Zabuni ya ujenzi yalifikisha Jiji la Arusha mikononi mwa Takukuru

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Jengo hilo la utawala linalomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha, ujenzi wake unaelezwa kuwa utagharimu Sh12 bilioni.

Arusha. Upungufu wa utangazaji wa zabuni ya ujenzi wa jengo la utawala umeliweka pabaya Jiji la Arusha kutokana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kubaini kulikuwa na mianya ya rushwa.

Jengo hilo la utawala linalomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha, linatarajia kujengwa kwa gharama ya Sh12 bilioni.

Hata hivyo, leo Jumatano Aprili 24, 2024, Takukuru imesema imebaini kukiukwa kwa taratibu za mchakato wa upatikanaji wa zabuni ya ujenzi wa jengo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema baada ya uchunguzi wao juu ya zabuni hiyo, wamebainika uwepo wa viashiria vya rushwa ulioanzia kwenye mchakato wa utangazaji wa zabuni hiyo.

 Zawadi amesema baada ya kubaini upungufu huo, walichukua hatua ya kusimamisha mchakato huo na kulitaka Jiji kutangaza upya kwa uwazi.

Amesema taasisi yake ilipata taarifa za tukio hilo mwishoni mwa mwaka jana na kuanza kulichunguza kwa karibu hadi pale walibaini ukweli na kuwataka viongozi kuitangaza upya.

 “Baada ya kupokea taarifa, tulifanya ufuatiliaji wa zabuni hiyo tukabaini uwepo wa mianya ya rushwa katika mchakato wa uteuzi wa njia ya manunuzi kama inavyoelekezwa na kanuni, na kwenye uundwaji na utekelezaji wa jukumu la uchambuzi yakinifu,” anesema Zawadi.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini amesema walikwisha pokea maelekezo ya upungufu huo na wamefanyia kazi ikiwamo kutangaza upya zabuni hiyo.

"Ni changamoto ndogo tu ilitokea na tumeshatangaza tenda ya wazi ya ujenzi wa mradi huo wenye namba 7003/2023/2024/W/26 tangu Januari, mwaka huu na utaratibu wa manunuzi unazingatia kanuni ya manunuzi ya umma ya mwaka 2013 (NeST),” amesema Hamsini.

Kwa upande mwingine,  Zawadi amesema katika ufuatiliaji wa fedha za umma zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu pia wamebaini upungufu katika miradi mingine minne.

Amesema walibaini upungufu kwenye mfumo wa maji katika vyoo vya Shule ya Sekondari Lake Eyasi  iliyoko Wilaya ya Karatu, unaojengwa kwa thamani ya Sh584.280 milioni na  katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Kamwaga ulioko Wilaya ya Longido wenye thamani ya Sh584.0 milioni.

"Katika miradi hii miwili, tuliagiza kamati ya ujenzi wa shule hizo zisimamie urekebishwaji wa miundombinu hiyo kwa kuzingatia kiwango cha ubora,” amesema Zawadi.

Ujenzi wa mtaro wa Barabara ya Mtaa wa Naurei iliyoko Kata ya Sekei Wilaya ya Arumeru wenye thamani ya Sh30 milioni, nao una upungufu sambamba na ujenzi wa nyumba za walimu 61 katika Shule ya Maweni iliyoko ndani ya Jiji la Arusha unaotekelezwa kwa Sh70 milioni.

“Kwenye ujenzi wa Mtaro wa Naurei, kwanza mradi umecheleweshwa na hakuna vibao vya tahadhari, lakini kwa ujenzi wa nyumba moja ya walimu sita kuna dosari katika malipo ya Sh2.4 milioni yaliyofanywa na mzabuni na vyote tumebaini na wahusika wamekubali na wanarekebisha,” amesema Zawadi.

Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za rushwa kwenye utekelezaji wa miradi ili kuendelea kulinda rasilimali fedha za umma zisitumike vibaya kwa masilahi ya wachache.