Mvua yatishia uwepo wa Ligi Kuu

Muktasari:

  • Jumanne wiki hii, ilishuhudiwa mchezo baina ya JKT Tanzania dhidi ya Yanga ukiahirishwa muda mfupi kabla ya kuanza kutokana na hali ya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kutokuwa nzuri.

Mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali hapa nchini, zimeonekana kutishia kutibua ratiba ya michezo ya Ligi Kuu Bara.

Jumanne wiki hii, ilishuhudiwa mchezo baina ya JKT Tanzania dhidi ya Yanga ukiahirishwa muda mfupi kabla ya kuanza kutokana na hali ya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kutokuwa nzuri.

Uwanja huo uliopo Mbweni, Dar es Salaam, ulijaa maji hali iliyowalazimu wasimamizi wa mchezo huo kuuahirisha, ukapigwa kesho yake Jumatano na kumalizika kwa suluhu.

Licha ya uwanja huo kutumika, lakini Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alionekana kutoridhishwa na uamuzi huo akisema ilipaswa uahirishwe kwani uwanja haukuwa vizuri.

“Kupata alama moja kwenye Uwanja kama ule ni kitu kizuri tu kwangu, unawezaje kushinda kwenye uwanja kama ule? Sijui ni maamuzi gani haya yamefanyika,” alilalamika Gamondi.

“Huwezi kucheza mpira wa kuvutia kwenye Uwanja kama ule, tunaona soka la Tanzania linapiga hatua ni jambo zuri, lakini Uwanja kama huu unakwenda kuiweka wapi heshima hiyo, kwa nini ilazimishwe mechi kuchezwa pale ingekuwa sawa hata kusogeza mechi mbele au kuhamishwa kupelekwa Uwanja mwingine,” alisema Gamondi.

Ukiachana na Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, viwanja vingine ambavyo vipo hatarini zaidi kuathiriwa na mvua pindi ikinyesha kwa kiwango kikubwa ni Manungu uliopo Morogoro, CCM Kirumba (Mwanza), Sokoine (Mbeya) na Nyankumbu (Geita).

WENYE VIWANJA WANASEMAJE

Mwenyekiti wa JKT Tanzania ambao ni wamiliki wa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Godwin Ekingo alisema wanachokifanya ni kutekeleza mambo yote ya msingi yanayohitajika ili uwanja wao uendelee kutumika katika kila mechi zao za nyumbani kwani fahari yao kubwa ni kucheza hapo.

“Mwanzoni tulikuwa tunatumia Uwanja wa CCM Kambarage kule Shinyanga kwa michezo yetu ya nyumbani ila baada ya kuonekana wetu wa Isamuhyo umekidhi vigezo tulirudi kwa ajili ya kuiweka timu yetu karibu na mashabiki wetu wanaotuzunguka,” alisema.

Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba, Lazaro Roman amesema kuna maboresho wameyafanya ambayo mvua ya kawaida ikinyesha mechi zinachezeka, lakini kama yakija mafuriko, hali itakuwa tete.

“Mechi ya Singida na Yanga mvua ilinyesha sana takribani saa tatu kabla ya mchezo kuanza lakini haikufanya mechi iahirishwe, uwanja wetu una mfumo wa kutoa maji uwanjani labda mvua iwe ya mafuriko ambayo hayawezi kuzuilika,” alisema Roman.

“Lakini kwa mvua hizi za kawaida bado uwanja wetu hauwezi kupata changamoto yoyote na kusababisha mechi kuahirishwa. Hata mechi iliyopita watu wengi walitegemea mechi ingeahirishwa lakini mechi haikuwa hivyo baada ya maji kuondoka uwanjani kwa haraka.”

KAULI YA BODI YA LIGI

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Steven Mguto, alisema ni mapema sana kuzungumzia suala hilo ingawa wao wanachotambua viwanja vyote vilivyopitishwa vimekidhi matakwa na ndio maana vinatumika kwa michezo mbalimbali.

“Suala la kufungia kiwanja linatokana na kutokidhi kwa mahitaji yanayohitajika na tunapata taarifa kutoka kwa wakaguzi wetu, tutakuwa na kikao hivi karibuni, hivyo tutakapopata ripoti kutoka kwao ndipo tutachukua hatua,” alisema.