Serikali yataifisha ng'ombe 114

Muktasari:

Kwa mujibu wa sheria za uhifadhi wa mazingira, mifugo haitakiwi kuingizwa katika maeneo ya hifadhi na inapojitokeza na kukamatwa hatua huchukuliwa kwa wahusika

Tabora. Serikali imetaifisha ng’ombe 114 kati ya 320 kwa idhini ya Mahakama  waliokamatwa ndani ya pori la akiba la Kigosi Muyowosi na wamiliki wake watano wamehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja ama kulipa faini ya Sh400,000 kila mmoja.

Uamuzi huo umetolewa leo Septemba 18,2018 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Chiganga  Mashauri, baada ya kuwatia hatiani  washitakiwa hao waliokuwa wanakabiliwa na kesi mbili tofauti zenye makosa yanayofana.

Watuhumiwa waliotiwa hatiani na mifugo yao kutaifishwa na Serikali ni Bahati Joseph Yusuph, Robert Dotto Kitapondya na Amos Masha waliokutwa na ng’ombe 100 ndani ya pori la akiba la Kigosi Muyowosi na wengine ni Mashine Mwandu na Issack Mashine waliokuwa na ng’ombe 14.

Watuhumiwa wote watano wamelipa faini ya Sh400,000 kila mmoja na kukwepa kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya kuingia na kuchungia mifugo ndani ya hifadhi ya Taifa.

Awali,  upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili Mwandamizi wa Serikali Idd Mgeni, umedai  mahakamani hapo washitakiwa walitenda makosa hayo Septemba 6,2018 ambapo waliingia ndani ya pori hilo la akiba bila kibali.

Wakili  Mgeni amedai katika shitaka la pili washtakiwa watatu walikutwa wakichunga ng’ombe  100  na wenzao wawili pia walichungia  ng’ombe 14 ndani ya pori hilo la akiba bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori nchini.

Mahakama iliwahukumu kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh100,000 kwa kosa la kwanza na kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh300,000 kwa kosa la pili kila mmoja.

Ngombe wengine 206 waliokutwa ndani ya hifadhi hiyo ambao wenyewe haijulikani walipo bado wanashikiliwa hadi hapo kibali kitakapo tolewa na mahakama ili wapigwe mnada kufidia uharibifu waliofanya katika pori hilo la akiba.