Ndege ya ATCL yasota kisiwa cha Malta tangu 2020

Dar es Salaam. Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), aina ya Bombardier Q300 DHC-8 Dash 8 inaelekea kutimiza miaka minne tangu ilipopelekwa katika kisiwa cha Malta Ulaya, kwa ajili ya kuifufua upya baada ya kupata hitilafu.

Ndege hiyo iliyosajiliwa kwa namba 5H-MWF, ilipelekwa nchini humo tangu Novemba 15, 2020 na bado haijajulikana matengenezo yake yatakamilika lini.

Taarifa ya ndege hiyo kuwa kwenye kisiwa hicho imeonekana katika akaunti ya Malta Aviation Outlook ya mtandao wa X.

Akiizungumzia ndege hiyo jana, Mkurugenzi mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema matengenezo hayo yatachukua muda mrefu kwa kuwa hiyo ni ndege ya zamani.

“Hiyo ni ndege ya zamani ndiyo maana imekaa muda mrefu, kwa sababu wanatakiwa watafute spare parts (vipuri), kwa hiyo itachukua muda mrefu.

“Hiyo ni Dash8- Q 300, imekuja miaka 2000 huko, kwa hiyo haihusiani na ndege hizi zilizonunuliwa hivi karibuni. Ni ya zamani sana,” alisema Matindi alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana.

Aliendelea kusisitiza kuwa matengenezo hayo ni makubwa kwa sababu kuna vitu ambavyo havipatikani kwa haraka.

“Hiyo ndege ilikuwa imeharibika wakati tunaanza, kwa hiyo ni ya kufufua, hatuingii gharama yoyote, tunafufua ndege iliyoharibika kwa miaka mingi.

“Yalikuwa mawili, ama tuiuze au tuifufue. Kwa hiyo tukaamua tuifufue, tunaweza kuitumia kwenye masoko ambayo hayana watu wengi, inachukua watu 50, kwa hiyo ukilinganisha na ndege tulizonazo ni kiwango cha chini.

“Inaweza kutumika kwenye viwanja ambavyo running way (njia ya kuruka na kupaa) zake ni ndogo,” alisema.

Akieleza jinsi ilivyopelekwa, Matindi alisema iliruka baada ya kukaguliwa na kupewa kibali na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).

“Ndege inapotakiwa ipelekwe kwenye matengenezo inakuwa inaweza kuruka, ndiyo maana unapewa masharti kwanza hairuhusiwi kubeba abiria.

“Kwa hiyo inapelekwa ikiwa kwenye hali ya uangalifu sana, mnawapa watu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), wanakuja wanaangalia wanakupa kibali cha kupeleka tu, inaitwa Ferry flight,” alisema.

Alisema kibali hicho ni cha kuruka mara moja tu, kwani ndege inayopelekwa kwenye matengenezo haionekani kuwa na usalama wa kutosha.

“Sharti la kwanza hairuhusiwi kubeba abiria, sharti la pili hao watu wa TCAA wajiridhishe kwamba inakwenda kwenye matengenezo,” alisema.

Kwa mujibu wa mtandao wa Aerospace Technology, ndege aina ya Bombardier Dash 8 Q300 ilibuniwa mwaka 1998 na Bombardier Aerospace De Havilland ya Downsville Ontario nchini Canada. Inatoka kwenye mfululizo wa Q familia ya Dash 8 zikiwemo Q100 (viti 37), Q200 (viti 39) na Q400 (viti 68 hadi 78).

Tangu imeanza kutengenezwa, kampuni hiyo ilipokea maombi 981 na imeuza ndege 868.

Ndege hiyo ina umbo kubwa na injini zenye nguvu kuliko Bombardier Q200.

Ndege hiyo ina uwezo wa kupaa hadi mwendokasi wa kilomita 528 kwa saa na inaruka kimo cha mita 7,620. Inaweza kuruka umbali wa kilomita 1,558. Ina uzito wa kilo 19,505.

Kwa mujibu wa mtandao wa BAE Systems, kuna aina nyingi za ukarabati wa ndege kulingana na muundo na madaraja yake, lakini umekusanywa katika makundi, yakiwamo ya muda mfupi (line maintainance) unaofanyika kila siku kama kuangalia vimiminika, marekebisho ya vioo.

Pili, kuna ukarabati mkubwa (heavy maintenance) ambao hufanyika mara chache, ikiwa pamoja na kubadilisha vipuri na sehemu za ndege.

Tatu ni ukarabati unaohusisha sehemu mahsusi za ndege (shop maintenance).