Simba Queens yaichapa Yanga Princess

Simba Queens imeendeleza ubabe wake mbele ya Yanga Princess baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Wanawake uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Simba Queens ambao ni vinara wa ligi hiyo, walianza kuandika bao dakika ya 49 kupitia Aisha Mnunka, baada ya kipindi cha kwanza timu kwenda mapumziko matokeo yakiwa 0-0.

Jentrix Shikangwa akaongeza la pili dakika ya 66 na kuifanya timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 2-0, kabla ya Mnunka kupigilia msumari wa tatu dakika ya 90+2. Bao la Yanga Princess lilifungwa na Kaeda Wilson dakika ya 90+5.

Ushindi huo umeifanya Simba Queens kufikisha pointi 34 ikiendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi 12, huku Yanga Princess ikisalia nafasi ya tatu na pointi zake 21 nyuma ya JKT.

Ikumbukwe kwamba, katika mzunguko wa kwanza, pia Simba Queens iliichapa Yanga Princess mabao 3-1 na hivyo kushinda nyumbani na ugenini.
Baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba Queens, Juma Mgunda, alisema:

"Tunamshukuru Mungu tumepata alama tatu, hakuna mechi rahisi, baada ya hapa tunakwenda kucheza dhidi ya bingwa mtetezi JKT Queens, tutajiandaa kupambana nao."

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Haalubono Charles, alisema:

"Nawapongeza Simba kwa kushinda, tulifanya makosa ambayo yametugharimu na tumepoteza mchezo huu, tunakwenda kujiandaa upya kwa michezo iliyobaki."