Kuna la kujifunza kauli ya Ndumbaro

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro amezua mjadala kufuatia kauli yake aliyoitoa hivi karibuni aliposema atasikitishwa endapo ataona Watanzania wamevaa jezi za Al Ahly katika mechi ya Simba au jezi ya Mamelodi Sundowns katika mchezo wa Yanga huku akisema watu hao hawatoruhusiwa kuingia uwanjani au wataingia kwa kuonyesha hati zao za kusafiria zinazoonesha sio Raia wa Tanzania.


 Alisisitiza kwamba kwa shabiki atakayeenda katika Uwanja wa Benjamin Mkapa akiwa amevaa jezi ya Mamelodi Sundowns lazima aoneshe hati ya kusafiria ya Afrika Kusini na akiwa na jezi ya Al Ahly aoneshe hati ya kusafiria ya Misri, nje na hapo akifanya fujo polisi watamchukua na kumpeleka katika kituo cha jirani.

Hapana shaka yoyote, lengo la Waziri Ndumbaro katika kutoa kauli hiyo lilikuwa ni kuhimiza uzalendo kwa mashabiki wa soka nchini ambao katika miaka ya hivi karibuni umekuwa hauonekani kwao pale timu au wanamichezo wetu wa Tanzania wanaposhiriki mashindano ya kimataifa.

Wapo ambao huenda mbali zaidi kwa kuamua kabisa kushangilia wageni na kuzomea cha nyumbani pindi kunapokuwa na mashindano fulani na hii imekuwa ikichangia kushusha morali na kuwafanya wanamichezo na timu zetu kufanya vibaya katika mashindano hayo ambayo wanashiriki.

Lakini hata hivyo, njia ambayo Waziri Ndumbaro ameitumia kufikisha ujumbe wake haikuwa sahihi na mwisho wa siku imesababisha ukosoaji wa wengi kwake na imeleta matokeo hasi.

Kwanza imetengeneza taswira kuwa hapa nchini serikali imekuwa ikiingilia masuala ya mchezo wa soka jambo ambalo limekuwa haliungwi mkono na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ambayo imekuwa ikisisitiza kwamba masuala ya soka yatolewe uamuzi na ufafanuzi wa viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza soka.

Hata hivyo, kiuhalisia hapa nchini serikali imekuwa ikijitahidi sana kutoa uhuru kwa viongozi wa soka kujiendeshea mambo yao.

Pili kauli ile imetafsiriwa na baadhi ya watu kama ya kibaguzi ambayo inaweza kusababisha vurugu na baina ya mashabiki wa timu moja na nyingine lakini pia ni kauli ambayo haiendani na kaulimbiu ya Fifa ambayo ni ‘Be Positive, Be Fair’.
Hii ni kauli mbiu ambayo inaweza kuonekana ni ya kawaida lakini ikawa na maana kubwa katika kuupa upekee mchezo wa soka.

Mamelodi Sundowns ama Al Ahly ni timu kubwa barani Afrika ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika mashindano mbalimbali hivyo sio ajabu kuwa na mashabiki katika nchi nyingine tofauti na huko zinakotoka na Tanzania siyo kisiwa kwamba yenyewe pekee haitokuwa na mashabiki wa timu hizo mbili, sio jambo la haki kuwanyima fursa hao kushabikia timu wanayoipenda.

Baada ya hili kutokea, pengine lipo la kujifunza kwamba kuna haja ya kutowahi kutoa matamko kwenye masuala yanayogusa hisia za wengine kwani yanaweza kuleta athari kwa mtu mmojammoja na kundi la wengi.

Kwa muda mrefu, Tanzania imekuwa ikisifiwa na kutajwa kama miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa ukarimu kwa wageni lakini pia watu wake wana kiwango cha juu cha kuvumiliana na kuishi bila migogoro hivyo hatupaswi kuiharibu sifa hii.

Ikumbukwe pia Tanzania kwa sasa tumeanza maandalizi ya kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 kwa kushirikiana na majirani zetu wa Kenya na Uganda.

Nyakati kama hizi zinaweza kutumika kupima ni kwa namna gani Tanzania tunaanza kuwa tayari kwa kuandaa mashindano hayo.

Tuyakwepe matamko kama haya kwa sababu yanaweza kutumika vibaya na kupelekea wale ambao wameiamini nchi yetu na kuipa ridhaa ya kuandaa Afcon waone kuwa walikosea na kujikuta wakifanya mabadiliko ya ghafla na kuwapa fursa hiyo muhimu watu wengine.

Kwa bahati nzuri, muda mfupi tu baada ya tamko lile kutolewa, makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji alituliza hali ya hewa baada ya kuwahakikishia Mamelodi Sundowns kupitia mtandao wa X kwa kuwaahidi watakuwa salama wao na mashabiki muda wote ambao watakuwa Tanzania.

Baadaye Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliandika barua kwenda kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) kulijulisha kuwa taratibu na kanuni zote zinazohusu mchezo wa soka zitafuatwa kwa mechi hizo za robo fainali.