Vigogo kununuliwa magari 102, mikopo ya asilimia 10 yarejea

Muktasari:

  • Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ya Sh10 trilioni.

Dar es Salaam. Waziri Ofisi ya Rais- Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amesema katika mwaka 2024/25, wamepanga kutumia Sh190.57 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa magari ya viongozi wa mikoa na wilaya, kuendelea na ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa miundombinu ya mikoa ikiwemo majengo ya utawala, ikulu ndogo, makazi ya viongozi na watumishi wa mikoa, wilaya na tarafa katika mikoa 26.

Amesema hayo leo Jumanne, Aprili 16, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25.

Amesema ununuzi wa magari tisa ya Wakuu wa Mikoa (RC) na Makatibu Tawala wa Mikoa (RAS) katika mikoa ya Katavi, Njombe, Iringa, Kigoma, Mwanza, Singida, Dar es Salaam na Manyara. Ununuzi wa magari 56 ya wakuu wa wilaya (DC) na 47 ya wakurugenzi wa halmashauri (DED).

Waziri Mchengerwa amesema kuendelea na ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa miundombinu ya mikoa ikiwemo; majengo ya utawala 49, ikulu ndogo 8, makazi ya viongozi 25 na makatibu tawala wa mikoa na wilaya 17, makatibu tawala wasaidizi wa mikoa 10 na tarafa 5.

Amesema kuendelea na ujenzi wa majengo ya utawala katika halmashauri 77 na ununuzi wa samani za majengo ya utawala katika halmashauri 21. Ukamilishaji wa nyumba 24 za wakurugenzi wa halmashauri na ujenzi wa nyumba 35 za wakuu wa idara.

Waziri huyo amesema kuanza utekelezaji wa miradi mitano ya kimkakati na kuendelea na ujenzi wa miradi 15 ya kimkakati katika halmashauri 20.

Kuhusu mikopo ya asilimia 10, Waziri Mchengerwa amesema Serikali imerejesha utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuanzia Julai, 2024 kwa utaratibu wa kutumia benki kwa halmashauri 10 za majaribio.

Amezitaka Halmashauri hizo ni Majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, Manispaa za Kigoma Ujiji na Songea, Miji ya Newala na Mbulu, Wilaya za Siha, Nkasi, Itilima na Bumbuli.

Amesema halmashauri 174 zilizobaki zitatumia utaratibu ulioboreshwa, ili kuondoa upungufu uliyosababisha changamoto za awali kwa kufanya mambo yafuatayo; uanzishwaji wa kitengo cha usimamizi wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Rais – Tamisemi na uanzishwaji wa kamati za usimamizi wa mikopo katika ngazi za ofisi za wakuu wa mikoa, halmashauri na kata.

Waziri Mchengerwa amesema majukumu ya kamati ngazi ya kata ni kutambua waombaji na kuthibitisha vikundi vya mikopo na kuvisajili kwenye mfumo kabla ya kuwasilisha kwenye kamati ya halmashauri.