Wananchi wanavyotoa kero kupitia Takukuru

Muktasari:

 Programu ya Takukuru Rafiki imewezesha kuibua kero katika sekta ya maji, afya, elimu, nishati, umeme, barabara na ardhi

Dodoma. Programu ya Takukuru Rafiki iliyoelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwamba ni ubunifu utakaosaidia kupunguza kero za wananchi na kufanya Serikali kuwajibika ipasavyo, pia imesaidia kuwa daraja kwa idara zingine za Serikali kupokea kero za wananchi.

Jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni amewasilisha kwa Rais Samia taarifa ya taasisi yake kwa mwaka 2022/23, kuhusiana na utendaji kazi ikiwamo kupokea kero 6,306 za wananchi ambazo zisipofanyiwa kazi zinaweza kusababisha vitendo vya rushwa ama manung’uniko.

Takukuru Rafiki  ni programu inayotekelezwa kupitia Mpango Mkakati wa Takukuru kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2025/26 na inalenga kupanua wigo wa kushirikisha wananchi na wadau katika kutambua na kutatua kero katika utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Utekelezaji wa programu hiyo unafanyika kupitia mikutano ya hadhara kwenye ngazi ya kata, kutambua kero zinazowakabili wananchi kwenye utoaji na upokeaji wa huduma za afya, elimu na utekelezaji wa miradi ya maendeleo wa miundombinu ya kutolea huduma.

Kero zinazohusu rushwa hushughulikiwa na Takukuru na zisizohusu rushwa hupelekwa kwenye idara husika.

Mkazi wa Chang’ombe mkoani Dodoma, Nzengo Kasubi amesema Takukuru Rafiki iliwahi kufika kwenye mtaa wao na miongoni mwa kero zilizotolewa na wananchi ni ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa maji na kero ya waendesha bodaboda.

Hata hivyo, Kasubi amesema kuna kero wanaona kama zimeshughulikiwa lakini zingine bado, hasa tatizo la maji na kero ya waendesha bodaboda.

Mjumbe wa nyumba kumi Mtaa wa Chang’ombe, George Simba amesema Takukuru Rafiki kwenye eneo lao iliwezesha wananchi kupata jukwaa la kupaza sauti kwa kutoa kero zinazohusu idara zote za Serikali. “Wananchi walikuwa huru kutoa kero yoyote, inayohusu idara yoyote ya Serikali,” amesema.

Rehema Dete mkazi wa Kijiji cha Sukamahela, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida amesema Takukuru Rafiki imewasaidia kupata sehemu ya kutolea kero zao na kuharakakisha utekelezaji.

“Programu ya Takukuru Rafiki hufanyika wazi katika mikutano ya kata jambo linalowajengea uwezo wananchi kuibua kero ambazo endapo zikiachwa ziendelee zinaweza kusababisha vitendo vya kushamiri zaidi rushwa nchini," amesema Dete.

Akizungumza wakati wa kukabidhi taarifa kwa Rais Samia, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni amesema katika kutekeleza maagizo ya Rais yanayohusu kuzuia rushwa, walibuni na kutekeleza programu ya Takukuru Rafiki.

Utaratibu wa upokeaji wa kero za wananchi na kuzifikisha katika sekta zinazotakiwa umekuwa ukifanywa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda katika mikutano yake ya hadhara anayoifanya nchini.

Hamduni amesema utekelezaji wa programu hiyo unahusisha mikutano ya wanufaika katika ngazi ya kata ambao wanatambua kero katika utoaji huduma au katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema kama hatua hazitachukuliwa kuhusu kero hizo, zinaweza kusababisha vitendo vya rushwa ama manung’uniko ya wananchi katika maeneo hayo.

Hamduni amesema kero zinazotambuliwa huwasilishwa kwa watoa huduma ili waweze kutatuliwa ama kuzipatia ufumbuzi.

Amesema katika kutekelea mradi huo, kero 6,306 ziliibuliwa na wananchi pamoja na wanufaika wa huduma na kero 3,513 zimetatuliwa.

Hamduni amesema kero zilizoibuliwa katika sekta ya maji, afya, elimu, nishati, umeme, barabara na ardhi na kuwa wanaedelea kushirikiana na sekta husika ili kutatua kero za wananchi katika ngazi ya chini.