NHIF yarejesha dawa 178 kwenye kitita kilichoboreshwa

Muktasari:

  • Ni zile zilizoondolewa kwenye kitita cha 2023  kwa madai kuwa waliweka mbadala wa dawa zilizoondolewa kulingana na mwongozo.

Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umezirejesha dawa  178 kwenye kitita chake cha mafao cha mwaka 2023 jambo litakalopanua wigo wa wanachama kupata dawa.
Hatua hiyo ya NHIF ni baada ya kuingia kwenye mazungumzo na Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (Aphfta) na Chama Cha Madaktari (MAT) na kuridhia kurejesha dawa hizo ambazo iliziondoa katika orodha Machi mwaka huu, kwa madai kuwa hazipo kwenye Orodha ya Dawa Muhimu za Taifa (NEMLIT).

Taarifa iliyotolewa na NHIF na kusababisha mvutano baina yake na wadau hao wa afya na hatimaye kuingia kwenye majadiliano Machi mwaka huu ilieleza:“Kati ya dawa 176 zinazodaiwa kuondolewa kwenye kitita cha NHIF, jumla ya dawa 138 hazipo kwenye NEMLIT, dawa aina 29 muundo wake haujajumuishwa katika NEMLIT.”

“Dawa nane muundo wake haujajumuishwa kwenye NEMLIT na dawa aina tatu zipo katika kitita kilichoboreshwa cha 2023 kinachotumika sasa,” Ilisema taarifa ya NHIF ikitaja sababu ya dawa hizo kuondolewa.

NHIF ilieleza kwenye kitita cha 2023 waliweka mbadala wa dawa zilizoondolewa kulingana na mwongozo.
Jana Jumatano, Mei 8, 2024, kupitia taarifa iliyotolewa na NHIF na kusainiwa na Kaimu Meneja Mawasiliano Grace Michael ilieleza kurejesha dawa hizo.

“Kufuatia mapitio ya orodha ya Taifa ya Dawa Muhimu iliyofanywa na  Wizara ya Afya Aprili mwaka huu  kwa kujumuisha muunganiko, muundo na nguvu kwa dawa 178 pamoja na kujumuisha dawa nne zilizokuwepo kwenye mwongozo wa Taifa wa matibabu lakini hazikuwemo kwenye NEMLIT na hatimaye kusaini nyongeza,  NHIF imejumuisha dawa hizo kwenye kitita,” alisema Grace

Kutokana na hayo, NHIF ilisema huduma za matibabu zitaendelea kupatikana katika vituo vyote vilivyosajiliwa nchi nzima na endapo kutakuwa na changamoto za utekelezaji watoa huduma wawasiliane na NHIF kuepusha usumbufu.

Kufuatia hatua hiyo ya NHIF, MAT na Aphfta walisema kilichofanywa na uongozi wa mfuko huo ni hatua ya kwanza ya utekelezaji wa makubaliano na sasa wanategemea bei ya dawa zitolewe.

Mmoja wa wajumbe wa Aphfta jina limehifadhiwa, ameiambia Mwananchi Digital kuwa dawa hizo ziliondolewa bila sababu na kurejeshwa kwake kutawaondolewa wananchi usumbufu wa kukosa dawa.

“Wananchi sasa hawatasumbuka kutafuta dawa, hii ni hatua ya kwanza yapo mambo mengi tuliyokubaliana ikiwemo gharama za kumuona daktari, bei ya dawa zote tunategemea nayo tupate majibu, suala la bei ya dawa ni muhimu wazingatie makubaliano yetu hatutakuwa tayari kukubali bei ambayo itatuondoa sokoni,”amesema mjumbe huyo.

Kwa upande wake, Rais wa MAT, Dk Deusdedit Ndilanha amesema kwenye majadiliano wadau waliona dawa hizo ni muhimu ndio maana walitafuta njia za kuzirejesha.

“Baada ya mazungumzo ilikubalika dawa zilioondolewa zirudi, hili ni eneo moja lakini lipo eneo la vipimo nalo tulikubaliana yafanyiwe kazi kwa hiyo suala la dawa kurejeshwa ni matunda ya mazungumzo tuliyoyafanya,” amesema.

Dk Ndilanha amesema mwongozo ambao NHIF walikuwa wanasimamia kuondoa dawa ulipitwa na wakati muongozo unaofanyiwa mapitio kila mwaka kuendana na wakati.
Ikumbukwe maboresho ya kitita kipya cha 2023 kilichotangazwa na NHIF ambacho kilipangwa utekelezaji wake kuanza Machi mosi mwaka huu, yalisitishwa  na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu baada ya kuibuka sintofahamu kwa watoa huduma wakiwamo MAT na Aphfta kugomea matumizi ya kitita hicho wakidai kinawakandamiza, wakishinikiza  kwa kusitisha huduma.

Mvutano huo ulimfanya Waziri wa Afya kuunda kamati huru iliyoratibu na kusimamia mazungumzo baina ya NHIF na wadau hao, huku huduma zikiendelea kutolewa.

Kilio cha wadau hao ni maeneo yaliyofanyiwa mapitio kwenye kitita hicho hasa ni ada ya usajili na kupata ushauri wa daktari, huduma za dawa, vipimo, upasuaji na gharama za kliniki za kawaida na kibingwa.