Takukuru yakagua miradi 17, yabaini mapungufu

Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja akitoa taarifa kwa waandishi wa habari. Picha  na Suzy Butondo

Muktasari:

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Shinyanga imefuatilia miradi 17 ya maendeleo yenye thamani ya Sh5.6 bilioni inayotekelezwa na Serikali ikibaini baadhi kujengwa chini ya kiwango na mingine kutokamilishwa kwa wakati.

Shinyanga.Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Shinyanga imefuatilia miradi 17 ya maendeleo yenye thamani ya Sh5.6 bilioni inayotekelezwa na Serikali ikibaini baadhi kujengwa chini ya kiwango na mingine kutokamilishwa kwa wakati.

Akitoa taarifa ya robo ya nne ya mwaka huu leo Agosti 24, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja amesema walifanya ufuatiliaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa matengenezo ya barabara zilizopo Manispaa ya Shinyanga chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ili kuona iwapo inatekelezwa kwa wakati.

Amesema kati ya miradi hiyo, miwili imeonekana kuwa na dosari ukiwemo mradi wa barabara inayochongwa na kuwekwa vifusi na Tarura katika kata ya Chamaguha, Ngokolo, Ndembezi, Kambarage na Mwasele wenye thamani ya zaidi ya Sh236 milioni uliotakiwa kukamilika Aprili 27, 2023 lakini haukukamilika kwa wakati.

“Mradi huo ulitakiwa kukamilika Aprili 27, 2023 lakini haukukamilika kwa wakati mbali ya mkandarasi kuongezewa muda wa ziada wa siku 75 kuanzia Aprili 28 hadi Julai 12, 2023 kukamilisha kazi…kwa sasa mkandarasi yupo kwenye kipindi cha makato ya fedha ikiwa ni adhabu ya kuchelewesha kwa mjibu wa mkataba,”amesema Masanja

Amesema mbali na ucheleweshaji huo, mkandarasi Brampem Global Investment Co.L.T.D wa Shinyanga anayetekeleza mradi huo amedaiwa kutekeleza kazi za mradi chini ya kiwango kinyume na mkataba wa kazi husika.

“Baadhi ya mapungufu katika matengenezo ya barabara hizo ni kutokuchonga barabara kwa usahihi, kina cha tabaka la kifusi kinachowekwa kutofikia kiwango kinachotakiwa, kutoshindiliwa ipasavyo na uchongaji wa mitaro ya pembezoni mwa barabara isiyoridhisha.Takukuru ilimshauri msimamizi wa mradi Tarura imtake mkandarasi arudie kazi zote alizotekeleza chini ya kiwango

“Ushauri ulifanyiwa kazi na mpaka sasa marekebisho yenye thamani ya zaidi ya  Sh76 milioni yameshafanyika hata hivyo tunaendelea kushirikiana na Tarura kumfuatilia kwa ukaribu mkandarasi ili amalize kazi zilizobaki kwa mujibu wa mkataba,”amesema Masanja

Amesema kupitia Proramu ya Takukuru Rafiki walipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Kata ya Kisuke Halmashauri ya Ushetu juu ya ukosefu wa vifaa tiba na madawa katika zahanati ya Kisuke na ukosefu wa maji kwenye vijiji vya Ididi na Mutongi akidai kero hizo zilifanyiwa kazi na wananchi kupata huduma.

Kwa upande wa dawati la uchunguzi kwa kipindi hicho, amesema walipokea taarifa 35 za malalamiko;  zilizohusu rushwa ni 26 ambapo katika Sekta ya Elimu taarifa zilikuwa saba, Serikali za Mitaa sita, Ardhi tano, Polisi mbili, Afya mbili, Maji moja na GPSA moja akidai uchunguzi wa taarifa hizo unaendelea.

Ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendela kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vya rushwa au ubadhirifu wa fedha kwenye miradi ya maendeleo ili hatua zichukuliwe.