Samatta, Msuva vita ya rekodi Afcon

Muktasari:

  • Taifa Stars inashiriki kwa mara ya tatu katika fainali za Afcon ikiwa tayari imeshafanya hivyo mwaka 1980 na 2019.

Dar es Salaam. Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazoanza Jumamosi hii huko Ivory Coast ni fursa nzuri kwa Mbwana Samatta na Saimon Msuva kuvunja au kuifikia rekodi inayoshikiliwa na Mrisho Ngassa ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.

Ngassa aliyewahi kuzichezea Yanga, Simba na Azam kwa nyakati tofauti aliifungia Taifa Stars mabao 25 ambayo ni mengi zaidi kuliko mengine yaliyowahi kufungwa na mchezaji mmoja akiwa na jezi ya timu ya Taifa.

Mabao hayo ya Yanga aliyafunga katika mashindano tofauti ambayo Taifa Stars ilishiriki kama vile yale ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia na kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Samatta ambaye ndiye nahodha wa Taifa Stars hivi sasa, ana nafasi kubwa ya kuifikia ama kuvunja rekodi hiyo ya Ngassa kwa vile ametanguliwa kwa mabao matatu tu.

Samatta ameifungia Taifa Stars mabao 22 ambayo yanamfanya ashike nafasi ya pili katika chati ya wafungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars.

Wakati Samatta akishika nafasi ya pili, Msuva yeye anashika nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars kwenye mashindano tofauti akiwa amepachika mabao 21.


Katika chati hiyo ya wafungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars, John Bocco anashika nafasi ya nne aliwa na mabao 16 na anayeshika nafasi ya tano ni Nteze John aliyefunga mabao 12.

Hata hivyo Samatta na Msuva hawatokuwa na kibarua rahisi cha kuifikia au kuvunja rekodi ya Ngassa kutokana na ubora na uzoefu wa timu ilizopangwa nazo kundi F kwenye mashindano hayo.

Taifa Stars imepangwa pamoja na Morocco ambayo mwaka jana ilifika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia, DR Congo ambayo imewahi kutwaa ubingwa wa Afcon mara mbili na kuna Zambia ambayo iliwahi kuchukua taji la mara moja.

Katika fainali za Afcon mwaka huu, Taifa Stars itaanza kucheza na Morocco, Januari 17, Januari 21 itacheza na Zambia na itafunga dimba dhidi ya DR Congo, Januari 24.