Lazima wawili watoke

Muktasari:

  • Michezo ya kwanza ya hatua hiyo ilishuhudia wimbi kubwa la mabao yaliyotinga nyavuni jambo ambalo linaonyesha kuwa hata leo na kesho hali inaweza kuwa hivyo hivyo.

Barcelona, Hispania, Mechi za pili za Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali zinapigwa leo na kesho kwenye viwanja tofauti na lazima timu mbili ziage mashindano.

Michezo ya kwanza ya hatua hiyo ilishuhudia wimbi kubwa la mabao yaliyotinga nyavuni jambo ambalo linaonyesha kuwa hata leo na kesho hali inaweza kuwa hivyo hivyo.

Jumanne iliyopita kulikuwa na mechi za kibabe, kuanzia sare ya 3-3 kati ya Real Madrid na mabingwa watetezi Manchester City au ile ya sare ya 2-2 kati ya Arsenal na Bayern Munich uwanjani Emirates.

Haikushia hapo, Jumatano kukawa na burudani nyingine matata kabisa, Barcelona ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Paris Saint-Germain na ile ya Atletico Madrid kuruhusu bao la dakika za mwisho kwenye ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya miamba ya Ujerumani, Borussia Dortmund.

Timu hizi zinatarajiwa kurudiana wiki hii, ambapo leo kutakuwa na mechi mbili ambazo zitazipitisha timu mbili kwenye nusu fainali.

Borrusia Dortmund ambayo ilipoteza ugenini kwa kuchapwa mabao 2-1, leo inarudi nyumbani kujiuliza upya ikitakiwa kupata ushindi wa mabao 2-0, ili iweze kufuzu hatua ya nusu, jambo ambalo litaifanya Atletico ilinde kile ilichonacho na kama itafanikiwa kupata sare basi itafuzu moja kwa moja.

Dortmund imekuwa na kiwango kizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, ikianzia kwa kuongoza kundi lililokuwa na timu ngumu kama za PSG, AC Milan na Newcastle United na kwenye 16 bora iliichapa PSV Eindhoven.

Atletico inataka kurudia makali yake ya nyuma, ambapo ilifika fainali mara mbili na kupoteza zote hizo kwa mahasimu wao Real Madrid. Kocha wao bado ni yule yule wa tangu kipindi hicho, Diego Simeone.

Mambo ni mengi. Kocha Xavi Hernández alishtua wengi Januari alipotangaza kwamba atang'atuka mwisho wa msimu huu kutokana na timu kufanya vibaya, lakini tangu wakati huo wachezaji wa miamba hiyo wameamua kukiwasha na kucheza soka la kiwango cha juu linaloweza kubadili mawazo ya kocha huyo. Barca imecheza mechi 13 na haijapoteza tangu Xavi alipotangaza huu ni mwaka wake wa mwisho kwenye kikosi hicho.

Kufika nusu fainali itakuwa hatua kubwa kwa timu hiyo kwa sababu haijafanya hivyo tangu msimu wa 2018-19. Lakini, pia litakuwa na msaada mkubwa kwenye uchumi wao, watakuwa wamejiongezea Euro 12.5 milioni za zawadi.

Mbele yao imesimama PSG, ambayo itahitaji kiwango bora kutoka kwa supastaa wao, Kylian Mbappe, ambaye kwenye mechi iliyopita, alishindwa kulenga lango katika mashuti yake matatu aliyopiga, huku pia akipoteza mipira mara 13 na kunaswa ameotea mara tatu.

Leo timu hiyo inafanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa inalinda ushindi wake iliyoupata ugenini au inaendeleza moto kwa kuibuka na ushindi dhidi ya timu hiyo ya Ufaransa.