Tamko la Serikali mbwa kutumika kukagua abiria

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile

Muktasari:

  • Mbunge wa Konde, Mohamed Said Issa amelalamikia matumizi ya mbwa kukagua abiria katika Bandari ya Dar es Salaam.

Dodoma. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuwachukulia hatua watumishi watakaokiuka utaratibu kwa kutumia mbwa wanapowakagua abiria, mizigo na vifurushi vyenye vyakula.

 Kihenzile amesema hayo leo Jumanne Aprili 16, 2024 akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde, Mohamed Said Issa.

Issa katika swali la nyongeza amehoji iwapo Serikali iko tayari kuwachukulia hatua watendaji wanaofanya ukaguzi kwa kutumia mbwa kwa mizigo ya abiria wanaokwenda Zanzibar kuwa ni suala la kila siku.

Amehoji Serikali inatoa kauli gani, ili jambo hilo lisijirudie.

Kihenzile amemwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TPA kuwa wanapofanya ukaguzi wazingatie utaratibu wa kutokagua abiria wala vyakula kwa kutumia mbwa.

“Ikibainika yuko mtendaji anafanya kinyume cha ilivyotarajiwa katika tamaduni zetu, utu wetu na kadhalika basi achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema Kihenzile.

Katika swali la msingi, Issa amehoji ni lini Serikali itaondoa mbwa wanaokagua mizigo katika meli za abiria kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa kuwa si rafiki kwa abiria.

Akijibu swali hilo, Kihenzile amesema Serikali kupitia TPA ina jukumu la msingi la kufanya ukaguzi wa kina wa abiria, mizigo na vifurushi.

Amesema jukumu hilo ni kwa abiria, mizigo na vifurushi  vinavyopita katika maeneo ya gati za abiria ikiwemo gati zinazohudumia Azam Sea Link na majahazi kwa ajili ya kudhibiti usalama wa abiria na usafirishaji wa bidhaa haramu kupitia maeneo hayo.

Amesema ukaguzi unaofanywa ni wa kawaida kwa kutumia midaki na pale kunapojitokeza mizigo au vifurushi vinavyotiliwa shaka, ndipo mbwa maalumu wa ukaguzi hutumika.

Naibu waziri amesema ukaguzi unaofanywa kwa kutumia mbwa hauhusishi abiria, mizigo na vifurushi vyenye vyakula.