Rais Samia awatunuku nishani Kikwete, Magufuli

Muktasari:

  • Ni miongoni mwa viongozi na maofisa 17,850 waliotunukiwa nishani na Rais Samia katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Dar es Salaam. MaraisĀ  Jakaya Kikwete na hayati John Magufuli, wametunukiwa nishani ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Nishani hiyo hutunukiwa wakuu wa nchi wastaafu walio hai na marehemu walioingia madarakani kwa njia ya kikatiba na kuendelea kuonyesha maadili mema yenye nidhamu, heshima na mfano wa kuigwa.

Rais Samia Suluhu Hassan amewatunuku nishani hizo Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, ambazo zimekabidhiwa leo Aprili 24, 2024 kwa wake zao, Salma Kikwete na Janeth Magufuli.

Kwa niaba ya wengine, nishani 26 zimetolewa kwa viongozi wa juu katika makundi sita ambayo ni Nishani ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwenge wa Uhuru Daraja la Pili, Utumishi Uliotukuka, Utumishi Mrefu na Tabia Njema, Utumishi Mrefu, na Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Nne.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Huduma Ikulu, Charles Mwankupili, Rais ametunuku nishani kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya kifungu cha nne cha Sheria za Shughuli za Rais Sura ya Tisa pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2002, tamko lililotolewa katika Gazeti la Serikali namba 297 la Aprili 23, 2024.


Nishani ya Mwenge wa Uhuru Daraja la Pili wa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wakati wa hafla hiyo, hutunukiwa makamu wa Rais, wastaafu, mawaziri wakuu waliopo madarakani na waliostaafu, waliohai na waliofariki dunia ambao waliondoka katika madaraka bila kashfa na hata baada ya kuondoka katika madaraka, wameendelea kuwa na maadili mema na kuishi kwa heshima ya ofisi.

Nishani hii wametunukiwa Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Awamu ya pili, John Malecela; Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohamed Gharib Bilal; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.


Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano

Hii hutunukiwa maofisa na askari wa vyombo vya usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waliotunukiwa ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda, Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali Camillius Wambura, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) Balozi Ally Idd Siwa, Mkuu wa Jeshi la Magereza Kamishna Jenerali Ramadhani Nyamka, Mkuu wa Jeshi la Uhamiaji Kamishna Jenerali Anna Makakala, na Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Kamishna Jenerali John Masunga.


Nishani ya Utumishi Uliotukuka

Kwa mujibu wa maelezo, hutunukiwa maofisa walio kwenye utumishi hai wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wa cheo cha Meja kwenda juu, na wale wa majeshi ya Polisi, Magereza, Uhamiaji, na Zimamoto na Ukoaji kwa cheo cha Mrakibu au wa juu wa cheo hicho, na maofisa waandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa ambao wametumikia miaka 20 mfululizo ya kuwa ofisa.

Waliotunukiwa nishani hiyo ni Luteni Jenerali wa JWTZ Salumu Haji Othman, Kamishna wa Jeshi la Polisi Suzan Kaganda, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Chacha Jackson, Kamishna Uhamiaji, Hassan Ally Hassan, na Kamishna wa Zimamoto na Uokoaji Mbaraka Semwanza.


Nishani ya Utumishi Mrefu

Nishani ya Utumishi Mrefu hutunukiwa maofisa walio hai wenye nyota wa JWTZ, maofisa walio hai waliotangazwa wa majeshi ya Polisi, Magereza, Uhamiaji na Zimamoto na Uokoaji, na Idara ya Usalama wa Taifa ambao wametimiza utumishi miaka 15 mfululizo wenye tabia njema yenye kusifika.

Waliotunukiwa ni Luteni Kanali Gaudencia Mapunda wa JWTZ, Kamishna wa Jeshi la Polisi Hamad Hamis Hamad, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Magreth Nyoka, Mrakibu Msaidizi Uhamiaji, Zawadi Luka na Mkaguzi wa Zimamoto na Uokoaji Omary Memba.


Nishani ya Utumishi Mrefu na Tabia Njema

Nishani hii hutunukiwa maofisa wasiokuwa na nyota walio katika utumishi ulio hai katika JWTZ, Wakaguzi Wasaidizi, Stesheni Sajini, Sajini na Koplo wa majeshi ya Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Uokoaji waliotumikia kwa muda usiopungua miaka 15 katika vyeo hivyo na watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa ambao wametumikia idara hiyo kwa miaka hiyo wakiwa na tabia njema ya kusifika.

Waliotunukiwa ni Sajini Neema Mahiga wa JWTZ, Stesheni Sajini Rehema Mbeye kutoka Jeshi la Polisi,

Mkaguzi Msaidizi Martin Nyakyoma wa Magereza, Mkaguzi wa Uhamiaji, Fatma Kunema na Sajini Jackline Munisi wa Zimamoto.