Mtaalamu aeleza sababu nyani kuvamia makazi ya watu Rombo, Moshi

Muktasari:

  • Hivi karibuni, wanaume wanaoishi pembezoni mwa Mto Mlembea, Wilaya ya Rombo walilalamika kwamba nyani wa kiume wamekuwa wakihatarisha usalama wa wake zao wanapoingia kwenye makazi yao.

Moshi. Wakati wilaya za Rombo na Moshi mkoani Kilimanjaro zikikabiliwa na wimbi la uvamizi wa nyani kwenye mashamba na makazi ya watu, wataalamu wa wanyamapori wamesema ongezeko hilo linatokana na sababu za kibinadamu.

Hivi karibuni, wanaume wanaoishi pembezoni mwa Mto Mlembea, wilaya ya Rombo, walilalamika kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Rombo (CCM), Profesa Adolf Mkenda kwamba nyani wa kiume wamekuwa wakihatarisha usalama wa wake zao.

Walisema wanapoingia kwenye makazi yao, wakifukuzwa hawaondoki na badala yake wanawakonyeza.

Nyani hao ambao hutembea kwa makundi, wamekuwa tishio kwa wakazi wa wilaya hizo kwa kuwa wamekuwa wakiingia kwenye makazi ya watu na kula vyakula vilivyopikwa, mahindi mabichi mashambani na kushambulia mifugo kama kuku, bata na mbuzi.

Akizungumza na katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri), Dk Victor Kakengi amesema tatizo la mwingiliano baina ya wanyama hao na binadamu limesababishwa na binadamu wenyewe kutokana na shughuli za kibinadamu kufanywa katika hifadhi za wanyama.

Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania(Tawiri), Dk Victor Kakengi

Kakengi ambaye ni mtaalamu wa wanyamapori, amesema uvamizi huo unatokana na mgogoro baina ya binadamu na nyani.

Amesema kila mnyama aliyepo duniani ana thamani yake katika mfumo wa ikolojia na kwamba endapo binadamu ataingilia katika himaya zao, ni lazima utatokea mgogoro baina yao.

“Chanzo cha mgogoro wa nyani na binadamu ni sisi binadamu. Sisi binadamu tuna majukwaa ya kutuongelea lakini hawa wanyama ni nani anawaongelea?” Ni lazima tuhakikishe tunawahifadhi.

“Mungu alimuumba binadamu akampa mamlaka ya kutawala wanyama na kuwahuisha, sasa unaposhindwa kumtawala mnyama, mnyama atakutawala wewe, na ndio hiki tunachokiona sasa, mgogoro baina ya nyani na binadamu kwenye wilaya zetu za Rombo na Moshi,” amesema Kakengi.

Kutokana na uhalisia huo, mtaalamu huyo amesema njia sahihi ya kufanya kuwa ni kulinda mifumo ya ikolojia na kuacha uharibifu kwenye maeneo ya wanyamapori.

“Binadamu tumeongezeka na tumekuwa wengi, miaka ya 1961 wakati tunapata uhuru, Tanzania tulikuwa na idadi ya watu milioni 8, sensa ya mwaka 2012 tukaongezeka na kufikia zaidi ya milioni 40, sensa ya juzi (mwaka 2022), tupo zaidi ya milioni 60,” amesema.

Mtaalamu huyo anaeleza kwamba ongezeko hilo linakwenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya mwanadamu na mahitaji ya mwanadamu ni kwamba anahitaji kula, kuishi, na mahitaji mengine mengi.

“Ili binadamu ale, anahitaji alime ili apate chakula, kama mwaka 1961 alilima ekari tatu zikatosha familia yake, ina maana leo hii ambapo tupo zaidi ya milioni 60 anahitaji kuwa na ekari nyingi zaidi ili kukidhi mahitaji ya chakula katika kaya yake,” amesema

Amefafanua kwamba kutokana na ongezeko hilo la watu, baadhi ya wananchi wamevamia makazi ya wanyamapori kwa ajili ya shughuli za kilimo hali ambayo huathiri mazingira yao, hivyo kusababisha wanyama hao kukosa chakula na kuingia katika makazi ya watu.

“Binadamu tumeshindwa kutunza mazingira ya hawa wanyama, tunakata miti ovyo kuhakikisha familia zetu zinakula, watu wameongezeka, kwa hiyo sisi binadamu tumeamua kujipendelea, na kuhatarisha mazingira ya hawa wanyama.

“Tunapolima baada ya kuona tumeharibu maeneo ambayo tulikuwa tunalima zamani na hata mbolea imeshuka chini, tunaanza sasa kufungua mashamba mapya kwa kuondoa misitu, tunalima karibu na kingo za mito.

“Hawa nyani kwao ni porini, msituni, chakula chao ni matunda pori, majani pori, sasa binadamu kwa ajili ya kujipenda mwenyewe, kwamba wewe ndio unastahili kuishi hapa duniani, unalima hadi kwenye kingo za mito, unategemea nini,” amesema.

Anasema wanyama wanapenda kukaa kwenye kingo za mito ambako kuna miti aina mbalimbali, hivyo ikitokea mazao yamelimwa kwenye eneo hilo wataona ni haki yao.


Nini kifanyike

Mtaalamu huyo ameeleza kwamba jambo la muhimu kufanya ni

“Msiporejea maisha kama ya zamani, hawa wanyama ni wanyamapori, watakuja kubeba na watoto, itafika mahali umeacha mtoto nje uko ndani unamenya ndizi, unakuta mtoto kabebwa na nyani.

“Turejee tulikotoka tusiharibu mazingira yao. Kwa mfano hapa Kilimanjaro wanachoma moto ili kufukuza panya na wanyama wadogo, tumelima hadi mtoni na sasa tunawafuata hadi makwao, matokeo yake tunakuja kulipa gharama kwa ajili ya kutowatawala wanyama na kuwahuisha kama tulivyoelekezwa na Mungu,” amesema.

Ili kufanikisha hilo, amezishauri taasisi za uhifadhi kama Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Wanyamapori (Tawa), Mamlaka ya Ngorongoro na wengine kuhakikisha wanahifadhi wanyamapori kwa kutumia matokeo ya tafiti zao, ili kupunguza mwingiliano wa wanyamapori na binadamu.

“Lakini tunashauri Serikali na watunga sera pale wanapotunga sera, sera hizo zitokane na matokeo ya tafiti zetu ili iwe rahisi kukabiliana na changamoto hii ambayo ipo kwenye maeneo ya jamii,” amesema.

Kuhusu kuwafunga nyani kengele hususani Rombo, Dk Kakengi amesema hilo lilifanyika Rombo lakini baadaye nyani walizoea kengele zile na kuona ni kitu cha kawaida, wakazoea na kuendelea kuingia kwenye makazi ya watu kama kawaida.

“Tawiri tulienda kufanya utafiti kule Rombo kuangalia kama tunaweza kuipatia utatuzi changamoto hii, tulifanya majaribio mbalimbali ya kufunga kengele nyani dume, kwa mfano ukimfunga kengele nyani mmoja dume akawa anakimbia na ile kengele nyani mwenzake anaweza kukimbia kwa sababu anahisi bado anafukuzwa na mwenye mali.

“Utafiti ule ulifanikiwa kwa muda mfupi lakini hawa wanyama wana akili, wakabaini kumbe ni mwenzetu kafungwa kengele, kwa hiyo wanafika mahali hawamwogopi aliyefungwa kengele, na wakaona ni sehemu ya maisha yao,” amesema.

 Ameshauri kwa Rombo na Moshi vijijini, serikali za mitaa zina wajibu wa kutumia matokeo ya utafiti wanaofanya, hiyo itapunguza kero lakini ile dhana ya kusema nyani wanasumbua, wauawe, wahamishwe, anahoji ni wangapi watauawa au kuhamishwa.

Kuhusu athari za mwingiliano na wanyama hao na binadamu, Dk Kakengi amesema asilimia 60 ya magonjwa yanayomwathiri binadamu yanatokana na wanyamapori, wakiwemo nyani ambao husababisha magonjwa ya mlipuko na afya ya binadamu.

“Kwa mfano Ebola, mafua, yanatokana na wanyamapori, unaweza kuugua ugonjwa ukaenda hospitali wakapima hawaoni chochote lakini wakakupa ‘antibiotic’ ambayo inaua vimelea vingi, kwa bahati nzuri mwili ukapambana ukupona, lakini ugonjwa unarudi,” amesema.


Wananchi waanza kula nyani

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa wilaya ya Rombo, wamesema kutokana na wingi wa wanayamapori waliopo katika maeneo hayo ikiwemo kima, tumbuli, ngedere nao wameanza kula nyani.

Mkazi wa Mtaa wa Rima wilayani humo, Adelaide John amesema baadhi ya watu wenye akili zao timamu wamekuwa wakiwakamata nyani na kisha kula nyama yao.

“Suala la kula nyani huko kwetu kuna watu wanaona ni jambo la kawaida, hata mimi nilishawahi kushuhudia watu wakila nyani. Mimi mwenyewe kuna siku nilienda mahali kula nyama, kumbe nilikula ya nyani bila kujua, lakini nashukuru Mungu haikuleta madhara,” amesimulia mama huyo.

Kwa upande wake, Jerome Tesha, mkazi wa Ushiri wilayani humo, amesema suala la watu kula nyama ya nyani kwao sio ngeni kwa kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakila nyama hiyo bila woga.

“Siku nyingi tu mbona watu wanakula nyama ya nyani, ni kitu cha kawaida huku kwetu wala sio kitu kipya,” amesema Tesha.