Sh1 bilioni zatengwa kukabiliana na athari za mafuriko Dar, Zanzibar

Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo akizungumza  leo bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 leo. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Mradi wa kuhimili athari za mafuriko na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko nchini waja.

Dodoma. Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imetenga Sh1.0 bilioni katika mwaka 2024/25 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam na Zanzibar.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 23, 2024 na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,  Dk Selemani Jafo wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake kwa mwaka 2024/25.

Katika makadirio hayo, Dk Jafo ameomba Bunge kuidhinishiwa Sh 62.67 bilioni katika mwaka 2024/25.

Dk Jafo amesema katika mwaka 2024/25, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya mradi wa kuhimili athari za mafuriko na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko nchini.

Amesema lengo la mradi huo ni kuijengea jamii uwezo wa  kuhimili athari za mafuriko,  kwa kuwa na shughuli endelevu za kujipatia kipato na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo yaliyoathiriwa na hali hiyo.

“Katika mwaka 2024/25 kiasi cha Sh1.0 bilioni kimetengwa kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam na Zanzibar,”amesema.

Aidha, Dk Jafo amesema katika mwaka huo watatekeleza mradi wa kurejesha ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame ya Tanzania.

Amesema kwa mwaka 2024/25, Sh405.7 milioni zimetengwa kwa ajili kukamilisha ujenzi wa malambo mawili na ukarabati wa lambo moja, mabirika matatu ya kunyweshea mifugo na majosho mawili katika Halmashauri ya Magu.

Pia kukarabati wa malambo (3), bwawa moja, mabirika (4) ya kunyweshea mifugo na majosho mawili katika Halmashauri ya Nzega na kukamilisha ujenzi wa mabwawa (3) na lambo (1), mabirika (4) ya kunyweshea mifugo na majosho (4) katika Halmashauri ya Mkalama.

Miundombinu ya kupumzikia Dodoma

Amesema kwa mwaka 2024/25, Sh456 milioni  zimetengwa kwa ajili ya usanifu na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mapumziko.

Ofisi ya Makamu kukarabatiwa

Dk Jafo amesema watatekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati wa Ofisi na makazi ya Makamu wa Rais.

Amesema kwa mwaka 2024/25, Sh700.00 milioni kimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.