Utafiti changamoto nguvu za kiume waja

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu  akizungumza wakati akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 ya Sh1.31 trilioni. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Katika mwaka 2024/25, Wizara ya Afya itafanya tafiti za nguvu za kiume na matumizi ya vinywaji vya kuongeza nguvu.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imetega Sh3.5 bilioni katika bajeti ya mwaka 2024/25 kwa ajili ya tafiti katika maeneo sita ikiwemo nguvu za kiume na matumizi ya vinywaji vya kuongeza nguvu.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu leo Mei 13, 2024 wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2024/25.

Ummy amesema katika kusimamia tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya Sh3.50 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza afua mbalimbali.

Amezitaja tafiti hizo ni magonjwa yasiyo yakuambukiza ikiwemo saratani, ufuatiliaji wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa na utafiti juu ya changamoto ya afya ya akili.

“Utafiti juu ya matumizi ya Energy Drink, utafiti kuhusu nguvu za kiume na dawa za tiba asili,” amesema Ummy.

Aidha, amesema katika kuimarisha huduma za afya ya akili, huduma za utengamao na tiba shufaa hususani kwa watoto, wazee na wenye ulemavu wametenga Sh9.31 bilioni.

Amesema kiasi hicho cha fedha kitatumika kutoa elimu kwa umma kuhusu vihatarishi vya afya ya akili na namna ya kukabiliana navyo na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya ya akili, katika hospitali za rufaa za mikoa na za halmashauri.

“Kuimarisha upatikanaji wa wataalamu wa afya ya akili katika ngazi zote, kuimarisha upatikanaji wa dawa za afya ya akili na kuanzisha huduma za afya ya akili kwa njia ya mtandao,” amesema.

Amesema pia kiasi hicho cha fedha kitatumika katika kuimarisha uratibu wa huduma, tafiti na mafunzo kuhusu afya ya akili kwa kukamilisha uanzishwaji wa taasisi ya Taifa ya akili.

Mambo mengine yatakayogharamiwa kwa fedha hizo ni kuimarisha utambuzi wa mapema wa watoto wenye ulemavu na kuanzisha huduma tatu za utengamao (Fiziotherapia, Tiba Kazi (occupational therapy), Matamshi na Lugha (Speech and language therapy) katika hospitali za rufaa za mikoa 10.

Ummy ameyataja mambo mengine ni kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za utengamao katika hospitali za rufaa za mikoa na kuendeleza utoaji wa huduma za utengamao kuanzisha kituo cha umahiri cha huduma za utengamao.

Pia fedha hizo zitatumika katika ununuzi wa dawa, vifaa na vifaatiba vya kutolea huduma za utengamao pamoja na vifaa saidizi.

Aidha, Ummy amesema zitatumika katika kuimarisha upatikanaji wa wataalamu wa utengamao na tiba shufaa kwa kuwajengea uwezo watalaamu waliopo na kuibua wapya.

“Zitatumika kuimarisha huduma za utengamao kwenye ngazi ya msingi na kuratibu uanzishwaji wa klabu za afya za wazee katika ngazi ya halmashauri,” amesema.