Wabunge wataka ukaguzi wa magari kidijitali

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo akizungumza wakati akijibu maswali ya wabunge leo Jumanne, Aprili 16 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Kamera za barabarani kutumika kuhakikisha magari yanayosafirisha mizigo na abiria yanaenda salama.

Dodoma. Wabunge wameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani kuanzisha mfumo wa kidijitali (APP-Application) utakaosaidia ukaguzi wa magari ya mizigo na abiria, ili kuwa na uhakika wa ukaguzi, badala ya ilivyo sasa baadhi hugongeshewa mihuri bila kukaguliwa.

 Waliotaka kuanzishwa mfumo huo ni wabunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko na Asha Abdalah Juma maarufu kama Mshua.

Katika swali la nyongeza, Asha amehoji Serikali ina mpango gani wa kuandaa mfumo wa mtandao wa kidijitali utakaowezesha kuona iwapo ukaguzi umefanyika.

Amesema hilo linatokana na uwepo wa baadhi ya vituo ambavyo kondakta amekuwa akikimbia ndani ya kituo na kugongewa muhuri, kisha kurejea ndani ya basi bila kujali kama gari limekaguliwa, hivyo kuwa na uwezekano wa kusababisha madhara kwa abiria.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amesema wizara ipo katika kipindi cha maboresho kuhakikisha magari yote ya mizigo yanapimwa uzito.

Amesema pia wanaboresha kwa kuweka APP itakayowezesha kufuatilia magari yote, ili kuhakikisha hayaongezi mzigo lakini yanasafiri kule yanapotakiwa kufika.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Asha Abdalah Juma maarufu kama Mshua akizungumza wakati akiuliza swali bungeni leo Jumanne, Aprili 16 2024. Picha na Merciful Munuo

Katika swali la msingi, Asha amehoji Serikali inadhibiti vipi vyombo vya usafiri wa umbali mrefu kusimamishwa barabarani mara kwa mara.

Sillo amesema Serikali ilishaweka utaratibu kwa magari yote ya mizigo na abiria yanayokwenda umbali mrefu kufanyiwa ukaguzi na upekuzi kwenye maeneo ya mizani kwa mujibu wa kanuni ya udhibiti wa uzito wa mizigo barabarani ya mwaka 2017.

Pia hufanyiwa ukaguzi na upekuzi kwenye maeneo hayo kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya udhibiti wa uzito wa magari ya mizigo na abiria ya umbali mrefu namba 1 ya mwaka 2016.

“Lengo ni kurahisisha na kuwahisha safari za magari hayo. Vituo vilivyotengwa kwa ajili ya ukaguzi huo ni Vigwaza, Mikumi, Makambako, Mpemba, Kasumuru, Njiku, Nyakahula, Msata, Kimokouwa, Mkuranga na Mnazi Mmoja,” amesema.

Amesema mabasi ya abiria ya safari za ndani yatakaguliwa kwenye vituo vya mabasi na sehemu maalumu zilizotengwa.

Sillo amesema iwapo vyombo hivyo vya moto vitakuwa vimefanya makosa kwa kukiuka sheria ya usalama barabarani vitachukuliwa hatua za kisheria, sehemu makosa hayo yalikotendeka.

Akiuliza swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko amesema kumekuwa na utaratibu wa trafiki kusimamisha magari kwa ghafla tena katika barabara kuu, jambo linaloweza kusababisha ajali.

“Sasa ninataka kujua ni lini Serikali itaanza kutumia mfumo wa kieletroniki ambao utakuwa unarekodi kama kuna makosa yoyote yametokea kuliko ilivyo hivi sasa, ili kupunguza ajali barabarani?” amehoji.

Sillo akijibu swali hilo, amesema wizara iko katika maboresho kuhakikisha wanaweka kamera za barabarani kuhakikisha magari yanayosafirisha mizigo na abiria yanakwenda salama, hivyo kutokuwa na ukaguzi wa ghafla.