Mchwa watajwa changamoto upandaji wa miti

Baadhi ya wadau wa mazingira wakiwa katika hafla ya makabidhiano ya mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Muktasari:

  • Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania, imekabidhi mradi wa kukabiliana na mabidiliko ya tabia nchi katika mikoa ya Pwani na Dodoma.

Dodoma. Mchwa waharibifu, mifugo inayozurura na gharama za uendeshaji hasa uchimbaji wa mashimo kwaajili ya kupanda miti, imetajwa kama changamoto kwenye mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, katika mikoa ya Dodoma na Pwani.

Akizungumza katika hafla ya kuufungaji wa mradi huo, Julai 21, 2023, Mratibu wa mradi huo, Savinus Kessy amesema: “Changamoto ya mchwa kuharibu miti na hasa nyakati za ukame, ilikuwa tatizo kubwa. Lakini pia mifugo inayozurura ovyo mitaani, nayo imesumbua.”

Mradi huo ulikuwa unatekelezwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), Vodacoma Tanzania kwa kushirikiana na halmashauri za Dodoma, Mkuranga na Kisarawe (mkoani Pwani).

Kampeni ya kijinaisha Dodoma ni sehemu ya mradi huo ambayo ilizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati huo akiwa Makamu wa Rais mwaka 2017 na kuwashirikisha pia wadau hao.

Kessy amesema moja ya mafanikio ya mradi huo licha ya changamoto mbalimbali walizokutana nazo, umefanikiwa kuliwezesha Jiji la Dodoma kupanda miti 70,000 kati ya miti 100,000 iliyokuwa imekusudiwa.

“Miongoni mwa changamoto ni uharibifu uliotokana na mifugo inayozurura ovyo mitaani na kusababisha miti iliyopandwa kuharibiwa,” amesema.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dunstan Shimbo amewataka waliokabidhiwa utunzaji wa miti kuhakikisha wanatafuta rasilimali nyingine katika kuwezesha uoto wa asili.

“Katika eneo la Medeli (mkoani Dodoma), Serikali inatamani kuona maono ya kupafanya kuwa msitu wa jiji na eneo la kupumzikia yanakamilika,” amesema.

Aidha, Shimbo amesema ufungaji mradi huo ni mwanzo wa kujadili changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji na namna ya kuzitatua ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana hayapotei wala kuharibika.

“Ni matamanio yangu kuona miti yote itakayokabidhiwa leo (jana), inakuwa na kuleta mabadiliko tuyatakayo ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani,” amesema.

Meneja wa Uhifadhi wa WWF, Dk Lawrence Mbwambo, amesema licha ya Tanzania kutokuwa na hali mbaya ya athari za mabadiliko ya tabia nchi, hatua za kukabiliana na janga hilo  ili kupunguza athari zinazojitokeza ikiwemo vipindi virefu vya ukame.

Amesema shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wameendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha nchi inafikia lengo la kurudisha uoto wa asili wa takribani hekta milioni 5.2 ifikapo mwaka 2030.

Naye Meneja wa Vodacom Foundation ambao ni wafadhili wa mradi huo, Sandra Oswald amesema wanatamani kuona miradi yote inaendelea kuleta matokeo chanya.

Amesema kampuni yake itaendelea kufadhili miradi mingine ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.