Takukuru yabaini viashiria vya rushwa miradi 12

Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Geita, Leonidas Felix akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Muktasari:

Miradi hiyo ni miongoni mwa miradi 33 yenye thamani ya Sh16.8 bilioni iliyofuatiliwa na kukaguliwa kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Geita. Miradi 12 ya maendeleo yenye thamani ya Sh5.6 bilioni iliyokaguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani hapa, imebainika kuwa na upungufu ikiwemo viashiria vya rushwa.

Miradi hiyo ni miongoni mwa miradi 33 yenye thamani ya Sh16.8 bilioni iliyofuatiliwa na kukaguliwa kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Miradi hiyo ni sekta ya maji, elimu, afya na miundombinu ya barabara.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake  Agosti 10, 2023 Kamanda wa Takukuru wa mkoa huo, Leonidas Felix amesema taasisi hiyo imebaini baadhi ya miradi ya elimu inayotekelezwa kwa fedha za Boost mafundi wenye mikataba ya kazi walikuwa hawakai eneo la kazi badala yake wanawaachia vibarua.

“Upungufu mwingine ni kutoshindanisha zabuni, ukiukwaji wa taratibu za manunuzi katika kutangaza zabuni pamoja na udanganyifu katika nyaraka za kupokelea vifaa vya ujenzi,” amesema Felix

Amesema katika kipindi hicho taasisi hiyo imefanya uchambuzi wa mifumo ili kudhibiti mianya ya rushwa na kubaini kazi 13 zilizokuwa na viashiria vya rushwa ikiwemo watendaji wa Serikali kutozingatia sheria na kanuni za manunuzi ya umma wakati wa kununua, kupokea na kutunza vifaa vya shule.

Felix amesema kwa kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu taasisi hiyo imepokea malalamiko 51 na tayari 41 uchunguzi umeanza na sita kati ya hayo uchunguzi umekamilika na tayari matano yameombewa vibali vya mashtaka katika ofisi ya taifa ya mashtaka.

Pia, katika kipindi hicho kesi mpya sita zimefunguliwa  huku kesi 10 zikiendelea mahakamani ambapo katika kipindi hicho Takukuru walizifikia kata 15 ambapo kero 154 ziliibuliwa.

Akizungumzia malalamiko ya wananchi kusuasua kwa utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa Jamii (CSR), Felix amesema kupatikana kwa kanuni za utekelezaji mpango wa CSR uliotolewa na Wizara ya Madini hivi karibuni utakuwa mwarobaini wa changamoto zilizokuwa zinakwamisha miradi kukamilika.