Shisha yatajwa kuchochea matumizi ya dawa za kulevya nchini

Arusha.Ongezeko la matumizi ya kilevi cha shisha nchini limetajwa kuchochea matumizi ya dawa za kulevya huku tatizo hilo likiwaathiri zaidi vijana.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Juni 25, 2023 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo katika maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani yanayofanyika jijini Arusha.

Lyimo amesema wamebaini baadhi ya wauzaji wa shisha kuchanganya dawa za kulevya jambo ambalo limeongeza matumizi ya dawa za kulevya nchini.

"Matumizi ya shisha yameongeza matumizi ya dawa za kulevya na kuchochea matumizi ya dawa hizo,"amesema

Lyimo amesema Mamlaka hiyo imejipanga Kupambana na dawa za kulevya nchini hatua ambayo imefanya Tanzania Kuwa mfano katika Kudhibiti dawa hizo .

Pia amesema umefika wakati elimu ya athari za dawa za kulevya kutolewa  mashuleni ili Kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya na biashara hiyo.