Sheria zipitiwe kukomesha ukatili

Kwa takriban wiki nzima sasa imekuwepo mijadala inayoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, ambayo imegusa masuala mtambuka na hasa ukatili kwenye jamii, hususan kwa watoto.

Kwa kuzingatia ripoti mbalimbali, changamoto za kijamii zinazohusu ukatili wa kijinsia na matatizo ya familia nchini ni nyingi na kubwa, ambazo zinaweka haja ya kuchukua hatua za haraka na za makusudi, ili kukomesha matukio haya.

Ukatili huu, hasa dhidi ya watoto na wanawake, unahitaji majibu ya kisheria na kisera, ambayo yanazingatia mabadiliko ya kweli na endelevu.

Kwa hali iliyopo, ni muhimu kurekebisha sheria na sera za familia ili kuhakikisha kwamba wazazi wote wanawajibika kikamilifu kwa malezi na ulinzi wa watoto wao.

Hii inaweza kujumuisha kubainisha majukumu na haki za wazazi katika malezi, ikiwa ni pamoja na wajibu wa kifedha na kihisia kwa watoto wao, hata kama wazazi hao wameachana.

Pamoja na hilo, yapo pia mahitaji bayana ya sheria madhubuti zinazolenga kuzuia na kukomesha ukatili wa kijinsia na udhalilishaji katika familia. Hizi ni pamoja na adhabu kali kwa wanaokiuka sheria hizi, bila kusahau mifumo imara ya kutoa haki kwa waathirika wa ukatili huu.

Vilevile, elimu ya umma na mafunzo kwa maofisa wa sheria ni muhimu ili kuhakikisha utekelezaji sahihi wa sheria hizi na wanaohusika kuzisimamia waondokane na ile ya dhana ya “hayo ni mambo ya kifamilia” au kukumbatia rushwa ambayo hupofusha macho yasione sheria.

Licha ya sheria, vilevile sera za elimu na masuala ya jamii zinapaswa kuimarishwa ili kutoa msaada na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa malezi bora na familia imara.

Elimu hii inapaswa kuanza mapema shuleni na kuenea katika jamii nzima ili kujenga ufahamu na kubadilisha mitazamo kuhusu malezi na majukumu ya wazazi.

Mzigo mkubwa katika hayo unabebwa na Serikali, lakini hapana shaka kwamba yenyewe peke yake haiwezi kufanikisha kila kinachohitajika. Hivyo, inapaswa kushirikisha wadau wa kijamii, mashirika ya kiraia na viongozi wa kidini katika kubuni sera na kampeni za kuhamasisha mabadiliko haya.

Ushirikiano huu utahakikisha kwamba mikakati inayowekwa inalingana na mahitaji halisi ya jamii na inakubalika na watu wote wanaohusika.

Kama ambavyo imekuwa ikielezwa, athari za masuala haya zimekwishakuwa kubwa kwa jamii yetu, hivyo maboresho haya yanapaswa kufanywa kwa haraka na kwa kuzingatia mahitaji ya kibinadamu.

Hatuwezi kuanzia hewani, zipo sheria ambazo tayari zimetungwa, lakini hazikidhi mahitaji na nyingine zinajichanganya.

Tukae chini kama nchi na kuzipitia upya na hata zile zilizolalamikiwa mahakamani tusiwe na kigugumizi cha kuzifanyia marekebisho ili kupata mustakabali mwema wa nchi yetu.

Hapa tunazungumzia masuala kama ya umri wa mtoto kuolewa ambayo yamepita kwenye tanuri la sheria kwa ngazi zote za mahakama, lakini bado Serikali haina haraka ya kukamilisha mchakato wake.

Hili ni jambo linaloibua maswali mengi, na wadau wamekuwa wakijiuliza hivi Serikali inanufaikaje na kuolewa kwa watoto wadogo wa miaka 15, badala ya kuweka wazi kuwa mtu mzima pekee, kwa maana ya aliyetimiza miaka 18, ndiye awe na ruhusa ya kuolewa.

Tunaitaka Serikali ichukue hatua kama hizo ili kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu na kujenga jamii salama.