Dullah Mbabe afungiwa kuzichapa Uingereza

Muktasari:

  • Mbabe ni bondia wa pili kufungiwa kucheza nchini Uingereza kwa miaka ya  karibuni, mwingine ni bondia namba moja nchini kwenye uzani wa super welter, Hassan Mwakinyo aliyewahi kufungiwa mwaka 2022.

Dar es Salaam. Bodi ya kusimamia ngumi za kulipwa nchini Uingereza imemfungia bondia Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ kuzichapa kwa muda nchini humo.

Uamuzi wa bodi hiyo umekuja siku chache baada ya bondia huyo namba tatu nchini kwenye uzani wa super middle kupigwa kwa Knock Out (KO) ya raundi ya nne Machi 31, 2024.

Mbabe alichapwa na Callum Simpson bondia namba 36 dunia, kwenye uzani wa super middle na wanne nchini Uingereza mwenye nyota tatu.

Kwa mujibu wa mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec), bodi hiyo imemfungia mbabe kuzichapa Uingereza kwa muda.

Adhabu kama hiyo aliwahi kukutana nayo, Hassan Mwakinyo bondia namba moja nchini kwenye uzani wa super welter mara baada ya pambano lake la Septemba 3, 2022, alipochapwa kwa Technical Knock Out (TKO) ya raundi ya nne la Liam Smith nchini humo.

Hata hivyo, Rais wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC), Chaurembo Palasa amefafanua chanzo cha adhabu hizo kuwa zinatolewa ili kulinda afya ya bondia baada ya kipigo na ndicho kimetokea kwa Dullah Mbabe.

“Baada ya muda atafunguliwa, hiyo ni baada ya kuwa amepigwa KO kule, ndipo bodi ya huko inakufungia kwa muda usipigane nchini humo ili kuangalia afya yako,” alifafanua Palasa akizungumzia uamuzi wa bodi hiyo.

Mbabe alichapwa na Simpson bondia wa nyota tatu ambaye hana rekodi ya kupigwa katika mapambano 14 tangu 2019 alipoingia kwenye ngumi za kulipwa, kati ya hayo 10 ameshinda kwa KO.

Mbabe bondia namba tatu kwa ubora nchini anayemiliki nyota moja na nusu ni wa 215 kati ya 1541 duniani kwenye uzani wa super middle.