Kisa cha Onana, Benchikha Simba

Hatimaye sababu ya kocha wa Simba Abdelhack Benchikha kumzuia Willy Esomba Onana kupiga penalti imefahamika.

Juzi usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Simba ilivaana na KVZ kwenye mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Muungano na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, lakini gumzo ilikuwa ishu ya penalti ya dakika za mwisho.

Mshambuliaji wa Simba Pa Omary Jobe alichezewa madhambi na beki wa KVZ dakika za nyongeza za mchezo huo na mwamuzi kuamuru Simba ipige mkwaju wa penalti.

Baada ya Simba kupata penalti hiyo, Onana aliuchukua mpira na kwenda kuutenga ili apige mkwaju huo, lakini Benchikha alinyanyuka kwa hasira kwenye kiti akipiga kelele na kuonyesha ishara ya kutokubaliana na ishu hiyo, huku akionyesha kidole kwa beki wa pembeni Israel Mwenda, kuwa ndiye anatakiwa kupiga.

Baada ya tukio hilo, Onana kinyonge aliuacha mpira ambao ulipigwa na Mwenda na kuukwamisha wavuni akiiandika Simba bao la pili na kwenda fainali.
Chanzo cha ndani kutoka Simba kimesema kuwa, siyo Mwenda wala Onana ambao ni machaguo ya kupiga penalti kwenye timu hiyo ndiyo maana mwalimu akachagua mtu wake.

“Unajua utaratibu hapa ni watu watatu mmoja anatakiwa kupiga penalti kwa kuwa ndiye chaguo la kocha, mtu wa kwanza kwetu ni Saido Ntibazonkiza, wa pili ni Clatous Chama ambao wote hawakuwepo uwanjani muda ule.

“Lakini wa tatu ambaye kwetu anaweza kupiga penalti au kuchagua mtu wa kupiga ni nahodha ambaye wakati ule alikuwepo Mohamed Hussein, na unaona kulikuwa na mazungumzo kabla Onana hajachukua mpira, lakini mwalimu akagoma,” kilisema chanzo hicho cha uhakika.

Katika mchezo huo uliokuwa wa kwanza wa michuano hiyo baada ya kupita miaka mingi, bao la kwanza la Simba lilifungwa kwa ustadi mkubwa wa Freddy Michael kipindi cha kwanza.

Chanzo hicho kinaendelea kusema kuwa Benchikha alimchagua Mwenda baada ya beki huyo kuonyesha uwezo mkubwa wa kupiga penalti kwa siku za hivi karibuni.
“Unakumbuka hata mechi tuliyotolewa na Mashujaa, Israel alifunga mkwaju wa penalti tena alipiga kisasa sana, kuanzia pale Mwalimu alimuamini na hata mazoezini amekuwa akimpa nafasi mara kwa mara apige.

“Lakini kwenye mchezo huohuo, Onana alipiga penati dhaifu kipa akadaka, nafikiri tangu pale mwalimu alianza kupoteza Imani na Mcameroon huyo kwa upande wa penalti,” kilimalizia chanzo hicho.

Akizungumza ishu hiyo, Mkuu wa Idara ya Habari Simba Ahmed Ally, alisema ni ukweli kwamba kocha hakutaka Onana apige penalti ile kutokana na ubora wa Mwenda kwa sasa.

“Kilichotokea ni kitu cha kawaida kabisa, kocha hakutaka Onana apige penalti kwa kuwa kwa wale waliokuwa uwanjani, Mwenda alionekana kuwa bora zaidi na hata mazoezini amekuwa akifanya vizuri.

“Hili ni jambo la kawaida kwenye soka wala halina shida kubwa, jambo zuri ni kwamba timu imekwenda fainali, mimi nipo Dar nasubiri mechi ya Ligi ya Wanawake ikimaliza nakwenda Zanzibar,” alisema Ahmed. Simba itacheza fainali jumamosi na mshindi kati ya Azam na KMKM.