Mtanzania Gabriel Geay achemka Boston Marathon

Muktasari:

  • Geay mwenye rekodi ya marathon ya taifa, mwaka 2023, alimaliza wa pili na kupata medali ya fedha katika mbio hizo kwa saa 2:06:04, mwaka huu ameshindwa kutamba na kujikuta akikosekana kwenye 10 bora.

Arusha. Wakati raia wa Ethiopia,Sisay Lemma akivunja rasmi utawala wa Mkenya, Evans Chebet katika mbio za Boston Marathon ambazo zimemalizika jioni hii nchini Marekani, mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay ameshindwa kufurukuta.

Geay mwenye rekodi ya marathon ya taifa, mwaka 2023, alimaliza wa pili na kupata medali ya fedha katika mbio hizo kwa saa 2:06:04, mwaka huu ameshindwa kutamba na kujikuta akikosekana kwenye 10 bora.

Sisay Lema alimaliza wa kwanza kwa muda wa 2:06:17 akifuatiwa na Mohamed Esa kwa 2:06:58, wote kutoka Ethiopia.

Bingwa mara mbili mfululizo wa mbio hizo mwaka 2022 na 2023 Evans Chebet, kutoka Kenya mara hii naye amekubali kutimuliwa vumbi la maana na kumaliza wa tatu kwa muda wa saa 2:07:22.

Hellen Obiri mshindi wa medali ya fedha ya Olimpiki mara mbili katika mbio za mita 5000 ametetea tena taji lake baada ya kushinda kwa upande wa wanawake.


Obiri ametumia muda wa 2:22:37 akifuatiwa na Wakenya wenzake Sharon Lokedi ambaye amemaliza wa pili kwa 2:22:45 na Edna Kiplagat kwa 2:23:21 huku Waethiopia wawili Buze Diriba kwa 2:24:04 na Senbere Teferi kwa 2:24:04 wakifunga tano bora.

Geay sasa atarudi Tanzania kujipanga na mashindano ya Olimpiki ambayo yatafanyika Paris Ufaransa mwezi Julai mwaka huu.