Kampuni matatani madai ya mtalii kula hadharani Zanzibar

Muktasari:

  • Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT) imeitoza faini ya Dola za Marekani 500 sawa na Sh1.3 milioni Kampuni ya utalii ya Organisateur Francophone Tours and Travel kwa madai ya kuruhusu wageni kula hadharani tofauti na miongozo.

Unguja. Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT) imeitoza faini ya Dola za Marekani 500 sawa na Sh1.3 milioni Kampuni ya utalii ya Organisateur Francophone Tours and Travel kwa madai ya kuruhusu wageni kula hadharani tofauti na miongozo.

Kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na kamisheni hiyo Machi 7, 2024, ulielekeza wafanyabiashara wanaopewa leseni kuhusu masuala ya utalii kuzingatia maadili na kuheshimu tamaduni za mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na ZCT imesema kawaida unapofika mwezi mtukufu huwa wanatoa miongozo na maagizo ya kufuata katika biashara za utalii ili kuheshimu taratibu na sheria zilizopo.

ZCT imesema kutokana na kitendo kilichodaiwa kufanywa na kampuni hiyo, wameitoza kiasi hicho cha fedha kutokana na kukiuka maagizo hayo.

Mbali na kuitoza faini, imemsimamisha kazi mwongoza watalii kwa kipindi cha miezi mitatu asifanye kazi hiyo.

Baadhi ya wananchi wamekuwa na maoni tofauti, wengine wakiunga mkono na wengine kudai ipo haja ya kuangalia vyema utaratibu huo.

Mohmud Issa, amesema hatua hiyo inastahili kupongezwa kwani kwa kipindi kirefu Zanzibar inajulikana wakati wa mwezi mtukufu watu hawaruhusiwi kula hadharani.

Wakati Issa akisema hayo, Yahya Daudi amesema ipo haja ya kuangalia vyema utaratibu huo kwani kila mtu ana imani yake, hivyo suala la kumlazimisha mtu asile hadharani ni jambo linaloleta utata.