Simba yaandaa mambo mawili kabla ya kuivaa Al Ahly

Muktasari:

  • Simba na Yanga zimefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali kwenye michuano hiyo mikubwa zaidi kwa upande wa klabu Afrika.

Dar es Salaam. Baada ya mapumziko ya siku mbili, Simba inarejea kambini leo Jumatatu lakini tayari imeanza kupiga hesabu mbili muhimu kabla ya kuikaribisha Al Ahly ya Misri kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, itakayopigwa Machi 29 mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuanzia saa 3:00 usiku.

Simba na Yanga zimefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali kwenye michuano hiyo mikubwa zaidi kwa upande wa klabu Afrika.

Hesabu ya kwanza kwa Simba ni kuweka kambi fupi Unguja, Zanzibar kabla ya kuwakabili Al Ahly. Hii imekuja baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha kuwaambia viongozi wa timu hiyo anataka kikosi chake kiwe pamoja na kukaa kwa utulivu zaidi.

Kocha huyo Mualgeria anaamini hilo litasaidia katika kujenga umoja wa timu na kupunguza makosa ambayo wachezaji hufanya pale wanapofanya mazoezi wakitokea majumbani kwao wakiwa Dar es Salaam kipindi hiki ambacho mastaa wengine wapo na timu za taifa.

Kiongozi mmoja wa Simba ameliambia Mwananchi, jambo hilo litafikiwa muafaka leo jioni baada ya kikao cha viongozi na benchi la ufundi.

Jambo la pili ambalo Simba inapigia hesabu ni namna ya kuwapata kwa wakati wachezaji wake walioitwa kwenye timu za taifa.

Mastaa Aishi Manula, Kibu Denis, Keneddy Juma na Mohamed Hussein 'Tshabalala' wameitwa Taifa Stars huku Mzambia Clatous Chama akiitwa Chipolopolo na Saidi Ntibanzokiza akiitwa kwenye kikosi cha Burundi.

Kutokana na ratiba za mechi za mataifa wanayochezea wachezaji hao zinaonesha kila taifa litakuwa uwanjani Machi 25, hivyo kurejea kikosini Simba itakuwa kuanzia Machi 27, ambapo zitakuwa zimebaki siku mbili tu kwa Simba kucheza na Al Ahly.

Simba inaangalia utaratibu wa kuyaomba mashirikisho ya soka wanapotoka wachezaji hao kuwaruhusu mastaa hao kusalia kikosini badala ya kujiunga na timu zao za taifa au waende wacheze mchezo mmoja na kurudi mapema.

Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally amesema kila jambo litafahamika leo Jumatatu baada ya viongozi benchi la ufundi na wachezaji kukutana.

"Baada ya mechi na Mashujaa (Ijumaa), timu ilikuwa mapumziko. Kesho (leo), ndio tunarejea kazini rasmi.

"Kila jambo litafahamika kesho wakati viongozi na benchi la ufundi watakapokutana ikiwemo kambi na hilo la wachezaji wetu walioitwa timu zao za taifa na tutatoa taarifa kamili kwa vyombo vya habari," alisema Ahmed.

Simba msimu huu imepania kuvuka hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukwama hapo mara nne katika misimu mitano iliyopita.