Mitambo ya kisasa kupima ujazo wa mafuta yasimikwa bandarini

Muktasari:

  • Mitambo ya kisasa ya kupima ujazo wa mafuta yakiwemo ya kula, ya taa, ndege, petroli, dizeli, ya vilainishi na mafuta mazito yanayoingia nchini (Flow Meters) ambayo imesimikwa katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara inatajwa kuinufaisha Serikali pamoja na wadau wa sekta ya mafuta.

Dar es Salaam. Mitambo ya kisasa ya kupima ujazo wa mafuta ya aina zote yanayoingia nchini Tanzania (Flow Meters) ambayo imesimikwa katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara inatajwa kuinufaisha Serikali pamoja na wadau wa sekta ya mafuta.

 Mitambo hiyo iliyosimikwa kwa awamu tatu na Serikali chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ina lengo la kupata takwimu sahihi za mafuta yakiwemo ya kula, taa, ndege, petroli, dizeli, ya vilainishi na mafuta mazito yanayoingia mara tu yanaposhushwa kutoka kwenye meli.

Mbali na hilo, dhumuni la mitambo ni kuifanya teknolojia kuwa sehemu muhimu ya upimaji wa ujazo wa mafuta badala ya utashi hivyo kupunguza makosa ya kibinadamu kama anavyobainisha Mhandisi wa Idara ya Mafuta wa TPA, Yona Malago.

Mhandisi wa Idara ya Mafuta TPA, Yona Malago akizungumza na waandishi wa habari juu ya uhakiki wa mitambo ya kupima ujazo wa mafuta leo Aprili 16, 2024.

Mhandisi Malago amesema hayo leo Jumanne, Aprili 16, 2024 wakati wa ushiriki wa kuhakiki wa mitambo hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam. Amesema hapo awali vilikuwa vinatumika vipimo visivyostahiki vya Dip Sticking na UTI.

“Vipimo hivyo si tu kwamba inahusisha matumizi makubwa ya binadamu katika upimaji na ukokotoaji wa kiasi cha mafuta, lakini pia ina viwango hafifu vya usahihi.

“Sasa hii mitambo mipya inafaida kwanza Serikali inapata kodi na tozo stahiki zinazotokana na uingizaji wa mafuta nchini, kutokana na utambuzi sahihi wa kiwango cha mafuta,” amebainisha Malago ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa.

Ametaja faida nyingine kuwa ni kuongezeka kwa shehena ya mafuta yanayoagizwa na nchi za jirani kupitia Bandari ya Dar es Salaam ambapo zitalipwa kodi stahiki.

Ameongeza mitambo hiyo ni shirikishi, kwani inahusisha taasisi za Serikali za wadau wa mafuta kama vile Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Wakala wa Vipimo (WMA), Mamlaka ya Maapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Aidha, meneja wa wakala wa vipimo vya mafuta yanayoingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam, Alfred Shungu amesema usimikwaji huo ni muhimu kwa kupata vipimo sahihi kwa kuwa vipimo hivyo havihitaji kuingiliana na binadamu.

Kwa upande wa waagizaji mafuta, Mkurugenzi Mtendaji katika kampuni ya AUGOSTA energy, Orlando D’Costa amesema kilichopo ni mitambo kuondoa upunjwaji wa mafuta wanayoagiza kutoka nje, jambo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu.

“Zamani ilikuwa wakati mwingine unaweza ukapunjwa kwenye meli au kwenye matenki kutokana na aina ya vipimo, lakini hivi sasa mafuta yatakayoagizwa ndio hayo yaliyolipiwa,” amesema.

Akitaja changamoto amesema zamani kulikuwa na upimaji kwenye meli na kwenye matenki, jambo ambalo kulikuwa na upokeaji mafuta pungufu. D’ Costa amesema hata TRA walikuwa wanachukua kodi ambayo haiendani na kiwango cha mafuta wanayopokea. 

D’Costa ameongeza kutokana na mitambo hiyo, sasa anaamini hata bei ya mafuta inaweza ikashuka kutokana na kulipia kodi stahiki na mafuta yanayopokewa.