kazi na iwapo hawatendi kazi basi wapunguzwe na kupelekwa maeneo mengine.

Getere amesema ni lazima wawe na lugha moja sio maji yajae umeme hamna, maji hayapo umeme shida.


Agusa uaibu waziri nkuu

Mbunge huto katika mchango aligusia hata cheo cha Dk Biteko: “Nilikuwa nawaza, hivi naibu waziri mkuu anapatikanaje, nikaangalia nikaona mwaka 1985 Ahamed Salim Salim alipewa, kumbe alipewaje. Kumbe kipindi hicho nchi ilikuwa na matatizo mengi kulikuwa na uchumi mgumu, akateuliwa kusaidia nchi,” amesema.

Ameongeza kuwa mwaka 1993, aliteuliwa Augustino Mrema kuwa naibu waziri mkuu ambapo kulikuwa na ujambazi wa kutupa, lakini akasaidia ukaisha na mambo yakaenda sawa.

“Sasa imekuja mwaka huu amepewa Doto amekuja wakati umeme ni shida kwenye nchi yetu. Kwa kipindi kifupi tumeona amepelekea mgawo wa umeme kupungua. Kumbe manaibu wanapewa kwa kazi maalumu. Nakuombea uifanye kazi hiyo,” amesema.


Tupate umeme

Aidha, amesema wamepewa matumaini wa kuwa vyanzo vingi vya umeme lakini wanachotakiwa kufanya ni kuwapa Watanzania uhakika wa upatikanaji wa umeme katika siku zijazo.

“Lazima mtwambie kuwa umeme umepatikana na unawake, sio kwamba tumezalisha mwingi halafu umeme unakatika kila siku. Mmetupa matumaini kwa hiyo mtupatie umeme,” amesisitiza.

Aidha, Getere amesema unavyoeleza kuwa vijiji vyote vina umeme ina maana ni vitongoji vilivyoko kati (center) ndivyo vilivyopata umeme na vitongoji vingine vyote havina umeme.

Ametaka kuangaliwa kwa jambo hilo kwa kuangalia wingi wa vitongoji kwenye kijiji.

Mapema, Dk Biteko akiwasilisha bajeti hiyo amesema moja ya kazi kubwa mbele yaoni kuhakikisha nchi inakuwa na umeme unaotosheleza mahitaji ya sasa na siku zijazo na ili kutimiza azma hiyo, wizara imepanga kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme kwa utumia Maji wa Julius Nyerere (MW 2,115) ambao uko katika hatua za mwisho mwisho.