Miradi 177 yachunguzwa na Takukuru

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru,   Salum Hamduni, katika hafla iliyofanyika Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma jana. Picha na Ikulu   

Muktasari:

  • Ni miradi iliyobainika kuwa na utekelezaji hafifu wakati wa ukaguzi, uchunguzi ulilenga kubaini viashiria vya rushwa na ubadhirifu

Dodoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeanzisha uchunguzi wa miradi 171 yenye thamani ya Sh143.3 bilioni  iliyobainika kuwa na utekelezaji hafifu wakati wa ukaguzi.

Akiwasilisha taarifa ya Takukuru ya mwaka 2022/23 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, jana Machi 28, 2024, mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, Salum Hamduni, amesema ilifanya ufuatiliaji wa rasilimali za umma katika miradi ya maendeleo 1,800 yenye thamani ya Sh7.7 trilioni.

Amesema lengo lilikuwa kubaini viashiria vya uwepo wa rushwa na ubadhirifu, kuangalia kama thamani ya fedha inapatikana katika miradi na uzingatiaji wa makadirio ya vifaa.

Hamduni ameitaja baadhi ya miradi iliyofanyiwa ufuatiliaji kuwa ni barabara za mzunguko katika Jiji la Dodoma, miradi inayotekelezwa kwa ‘force account’ katika Halmashauri ya Jiji la Arusha na mradi wa ujenzi wa soko la kisasa la machinga lililopo eneo la Bahi Road, jijini Dodoma.

Takukuru pia, imefanya ufuatiliaji katika miradi 12 ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji yenye thamani ya Sh107.4 bilioni kwenye mikoa ya Morogoro, Dodoma, Iringa, Tabora na Mbeya.

“Matokeo ya ufuatiliaji yalionyesha uwepo wa mianya ya rushwa, baadhi ya miradi ilionekana kutosajili na Bodi ya Makandarasi, Wakala Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha), ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi uliosababisha uwepo wa riba,” amesema Hamduni.

Hamduni amesema pia walibaini malipo kufanyika pasipo baadhi ya kazi kufanyika, malighafi za ujenzi kutopimwa ubora wake kinyume cha mkataba, ujenzi kufanyika bila matakwa ya mkataba, kutozingatiwa Sheria ya Manunuzi ya Umma na kuwepo kwa nyongeza ya kazi (variation) pasipo kufuata utaratibu.

Amesema Takukuru ilichukua hatua mbalimbali, ikiwamo kuhakikisha marekebisho katika miradi husika inafanyika na walilenga zaidi kuhakikisha Serikali haipati hasara, kutoa elimu kwa wasimamizi wa miradi na kuzishauri mamlaka zilizohusika namna bora ya kuziba mianya ya rushwa.

“Jumla ya miradi 171 yenye thamani ya Sh143.3 bilioni ilibainika kuwa na utekelezaji hafifu. Tulianzisha uchunguzi wa miradi hiyo iliyokuwa katika sekta ya ujenzi, fedha, maji, kilimo na majengo,” amesema.

Amesema mapendekezo 3,608 yalitolewa ili kurekebisha kasoro zilizobainika katika ufuatiliaji huo.

Hamduni amesema katika kuhakikisha marekebisho ya miradi husika yanafanyika ama kwa gharama za mkandarasi au fedha zilizofujwa zinarudishwa serikalini, mapendekezo 2,740 sawa na asilimia 89.4 yalitekelezwa.