Kelvin John apewa jezi ya nahodha Stars

Muktasari:

  • Kelvin ambaye hakupata nafasi ya kucheza mchezo wa kwanza wa FIFA Series 2024 ambao Taifa Stars ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Bulgaria, ameonakana kwenye maandalizi ya kuivaa Mongolia akifanya mazoezi na jezi hiyo

Mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji, Kelvin John kwa mara ya kwanza amepewa jezi namba 10 kwenye timu ya taifa 'Taifa Stars' ambayo imekuwa ikivaliwa na nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Samatta.

Kelvin ambaye hakupata nafasi ya kucheza mchezo wa kwanza wa FIFA Series 2024 ambao Taifa Stars ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Bulgaria, ameonakana kwenye maandalizi ya kuivaa Mongolia akifanya mazoezi na jezi hiyo.

Mshambuliaji huyo ambaye alifungiwa vioo na kocha, Adel Amrouche ambaye kwa sasa yupo matatani baada ya kufungiwa na CAF kutokana na utovu wa nidhamu, ameongezwa kikosini Stars na kocha Hemed Suleiman 'Morocco' ambaye anakaimu nafasi hiyo kwa sasa.

Kutokana na kutokuwapo kwa Samatta kwenye kikosi hicho ambacho leo Jumatatu saa 10:00 jioni kwa Afrika Mashariki kitavaana na Mongolia huko Azerbaijan, ndio sababu ambayo Kelvin amepewa namba hiyo ya jezi ambayo amekuwa akipenda kuivaa tangu akiwa katika timu za vijana chini ya miaka 17 na 20.

Katika kipindi hiki cha mechi za kimataifa za kalenda ya FIFA, Samatta aliomba kutoitwa kwenye kikosi hicho jambo ambalo liliafikiwa na kaimu kocha mkuu ambaye aliamua kumuongeza kwenye kikosi hicho, Kelvin.

Kilichotokea kwa Kelvin na jezi ya Samatta kinafanana na kile kilichotokea kwa nyota wa Braga Armindo Bangna (Bruma) ambaye ameandika historia ya kuivaa jezi Na.7 ya timu ya taifa ya Ureno ambayo imevaliwa na supastaa wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo tangu mwaka 2007.

Ronaldo ambaye hajajumuishwa kwenye kikosi cha Ureno cha kocha Roberto Martinez kilichokabiliana na Sweden kwenye mchezo wa kirafiki wa ushindi wa mabao 5-2, ameivaa jezi hiyo kutokana na Ronaldo kuomba asijumuishwe kikosini kwa ajili ya mchezo huo.

Kelvin anavaa jezi ya mtu ambaye aliwahi kuishi naye KRC Genk nchini Ubelgiji ambako mara kadhaa walijirekodi video wakipiga tizi pamoja.