Mmoja afariki dunia, watatu wajeruhiwa wakiiwahi Simba Kwa Mkapa

Dar es Salaam. Shabiki mmoja wa timu ya Simba amefariki dunia na wengine watatu wamejeruhiwa (majina hayajapatikana), katika ajali iliyotokea leo Ijumaa Machi 29, 2024 alfajiri katika eneo la Vigwaza mkoani Pwani ikihusisha gari aina ya Toyota Coaster iliyowabeba mashabiki wa Tawi la Kiwila wa mkoani Mbeya.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo huku akieleza bado chanzo cha ajali hakijajulikana.

“Ni kweli imetokea hiyo ajali imesababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi watatu, taarifa nyingine tunaendelea kuzifuatilia na taarifa zaidi tutawapatia,”amesema Lutumo.

Shuhuda wa ajali hiyo ambaye pia ni shabiki wa Simba, Kassim Hassan kutoka Tawi la Wekundu wa Dodoma amesema wameshuhudia ajali hiyo wakiwa njiani kwenda Dar es Salaam kutazama mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu hiyo na Al Ahly.

Muda mchache baada ya ajali hiyo, Klabu ya Simba kupitia mitandao yake ya kijamii ilitoa taarifa kuhusu ajali hiyo ikiandika: “Ajali ya kwanza imehusisha mashabiki wa Tawi la Kiwila Rungwe ambapo imetokea katika eneo la Vigwaza Pwani, taarifa za awali kutoka jeshi la polisi zinaeleza mtu mmoja amepoteza maisha.

“Ajali ya pili, ya Tawi la Wekundu wa Boda kutoka Tuduma imetoka Doma Mkoani Morogoro, mtu mmoja ameumia hakuna madharani makubwa, tayari viongozi wanaelekea Vigwaza ili kutoa msaada kwa waadhirika. Uongozi wa Simba unatoa pole kwa wote walioadhirika na ajali hizo.”

Fuatilia taarifa zaidi katika mitandao yetu