Simba vs Ahly.. Simba heshima, Al Ahly rekodi

Muktasari:

  • Licha ya kuwa ni mechi ya kwanza kuwania kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu, lakini itakuwa ya heshima zaidi kutokana na rekodi za timu hizo mbili ambazo rangi yao asili ni nyekundu.

Dar es Salaam. Leo ndio ile siku iliyosubiriwa kwa hamu na wadau wa soka Afrika kushuhudia mechi ya mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Al Ahly kutoka Misri, mchezo utakaopigwa kuanzia saa 3:00 usiku, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Licha ya kuwa ni mechi ya kwanza kuwania kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu, lakini itakuwa ya heshima zaidi kutokana na rekodi za timu hizo mbili ambazo rangi yao asili ni nyekundu.

Simba ambao ni wenyeji imekuwa na rekodi bora inapokuwa katika Uwanja wa Mkapa kwa miaka ya hivi karibuni, kutokana na matokeo ambayo imekuwa ikiyapata.

Wekundu hao wa Msimbazi wamedhihirisha hilo hata mbele ya wapinzani wao wa leo Al Ahly ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo kwani wamefika kwa Mkapa mara nne jumla kucheza na Simba na mara zote wameondoka bila ushindi.

"Simba ni timu imara nafikiri kila mmoja anafahamu kuwa hatujawahi kuifunga hapa kwa Mkapa, tunakwenda uwanjani kwenye mchezo mwingine mgumu kwa timu zote," alisema Hossam Ghally Mkuu wa Msafara wa Alhy.

Kwa miaka ya hivi karibuni, timu hizo mbili zimekutana mara sita kwenye michuano ya CAF, ambapo kila moja imeshinda mara mbili ikiwa nyumbani kwake na kupoteza mara mbili ikiwa ugenini huku mechi mbili za mwisho zote zikimalizika kwa sare.

Mechi hizo ni zile za michuano mipya ya African Football League (AFL), ambapo mchezo wa kwanza uliopigwa kwa Mkapa Oktoba 30, mwaka jana, ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 yale ya Simba yakifungwa na Kibu Denis na Sadio Kanoute huku kwa Al Ahly yakiwekwa nyavuni na Reda Slim na Kahraba Mahmoud na mechi ya marudiano ikapigwa Cairo Misri na kumalizika kwa sare ya mabao 1-1 yaliyofungwa na Kahraba na Kanoute kwa Simba.

Kutokana na rekodi hizo, kila timu leo itakuwa ikisaka heshima ambapo Simba inataka kushinda ili kuendeleza ubabe mbele ya Al Ahly ikiwa nyumbani huku Ahly ikitaka kushinda ili kuvunja mwiko wa kutoshinda kwa Mkapa kwa kipindi chote.

Aidha Simba itakuwa ikitaka heshima ya kuvuka robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu baada ya kugota hapo mara nne katika misimu mitano iliyopita.

Pia Al Ahly itataka heshima ya kuendelea kutawala soka la Afrika kwa kuvuka hatua hiyo na kutetea taji lake ililolitwaa kwa mara nyingi zaidi kwenye historia ikifanya hivyo mara 11.

Kocha Mkuu wa Simba Abdelhak Benchikha alisema mechi hiyo ni ya heshima kwao na wanataka kushinda nyumbani ili kurahisisha kazi ugenini.

"Ni mechi ngumu lakini tupo tayari kupambana, tunataka kushinda nyumbani ili kuweka heshima lakini pia iwe chachu ya kufanya vizuri zaidi kwenye mechi ya marudiano itakayopigwa Cairo siku chache zijazo," alisema kocha huyo ambaye msimu uliopita akiwa na US Alger aliichapa Ahly bao 1-0 kwenye fainali ya CAF Super Cup na kutwaa taji hilo.

Marcel Koller, kocha mkuu wa Al Ahly alisema itakuwa ni mechi ngumu ambayo itahitaji kujitoa zaidi kwa wachezaji wake ili kupata kile wanachokitaka.

"Ni mechi inayohitaji kujitoa zaidi. Timu zote zinahitaji ushindi hivyo tutacheza kwa tahadhari tukiwaheshimu wapinzani wetu, uzuri tunafahamiana," alisema Koller.

Wakati Simba itamtegemea zaidi Saido Ntibazonkiza ambaye amehusika kwenye mabao manne ya michuano hiyo msimu huu, Ahly itakuwa ikitegemea ubora wa Hussein El Shahat ambaye amehusika kwenye mabao matatu.

Katika mchezo huo, Al Ahly itawakosa baadhi ya nyota wake muhimu wakiwemo viungo Emam Ashour na Aliou Dieng wenyewe majeraha huku kwa Simba nayo ikimkosa kipa Aishi Manula.

Baada ya mechi hiyo timu hizo zitakutana tena Aprili 5, mwaka huu jijini Cairo kwenye mechi ya mkondo wa pili ambapo mshindi wa jumla atatinga hatua ya nusu fainali.

Simba itaingia kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kushinda mechi tatu mfululizo za ligi huku Ahly ikiwa imepoteza mechi moja kati ya tatu za mwisho za ligi ilizocheza.

Mechi sita zilizopita 


Oktoba 24, 2023 Al Ahly 1-1 Simba

Oktoba 20, 2023 Simba 2-2 Al Ahly

April 9, 2021 Al Ahly 1-0 Simba

Februari 23, 2021 Simba 1-0 Al Ahly

Februari 12, 2019 Simba 1-0 Al Ahly

Februari 2, 2019 Al Ahly 5-0 Simba.